March 13, 2023

SERIKALI YAWASILISHA MAPENDEKEZO YA UKOMO WA BAJETI 2023/2024


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta jambo na Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azan Zungu na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), baada ya kuwasilishwa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, ukumbi wa Pius Msekwa, bungeni jijini Dodoma.

 

 

Serikali imewasilisha kwa wabunge Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, ambapo imepanga kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trililion 44.3.

 

Bajeti hiyo inajumuisha shilingi trilioni 29.2 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 15.1 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. 

 

Akiwasilisha mapendekezo hayo jijini Dodoma Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alisema kiasi hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 7.0 ikilinganishwa na bajeti iliyoidhinishwa na Bunge ya mwaka wa Fedha 2022/23 ya shilingi trilioni 41.5.

 

Alisema jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 31.4, sawa na asilimia 70.7 ya bajeti yote ambapo kati ya mapato hayo, mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 13.0 hadi shilingi trilioni 26.7 kutoka makadirio ya shilingi trilioni 23.7 mwaka 2022/23.

 

Misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo inatarajiwa kufikia shilingi trilioni 5.4, sawa na asilimia 12.3 ya bajeti yote”, alisema Dkt. Nchemba.

 

Dkt. Nchemba alisema Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 5.4 kutoka soko la ndani ambapo shilingi triioni 3.5 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na shilingi trilioni 1.9 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

 

Alisema Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 2.1 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu.

 

Kuhusu mgawanyo wa matumizi, Dkt. Nchemba alisema kuwa kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 29.2 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikijumuisha shilingi trilioni 12.8 kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali na gharama nyingine za Mfuko Mkuu na shilingi trilioni 10.9 kwa ajili ya mishahara ikiwemo upandishaji wa madaraja kwa watumishi na ajira mpya, na shilingi trilioni 6.4 kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC).

 

“Matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 15.1 ambapo kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 11.9 ni fedha za ndani, sawa na asilimia 78.3 ya bajeti ya maendeleo na shilingi trilioni 3.2 ni fedha za nje”, aliongeza.

 

Dkt. Nchemba alisema kuwa ukomo wa fedha za maendeleo upo ndani ya wigo wa kati ya asilimia 30 na 40 ulioanishwa kwenye Mpango Elekezi wa Muda Mrefu (2011/12 – 2025/26) ambapo utengaji wa fedha za maendeleo umezingatia miradi inayoendelea ikiwemo miradi ya kimkakati na ya kielelezo pamoja na utekelezaji wa miradi kupitia utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kugharamia miradi ya maendeleo kwa utaratibu uliozoeleka.

 

Aidha, bajeti ya matumizi ya kawaida imeongezeka kufuatia kukamilika kwa miradi ya maendeleo hususan kwenye sekta za huduma za jamii ambazo kwa sasa zinahitaji fedha za matumizi ya kawaida kwa ajili ya uendeshaji”, alibainisha Dkt. Nchemba.

 

Alisema katika mwaka 2023/24, Serikali inatarajia kuongeza ukusanyaji wa mapato, ili kugharamia sehemu kubwa ya matumizi yake na kuendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Namba 11 ya Mwaka 2015 pamoja na sheria nyingine kwa lengo la kubana matumizi na kuelekeza fedha kwenye utekelezaji wa vipaumbele vilivyoainishwa.

 

Dkt. Nchemba alisema utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24 pamoja na Mfumo na Ukomo na Bajeti ya mwaka 2023/24, unatarajiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati, kuimarisha sekta za uzalishaji ili kutoa mchango zaidi katika ukuaji wa uchumi, kuongeza mapato ya Serikali, fursa za ajira na maendeleo ya watu na nchi kwa ujumla na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za kijamii kama vile elimu, afya, maji, barabara n.k.

No comments:

Post a Comment

Pages