HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 25, 2023

TMA yaongoza vikao kutathimini ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, na Afisa Kiungo wa Tanzania katika Jopo la IPCC (kulia) akiongoza kikao cha kamati ya jopo hilo (Contact Group) katika mkutano wa 58 wa IPCC (IPCC 58) uliofanyika Interlaken, Uswiss kuanzia tarehe 13 hadi 18 Machi, 2023. Aliyeketi kushoto kwake ni Bi. Tina Christensen (Mwenyekiti mwenza) kutoka Denmark.



Na Mwandishi Wetu, Interlaken, Uswisi


KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’a, ambaye pia ni Ofisa Kiungo wa Tanzania katika Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na  TMA yaongoza vikao kutathimini ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi (Intergovernmental Panel on Climate Change - IPCC), ameongoza vikao vya kamati ya jopo hilo katika mkutano wa 58 wa IPCC uliofanyika Interlaken, Uswisi kuanzia Machi 13 hadi 18, 2023.


Jopo la IPCC lilikutana kwa lengo kuu la kuidhinisha Taarifa ya Sita ya Tathmini ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi.


Utaratibu wa kuidhinisha taarifa za tathmini za IPCC uhusisha kamati ambazo huteuliwa kufanya mapitio ya maeneo maalumu katika rasimu ya taarifa na kutoa mapendekezo.


Kwa upande wake, Dk. Chang’a, aliteuliwa kuongoza kamati ya kuidhinisha  “Sehemu A” ya taarifa hiyo akishirikiana na Bi. Tina Christensen kutoka Denmark. 


Sambamba na kuongoza kamati hiyo, Dk. Chang’a alitoa mchango wa kitaalamu wa sayansi  ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kwa Tanzania katika taarifa hiyo kwa manufaa ya nchi yetu na hivyo kuitangaza vyema Tanzania kimataifa. 


Katika hatua nyingine, Dk. Chang’a alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Korea (Korean Meteorological Adminstration – KMA), kuhusu ushirikiano na TMA katika masuala ya hali ya hewa ambapo kiongozi huyo alisema  KMA iko  tayari  kupanua wigo wa ushirikiano na TMA. 


Miongoni mwa maeneo ambayo walikubaliana KMA na TMA kushirikiana ni matumizi ya mifumo ya kiditajitali katika uandaaji wa utabiri wa hali ya hewa,ufungashaji na usambazaji wa taarifa za hali ya hewa.  


Aidha, Dk. Chang’a alikutana na kufanya mazungumzo na Bi. Shirley Matheson ambaye ni Mratibu wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (Worldwide Fund for Nature –WWF) na kujadiliana kuhusu WWF kushirikiana na TMA katika masuala ya hali ya hewa na tabianchi.


IPCC ni Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi liloanzishwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataif. 


Jopo hilo linaundwa na nchi zote wanachama wa WMO kupitia wataalamu ambao ni Maafisa Viungo (Focal Points) wanaowakilisha nchi zao katika Jopo hilo. 


Kwa Upande wa Tanzania, TMA imepewa dhamana ya kuiwakilisha Tanzania katika masuala hayo ambapo Afisa Kiungo wa Tanzania ni Dk. Ladislaus Chang’a. Jukumu la Msingi la IPCC ni kutumia tafiti mbalimbali zinazohusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi na kuandaa taarifa za Tathmini ambazo ni muhimu katika kutoa maamuzi ya sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi. 


Tangu Jopo hilo lianzishwe mwaka 1988 limefanikiwa kutoa taarifa tano za tathmini.


No comments:

Post a Comment

Pages