Wazazi na walezi wametakiwa kuwasimamia watoto wanapokwenda kusherehekea Skukuu ili kuwalinda na wanaofanya matendo mabaya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla ametoa wito huo alipojumuika na waumini wa Masjid Kauthar Fuoni Mambosasa katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.
Amesema ili kuwaepusha watoto na matendo ni vyema kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanafuatana na wakubwa wao ambao wataweza kuwasimamia wanapokwenda viwanja vya kufurahikia Skukuu.
Ameeleza kuwa kuwasimamia watoto kutaweza kudhibiti vitendo vilivyo nje ya Maadili ikiwemo kufanya matendo maovu pamoja na kwenda sehemu zisizo na maadili.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kipindi chote cha skukuu ni vyema wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanavaa mavazi yenye staha kwa mujibu wa utamaduni wa kizanzibari.
Aidha Alhajj Hemed amewakumbusha waumini kuhakikisha wanatekeleza wajibu wa kutoa Zakatul Fitry ili kutakasa funga zao na kuwasaidia wahitaji kuweza kusherehekea Eid wakiwa na furaha jambo ambalo litaongeza mapenzi baina yao na kutekeleza maelekezo ya Mtume Muhammad (S.A.W).
Pamoja na hayo amewasisitiza wauminii kuendelea kufanya Ibada kama walivyofanya katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Aidha Mhe. Hemed amesisitiza wajibu wa kila mwananchi kulinda amani na utulivu uliopo nchini hatua ambayo itasaidia kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar pamoja na kukaribisha wawekezaji.
Akitoa Khutba katika Sala hiyo Shekh Shukuru Ramadhan Fadhil ameeleza kuwa ni vyema kwa waumini kufanya mema yaliyoamrishwa na Allah Mtukufu pamoja na kuacha yote yaliyokatazwa ili kutafuta Radhi zake.
Ameeleza kuwa miongoni mwa sababu za kukosa baraka na Rehma kutoka kwa Allah ni kukithiri kwa maasi ambapo amewanasihi waumini kurudi kwa Allah Mtukufu ili neema zizidi Nchini.
No comments:
Post a Comment