HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 14, 2023

Mkazi Babati atwaa Bodaboda ya Kwanza 'NMB Bonge la Mpango - Moto Ule Ule'


 

 Mkuu wa Idara ya Mauzo ya Mtandao wa Kibenki NMB, Donatus Richard (katikati), akizungumza na mshindi wa droo ya kwanza ya Bonge la Mpango – Moto Uleule iliyofanyika Makao Makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, ambapo mkazi wa Babati mkoani Manyara, Stella Mafuwe alijishindia Bodaboda. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi Benki ya NMB, Aikansia Muro na kulia ni mwakilishi kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Elibariki Senga Senga.  (Na Mpiga Picha Wetu).

Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi Benki ya NMB, Aikansia Muro (kushoto), akizungumza na Deocles Mushemo Muganyizi aliyejishindia shilingi 200,000 katika droo ya kwanza ya Bonge la Mpango – Moto Uleule iliyofanyika Makao Makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam. Kulia ni mwakilishi kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Elibariki Senga Senga na katikati ni Mkuu wa Idara ya Mauzo ya Mtandao wa Kibenki NMB, Donatus Richard.  (Na Mpiga Picha Wetu).

 

 

NA MWANDISHI WETU


DROO ya kwanza ya msimu wa Tatu wa Kampeni ya Weka Akiba na Ushinde na Benki ya NMB 'NMB Bonge la Mpango - Moto Ule Ule,' imefanyika Alhamisi hii, ambako washindi 12 wamejinyakuliwa zawadi zenye thamani ya Sh. Mil. 5, kati ya Sh. Mil. 180 zinazoshindaniwa katika wiki 12 za kampeni hiyo, huku Stella Meleck Mafuwe wa Babati mkoani Manyara akijinyakulia Bodaboda.


NMB Bonge la Mpango ilizinduliwa Machi 29 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Paulo Chacha, chini ya kaulimbiu ya 'Moto Uleule - #Hatupoi', ikilenga kuhamasisha uwekaji akiba, kurejesha kwa jamii sehemu ya faida yake, huku pia ukiwa ni mkakati wa NMB kuendelea kuwa chaguo la kwanza la wateja kwa usalama wa fedha zao pamoja na uhakika wa huduma bora za kibenki.


Mkuu wa Idara ya Mauzo ya Mtandao wa Kibenki wa NMB, Donatus Richard, ndiye aliyechezesha droo hiyo ya kwanza, iliyofanyika Makao Makuu ya NMB, jijini Dar es Salaam, ikisimamiwa na Afisa wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Elibarik Sengasenga, ambaye kwa niaba ya bodi aliipongeza NMB kwa uratibu mzuri na kukidhi matakwa ya kisheria na kikanuni wakati wa uendeshaji wa droo za kampeni hiyo kwa misimu miwili iliyopita.


Ukiondoa Stella Mafuwe wa Babati aliyetwaa Bodaboda, naye Deocles Mushemo Muganyizi ambaye ni mteja wa NMB Tawi la Kenyatta Road jijini Mwanza, alijishindia pesa taslimu kiasi cha Sh. 200,000, huku washindi wengine 10 wakijinyakulia Sh. 100,000 kila mmoja.


Akizungumza kabla ya droo hiyo kuchezeshwa, Donatus alizitaja zawadi nyingine za kampeni hiyo kuwa ni pesa taslimu Sh. Mil. 5, friji la milango miwili, 'smart tv' (inchi 55), 'smartphone' aina ya iPhone 14 Pro Max na Samsung Z-FLIP, pikipiki za mizigo (za matairi matatu aina ya Skylark) na kompyuta malaria 'laptop' kwa washindi wa kila mwezi na wale wa fainali ya kuhitimisha shindano hilo.


"Jumla kuu ya thamani ya zawadi mbalimbali za 'Bonge la Mpango - Moto Uleule' ni Sh. Mil. 180 zitakazoshindaniwa na wateja wetu wote wenye akiba inayoanzia Sh. 100,000 ama wateja wapya watakaofungua akaunti nasi wakati huu na kuweka akiba inayoanzia kiwango hicho na kuendelea," alibainisha Donatus na kuongeza:


"Katika wiki 12 za Bonge la Mpango, washindi 90 watajishindia pesa taslimu Sh. 100,000 kila mmoja (washindi 10 kila wiki - sawa na Sh. Mil. 9) na mshindi mmoja kila wiki akishinda Sh. 200,000. Katika kila wiki (kwa Wiki tisa) NMB itakabidhi bodaboda moja moja yenye thamani ya Sh. Mil. 2.5 ambapo zote 9 zitakuwa na thamani ya Sh. Mil. 22.72."


Akaongeza kuwa, zawadi nyingine ni kwa wateja 10 wa droo za kila mwezi ambao watashinda bodaboda zenye thamani ya Sh. Mil. 25, huku wateja wengine 10 wa kila mwezi wakitarajiwa kujishindia pesa taslimu Sh. Mil. 1 kila mmoja (sawa na Sh. Mil. 10 kwa wote).


"Katika 'Grand Finale,' NMB itatoa pikipiki tano za miguu mitatu - thamani ya kila moja ni zaidi ya Sh. Mil. 5.5 (zote Sh. Mil. 25.55), lakini pia itakuwa fainali ambayo wateja wetu wengine watano watajinyakulia friji la milango miwili, TV, 'smartphone,' 'washing machine' na kompyuta mpakato 'laptop,' vyote vikiwa na thamani ya Sh. Mil. 14.1," alibainisha Donatus.


Kwa upande wake, Elibariki Sengasenga alitumia nafasi hiyo kutoa pongezi kwa niaba ya GBT, ambako alibainisha kuwa Bodi yake ndio yenye mamlaka ya utoaji wa leseni na vibali vya kuratibu na kuendesha michezo yote ya kubahatisha nchini, sambamba na usimamizi wa droo za Bahati Nasibu Tanzania.


Akasisitiza kuwa kwa miaka miwili, NMB imekuwa na kampeni mbalimbali zinazotoa zawadi kwa wateja wao, ambazo zimefanyika kwa kuzingatia vigezo na masharti ya GBT, huku akiwatakia kila la heri wateja benki hiyo katika ushiriki wao kwenye msimu wa tatu wa NMB Bonge la Mpango.



No comments:

Post a Comment

Pages