April 09, 2023

Mkurugenzi wa Kyem atoa msaada kituo cha watoto yatima buloma kibaha

 

Na Victor Masangu, Kibaha

KAMPUNI ya Kyem General Supplies  Limited ya Kibaha Mailimoja inayojishughulisha na masuala ya  uuzaji na usambazaji  wa vyuma chakavu  pamoja na vifaa vya ujenzi imetoa msaada wa vyakula mbalimbali kwa watoto yatima wa kituo cha Buloma Foundation kilichopo Kata ya Sofu katika Halmashauri ya Mji Kibaha.
 Msaada uliotolewa ni pamoja na mchele kilo 100,unga kilo 100, sukari ,mafuta ya kupikia,sabuni na Mbuzi mmoja ambapo lengo la msaada huo ni kusaidia watoto hao katika Sikukuu ya Pasaka.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo Josephu Mwakasyuka ,amekabidhi msaada huo leo katika hafla fupi iliyofanyika katika kituo hicho huku akisema kampuni itaendelea kutoa misaada hiyo katika makundi mbalimbali ya jamii inayoishi katika mazingira magumu.

Mwakasyuka, amesema kuwa kampuni ya Kyem inatambua kuwa watoto yatima ni jamii inayopaswa kuishi kama binadamu wengine hivyo lazima wasaidiwe katika mahitaji yao ya kila siku.

"Leo tumeona tuje kuwaona watoto yatima wa kituo hiki cha Buloma na tumewaletea vyakula mbalimbali kama vile mchele,unga,sukari,sabuni na Mbuzi mmoja ili kwa pamoja viwasaidie katika sikukuu ya Pasaka ", amesema Mwakasyuka.

Aidha, Mwakasyuka amesema kampuni imeweka mipango endelevu ya kusaidia yatima pamoja na jamii inayoishi katika mazingira magumu kama vile wajane,Walemavu na wazee bila kuangalia kabila wala dini.

Hatahivyo, Mwakasyuka amewaomba wadau wengine kujitokeza katika kusaidia watoto yatima waliopo katika kituo hicho na hata  jamii nyingine inayoishi katika mazingira magumu kwakuwa na wao wanamahitaji sawa na binadamu wengine.

Kwa upande wake msimamizi wa kituo hicho Baraka Peter, ameishukuru kampuni ya Kyem General Supplies kwa msaada huo kwani kiwango cha msaada walichotoa ni kikubwa na kitaweza kuwasaidia mwezi mzima.

Peter,amesema kituo hicho kwasasa kina watoto 46 ambapo kati yao wakiume ni 24 na wakike 22 nakusema wengi wao wanasoma Shule ya awali, Msingi , Sekondari na watoto watatu wanasoma vyuo vikuu.

"Ninatumia fursa hii kuishukuru kampuni hii kwa msaada huu mkubwa maana inawezekana mkaona ni kidogo lakini kwa moyo wa dhati mlichotoa ni kikubwa Sana na kitawasaidia watoto hawa kupata chakula cha mwezi mzima", amesema Peter

Hatahivyo , baadhi ya watoto yatima wa kituo hicho akiwemo Lilian Masawe na Yohana Almasi wameishukuru kampuni hiyo kwa hatua kubwa ya kuwakumbuka katika sikukuu ya Pasaka na kuomba wasichoke kuisaidia kwakuwa changamoto zao ni nyingi.


No comments:

Post a Comment

Pages