HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 10, 2023

BENKI YA CRDB SONGEA WAZINDUA SHINDANO LA KUTUMIA MFUMO WA KISASA WA SIM BANKING NA STEPHANO MANGO, SONGEA

 

MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Wiliman Ndile, akizungunza wakati wa uzinduzi wa zoezi la matumizi ya SimBanking.


Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Songea, Method Muganyizi, awali akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya hiyo kuhusu malengo ya benki hyo katika kuhakikisha wananchi wanatumia benki kwa mfumo wa kisasa wa Simbanking mahali popote bila kujali aina ya simu.


Na Stephano Mango


MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Wiliman Ndile amewataka wakazi wa Wilaya hiyo kutumia mfumo wa kibenki kwa njia ya kisasa kupitia simu za kiganjani (SIM BANKING)ili kupunguza changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili ikiwemo kutapeliwa fedha na watu wanaodaiwa kuwa ni vibaka.

Ndile ameutoa wito huo  wakati akizindua zoezi la matumizi ya Simbanking lililoandaliwa na Benki ya CRDB ambapo uzinduzi huo kwa kanda ya kusini umefanyika Songea Mkoani humo huku zoezi hilo likiwa limehudhuliwa na mamia ya wakazi wa Wilaya hiyo.

Mkuu huyo amesema kuwa kumekuwepo na baadhi ya changamoto kwa Wananchi wanapohitaji kutumia account zao za benki ambapo wengine wanalazimika kutembea umbali mrefu kuifuata huduma ya kibenki jambo ambalo baadhi yao wamekuwa wakipatwa na matatizo ya kuibiwa na watu wajulikanao kama vibaka.

Aidha Ndile ameipongeza benki ya CRDB kwa kubuni mbinu hiyo jambo ambalo amesema litawasaidia Wananchi kupunguza changamoto ya kuibiwa fedha zao hasa katika kipindi cha uuzaji wa mazao yao ambapo wengi wamekuwa wakiibiwa msimu huo.

Kwa upande wake Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Songea Method Muganyizi awali wakati akitoa taarifa kwa mkuu wa Wilaya hiyo amesema kuwa malengo ni kuhakikisha Wananchi wanatumia benki kwa mfumo wa kisasa wa Simbanking mahali popote bila kujali aina ya simu.

Muganyizi amesema baada ya uzinduzi huo ambao unaenda sambamba na zawadi mbalimbali kwa wateja wao ikiwemo simu ya kiganjani ya kisasa (Smartphone) ambayo itakuwa inatolewa kwa mteja anayefanya mihamala mara nyingi, hiyo ni zawadi ya kila wiki,

Alieleza kuwa zawadi nyingine ni fedha taslimu zaidi ya milioni 350 kutolewa kila siku na gari aina ya Toyota Crown kila baada ya miezi miwili na gari aina ya Toyota Vanguard yenye thamani ya zaidi ya sh milion 40 itatolewa mwisho wa mwaka wakati wa kutamatisha zoezi hilo, huku akisema huduma hiyo inapatikana kwa kubonyeza *150*03# ok au SIM BANKING APP (kwa watumiaji wa simu Android au iphone)

Kwa upande wake Meneja Biashara CRDB tawi la Songea Deusdedit Robert amesema kuwa Wananchi wengi wanapata muamko wa kutumia simbanking baada ya kutambua kuwa itawarahisishia shughuli za kibenki na kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu.

Robart alisema kuwa benki ya CRDB imekuwa ikitoa huduma nyingine mbalimbali, hali ambayo imekuwa ikiwavutia watu mbalimbali kuja kujiunga nayo na kuendelea kunufaika na huduma nzuri zinazotolewa na benki hiyo

Mmoja wa Wananchi Hamis Mchopa ambaye amefungua Account kwenye Benki ya CRDB na kupatiwa elimu ya matumizi ya Simbanking amesema kuwa atawashauri na wenzake hasa wafanyabiashara wadogo (Wajasiliamali) kujiunga na mfumo huo ili kuepuka usumbufu. 

No comments:

Post a Comment

Pages