Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Sarah Mwaipopo akifungua mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuhusu sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma. Mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Cha Uongozi wa Mwalimu Nyerere Kibaha mkoani Pwani.
Na Mwandishi Wetu
WATUMISHI wapya kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu Mkuu wa Serikali wametakiwa kuwajibika ipasavyo katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi kwa kuwa hakuna haki bila uwajibikaji katika Utumishi wa Umma.
Hayo yamesemwa jana tarehe 4 Mei, 2023 na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Sarah Mwaipopo wakati akifungua mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) yenye lengo la kuwajengea uwezo kuhusu masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwemo kufanyakazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.
Ambapo amebainisha kuwa, Ofisi hiyo imekusudia kuwajengea uwezo watumishi hao katika masuala mbalimbali yanayohusu majukumu yao, haki na wajibu wao kama watumishi wa umma, Muundo wa Serikali, taratibu za utendaji kazi, maadili, nidhamu, uadilifu na ustahimilivu ambavyo vyote kwa pamoja vinapaswa kuzingatiwa ili kuimarisha utendaji kazi kwa watumishi wa umma hususan kwa ajira mpya.
Ameleza kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa matakwa ya kisheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ambpo Ofisi imeona umuhimu wa kutenga bajeti ili kufanikisha mafunzo haya muhimu yatakayowajenga na kuwapa uelewa katika masuala mbalimbali ya kiutumishi.
"Mafunzo haya yatawasaidia katika kuimarisha utendaji kazi, nidhamu na maadili ikiwa ni pamoja kuwawezesha kuepuka makosa mbalimbali ya kinidhamu na yale ya kiutumishi ambayo yangeweza kufanyika kwa kukosa uelewa ili kuweza kuyaepuka wakiwa mahali pa kazi." Amesema Sarah Mwaipopo
Aidha, amewataka watumishi wapya kujifunza na kuelewa vyema dira, dhima na misingi muhimu ambayo Taasisi imejiwekea katika utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya usimamizi wa mashauri ya madai na usuluhishi yanayofunguliwa na au dhidi ya Serikali, ndani na nje ya nchi.
"Misingi hii inahusu uwajibikaji, uadilifu, uaminifu na weledi ambayo ikitekelezwa vyema ni nguzo ya maendeleo endelevu ya nchi yetu" Amesema Sarah Mwaipopo.
Naye Francis Oswald, Wakili wa Serikali ameishukuru Ofisi kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu ambayo yatawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Mafunzo hayo ya siku mbili yamewahusisha watumishi 64 waajiriwa wapya wa Ofisi hiyo wa kada mbali mbali ikiwemo Mawakili wa Serikali 41, Maafisa TEHAMA 2, Makatibu sheria 4, Katibu Muhtasi 3, madereva 9, Watunza Kumbukumbu 4 na Afisa Usafirishaji mmoja.
No comments:
Post a Comment