.
Na Dotto Mwaibale, Singida KANISA la Moravian Jimbo la Magharibi Tabora linatarajia kuanzisha mradi wa
ufugaji wa mbuzi wa kisasa na nguruwe ili liweze kujiendesha kiuchumi. Hayo yamesemwa na Mchungaji wa Kanisa hilo Parishi ya Sabasaba Mkoa wa
Singida, Yona Ezekiel wakati akizungumza katika ibada ya Sikukuu ya Vijana
iliyofanyika May 14, 2023 kanisani hapo. "Kanisa letu linategemea kuwa na miradi ya ufugaji wa mbuzi wa kisasa
na nguruwe miradi ambayo itaendeshwa na vijana na wanawake," alisema
Mchungaji Ezekiel. Alisema Jimbo la Kanisa la MoravianMagharibi Tabora Septemba mwaka huu
wanatarajia kupokea mbuzi wa kisasa ambapo kila Parishi itapata wawili jike na
dume ambao wanufaika watakuwa vijana na wanawake. Aidha, Mchungaji Ezekiel aliwataka vijana wa kanisa hilo kujiandaa kufanya
mradi huo sambamba na ufugaji wa nguruwe ambao pia watatolewa na jimbo hilo
lengo likiwa ni kuliinua kiuchumi. Mchungaji Ezekiel akimnukuu Hayati Baba
Askofu Joseph Reuben Kalindimya kuhusu vijana katika andiko lake alilolitoa mwaka 1990
alisema vijana ni kanisa la leo na nguvu kazi ya kanisa hivyo wanakila sababu
ya kuibua miradi mbalimbali itakayosaidia kulijenga na kuwa wanategemewa
kwa mambo mengi ili kulifanya kanisa likue. Aliwataka vijana kuchukua tahadhari na mafundisho ya dini ya uzushi na
uongo ambao walengwa ni vijana kama ilivyotokea katika nchi moja ya jirani
ambapo baadhi ya watu walipoteza maisha katika misitu ya kufunga baada ya
kuelezwa ili wamfikie Yesu ni lazima wafunge wapate njaa hadi wafe. Alisema wengi wa vijana hao walikuwa ni wasomi na wengine walikuwa
wakifanya kazi kwenye mashirika makubwa ya kimataifa ambao walitakiwa kukabidhi
vitu vyao vya thamani kabla ya kuingia kwenye mfungo huo. Mchungaji Ezekiel alisema mafundisho ya namna hiyo yanatakiwa yapingwe na kukemewa
kwa nguvu zote kutokana na kuingia katika kanisa la leo. Aidha, Mchungaji Ezekiel aliwataka vijana wajitege na vitendo vya
mmomonyoko wa maadili ambavyo vimeanza kukithiri katika jamii kama ukatili wa
kijinsia, ndoa za jinsia moja na usagaji. Katibu wa Umoja wa Vijana wa kanisa hilo, Israel Mwaisela akitoa taarifa
alisema vijana walianza kuadhimisha sikukuu ya vijana mwaka 2021 baada ya kuwa
Parishi kamili mwaka 2020. Alisema maadhimisho hayo ni ya tatu tangu kuanzishwa kwa parishi hiyo nakuwa
mafanikio kadhaa waliyopata idara ya vijana ni kuhudhuria ibada na semina
mbalimbali, kuwa chachu ya maendeleo ya kanisa na kuanzisha kwaya ya vijana. Alitaja baadhi ya changamoto kuwa na idadi ndogo ya vijana na hiyo
inatokana na Parishi hiyo kuwa na vijana wachache, kukosa semina na vyanzo vya
mapato katika idara ili kusaidia maendeleo ya kanisa. Muhubiri katika ibada hiyo, Bwigane Obed Mwalwiba akinukuu neno la Mungu kutoka
kitabu cha Muhubiri 12 mstari wa kwanza alisema mkumbuke Mungu wako siku za
ujana wako na kila kijana anatakiwa kumkumbuka muumba wake kwa kuomba kila wakati akiwa bado ana nguvu na si vinginevyo. Alisema na hasitokee mtu akamdharau kijana kwa namna moja ama nyingine na
akawataka kuliamini neno la Mungu na kulitangaza na wale wenye karama
mbalimbali wawafundishe wenzao ili nao wazijue kwani zinafaida kubwa katika
kanisa. Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi wa Kanisa hilo Parishi ya Sabasaba Edward Mdaki akizungumza wakati akitoa taarifa kuhusu hatua za mwanzo za ujenzi huo baada ya kulipia gharama za kiwanja alise jana waumini wa kanisa hilo walianza kuchimba shimo la maji taka ambapo aliomba kazi hiyo ya kujitolea iendelee kwa kila muumini kushiriki. "Kila muumini kwa nafasi yake tunamuomba ajitoe kwa kazi hii ya ujenzi wa nyumba yetu ya Mungu ya kuabudia tumeanza uchimbaji wa shimo la maji taka 'choo' na baadae tutaanza ujenzi wa kanisa la muda wakati tukiendelea na maandalizi ya ujenzi wa kanisa la kudumu," alisema Mdaki. Mdaki alitumia nafasi hiyo kuwaomba wadau mbalimbali kusaidia ujenzi huo kwa kutoa chochote walichonacho iwe nguvu kazi na mahitaji mengine kama ya chakula na maji kwa ajili ya kusaidia watu wanaoendelea na kazi ya uchimbaji wa shimo la maji taka katika eneo hilo. Aliomba kwa mtu yeyote, Taasisi, Wafanyabiashara na madhehebu mbalimbali watakao kuwa tayari kuwaunga mkono katika jambo hilo kwa kutoa vifaa vya ujenzi, mchanga, matofali au fedha wanaweza kutoa kupitia Akaunti Namba 50810046663 Benki ya NMB Kanisa la Moravian Sabasaba Singida mjini au wawasiliane na Mchungaji Yona Ezekiel kwa namba 0758148508 kwani kutoa ni moyo wa mtu na sio utajiri na Mungu atawabariki na kuwaongezea kingi katika kazi zao. |
Mtumishi wa Mungu Bwigane Obed akihubiri katika ibada hiyo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa kanisa hilo, Agnes Mwaihojo akizungumza nawakina mama (hawapo pichani) wakati wa ibada hiyo.
Kwaya ya Vijana wa kanisa hilo ikitoa burudani ya nyimbo za kumsifu Mungu.
No comments:
Post a Comment