HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 10, 2023

Rais Dkt. Samia aridhia Ombi la Wakaazi wa Magomeni Kota, TBA yaweka wazi utaratibu wa mauzo ya Nyumba

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuwaongezea muda wa manunuzi, Wakaazi wa Magomeni Kota kutoka miaka 15 iliyoelekezwa na Serikali awali hadi kuwa miaka 30 ikijumuisha miaka mitano (5) ya kukaa bure.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa TBA ACRH. Daud Kondoro wakati akitoa taarifa kwa wanahabari kuhusu gharama na utaratibu wa mauzo ya nyumba za Magomeni Kota zilizopo Wilayani Kinondoni jijiji humo..


“Leo nimewaita ili niweze kuzungumza na watanzania kupitia ninyi juu gharama na utaratibu wa mauzo ya nyumba za Magomeni Kota ambazo ziligawiwa kwa wakaazi 644,” amesema ACRH. Kondoro na kuongeza,


“Kama mnavyofahamu baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzindua nyumba za Magomeni Kota mnamo Machi 23, 2022 alitoa maelekezo ya wakaazi wa Magomeni Kota kuuziwa nyumba hizo kama Wakaazi Wanunuzi bila kuzingatia gharama za thamani ya ardhi, maeneo jumuishi kama ngazi na lift pamoja na mandhari ya nje,”.


ACRH. Kondoro ameeleza kuwa awali baada ya timu ya wataalam kufanya tathmini kwa kuzingatia maelekezo ya Rais ilikuja na gharama za ununuzi wa nyumba hizo ambazo ni Milioni 48,522,913.00 kwa nyumba ya chumba kimoja na Milioni 56,893,455.00 kwa nyumba ya vyumba viwili kwa muda wa miaka 15 ya ununuzi ikijumuisha miaka 5 ya kukaa bure.


Kwamba hata hivyo baada ya wakazi wa Magomeni Kota kujulishwa juu ya gharama hizo, walimuomba Rais Dkt. Samia kuwapunguzia gharama za ununuzi wa nyumba hizo pamoja na kuwaongezea muda wa kulipia. 


“Baada ya kupokea maombi hayo, Dkt. Samia, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameridhia kuwaongezea muda wa manunuzi, wakaazi wa Magomeni Kota kutoka miaka kumi na tano (15) iliyoelekezwa na Serikali awali hadi kuwa miaka thelathini (30) ikijumuisha miaka mitano (5) ya kukaa bure,” ameeleza ACRH. Kondoro.


Amebainisha kuwa gharama na utaratibu wa mauzo ya nyumba hizo kuwa ni Nyumba ya chumba kimoja inauzwa Shilingi 48,522,913.00 na muda wa malipo ni miaka 30.

Huku Nyumba ya vyumba viwili ikiuzwa kwa Shilingi 56,893,455.00 na muda wa malipo ni miaka 30.


Kwamba baada ya kuwajulisha kwa barua wakaazi 644, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) iko tayari kuwatambua wakaazi waliotayari kutekeleza utaratibu huu wa ulipaji na kuingia nao mkataba wa mkaazi mnunuzi.


Pia amesema Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) iko tayari kuwatambua wakaazi wasiokuwa tayari kutekeleza utaratibu huu ambao wataruhusiwa kukaa bure kwa miaka mitano (5) na baada ya muda huo kukamilika, nyumba watazirejesha Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

No comments:

Post a Comment

Pages