Afisa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Singida, Hashim Mkwayu akizungumza na mawakala wa mabasi Stendi Kuu ya Mabasi Misuna wakati akitoa elimu kuhusu umuhimu wa kutoa risiti za kielektroniki kwa abiria wakati wa kampeni maalum iitwayo Tuwajibike ilioanza May 9, 2023 na kuwalenga wafanyabiashara wote.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Singida
imeendesha kampeni ya Tuwajibike yenye lengo la kuwataka wafanyabiashara na
mawakala wa mabasi kutoa risiti za kielektoniki (EFD) wanapouza bidhaa zao na
kuwakatia tiketi abiria wao chini ya kauli mbiu isemayo ukiuza toa risiti na
ukinunua dai risiti.
Akizungumza na mawakala wa mabasi Stendi Kuu ya
Mabasi Misuna Afisa Kodi wa TRA, Hashim Mkwayu alisema lengo la kampeni hiyo
imelenga utoaji wa elimu kwa mawakala wa mabasi kuhusu umuhimu wa kutoa risiti za kielektroniki kwa abiria na
kuwahimiza abiria wao kuhakikisha wanadai risiti tofauti na hapo watatozwa
faini.
Alisema TRA mkoani hapa haitasita kuwachukulia
hatua kali za kisheria mawakala wa magari ya usafirishaji abiria ambao
watabainika kutotoa risiti hizo kwa abiria na abiria ambaye atashindwa kudai
risiti.
Alisema adhabu hiyo pia itawahusu mawakala ambao watashindwa kutoa risiti kwa mizigo yote itakayokuwa inasafirishwa kwenye magari
hayo.
Alisema kampeni hiyo pia itawahusu
wafanyabiashara wote wenye maduka yanayouza bidhaa mbalimbali, maduka ya dawa,
vipodozi, chakula, wauza nyama (bucha) mahoteli, nyumba za kulala wageni, vifaa
vya ujenzi nguo na nyingine zote.
Aidha, Mkwayu alisema TRA itawachulia hatua
mawakala wanaokatisha tiketi katika vituo visivyo rasmi (Vituo Bubu) ambao
wanatoa risiti zisizo za kielektroniki kwani kwa kufanya hivyo wamekuwa
wakiikosesha Serikali mapato.
Hatua hiyo imekuja kufautia malalamiko kutoka kwa
baadhi ya mawakala hao kuhusu kuwepo kwa vituo bubu ambavyo vinasababisha mkanganyiko wa bei
wakati wa kuwaandikia risiti za kielektroniki abiria ambao wameandikiwa tiketi
za kawaida na kupelekea kutozwa faini.
Wakala wa mabasi hayo Ibrahimu Abdul alisema
vituo hivyo bubu vimekuwa ni changamoto kubwa kwao na akaomba vyombo husika Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), TRA. Polisi na Manispaa ya Singida wakae pamoja kutafuta
njia ya kuiondoa.
" Nia ya Serikali ya ukusanyaji wa mapato
ni njema kwani fedha zinazopatikana
ndio zonazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, kulipa mishahara,
kununua madawa na vifaa tiba na mambo mengine sasa haiwezekani kukawa na watu
wachache wanao tuharibia kazi kwa kukwepa kulipa kodi kwa njia za ujanja
ujanja," alisema Abdul.
Afisa Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka Mamlaka ya
Mapato Tanzania TRA Mkoa Singida Swaumu Mvungi alisema mamlaka hiyo itaanza
kuyafuatilia maeneo yote ambayo sio rasmi yanayotumika kama vituo vya magari na
kutoa risiti ambazo sio za kielekitroniki.
Alivitaja vituo hivyo kuwa ni Sabasaba, Jovena,
Namfua na Msufini na akatoa onyo kwa mawakala wanaofanya hivyo kuacha mara moja
kabla ya kufikiwa na mkono wa sheria na kuwa kampeni hiyo inafanyika katika wilaya zote mkoani hapa ambazo ni Mkalama, Iramba, Singida Manispaa,Ikungi Manyoni, Itigi na Singida DC..
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Mabasi Mkoa
wa Singida, Musafiri Ramadhani alisema jambo la kuondoa vituo bubu hivyo
liangaliwe kwa mapana kwani ni changamoto kubwa kwao.
Wakala Patrick Mgimbwa alisema jambo hilo
lisifanyiwe masihara wala kufanywa la kisiasa kwani mawakala hao wa vituo bubu wamekuwa
wakitoza nauli watoto wa jamii ya kifugaji hadi Sh.50,000 kutoka Singida hadi
Dar es Salaam na kuwa wizi huo wa mchana kweupe umepewa jina la 'Abiria zawadi
ya Mungu,
Kwa upande wake Wakala Athumani Kimwanga aliwaomba TRA wapite katika maeneo yote vilipo vituo bubu hivyo wakiwa wamevaa nguo za kawaida na kufanya uchunguzi hata kwa kujifanya ni abiria watabaini hayo yanayolalamikiwa na kuweza kuvikomesha vitendo hivyo.
No comments:
Post a Comment