August 30, 2023

Walimu waitwa MCB waepuke 'kausha damu'

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya  Mwalimu Commercial (MCB), Francis Ramadhani akiongoza kikao cha wanahisa wa benki hiyo hivi karibuni.
Mmoja wa wanahisa wa Benki ya Mwalimu Commercial (MCB), akizungumza wakati wa mkutano huo uliomalizika mjini Dodom hivi karibuni.

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

 

WALIMU wote hapa nchini wamehimizwa kuitumia Benki ya Biashara ya Mwalimu (MCB), ili kuikuza taasisi hiyo na kuondokana na mikopo ya kausha damu.

Wito huo ulitolewa hivi karibuni na wanahisa wa Benki ya Biashara ya Mwalimu (MCB), wakati wa mkutano wa saba wa wanahisa mwaka 2023 uliofanyika jijini Dodoma ukikutanisha wanahisa ambao ni walimu wastaafu na waliopo kazini.

Kwa nyakati tofauti wanahisa hao walisema walimu wengi wanadhalilika kutokana na mikopo ya kausha damu hali inayodumaza maendeleo ya kazi zao na uchumi binafsi.

Mwanahisa Mwalimu Romana Kimambo kutoka Wilaya ya Kisarawe, alisema benki hiyo ni kitega uchumi cha walimu wote hapa nchini kwa kuwa wameshiriki kuwekeza mtaji wa benki yao.

"Ndugu wanahisa, nayasema haya kwa uchungu maana tumefanyakazi nzuri ya kutafuta mtaji na kuanzisha benki yetu, lakini cha kushangaza walimu wenzetu wanachelewa kujiunga huku, wameng'ang'ania kausha damu," alisema Mwalimu Kimambo.

Mwalimu Eliud Ole Mtambala, kutoka shule ya msingi Chamwino, Manispaa ya Dodoma, alisema haoni sababu ya walimu kutumia benki nyingine wakati taasisi yao ipo na inaweza kuwavusha huku ikiwaheshimisha.

"Nina wahurumia walimu wenzangu, natoa rai wajitoe huko walikokamatika, waje MCB iwape matumaini na uhakika wa kiuchumi," alisema Mwalimu Mtambala.

Akifungua mkutano huo uliojaa wanahisa kutoka kila upande wa nchi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Mwalimu Commercial (MCB), Francis Ramadhani, alisema thamani ya benki hiyo imekuwa kutoka  sh. bilioni 30 hadi Sh. bilioni 83.

“Nataka kuwahakikishia wanahisa wote, mageuzi makubwa yanayoendelea kufanywa ndani ya benki yetu, ni ya msingi na yamesaidia kuiinua MCB hatua kwa hatua hadi mwaka 2022.

“Tumefikisha miaka saba mwaka 2022 katika utoaji wa huduma tangu benki ianzishwe, na katika kipindi hicho benki imeweza kukuza mali na thamani yake kwa zaidi ya mara mbili.

"Ninawashauri walimu waje wapitishe mishahara yao yaani wakiitumia vema benki hii nawahakikishia itakuea kubwa sana," alisema ndugu Francis.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, MCB imeongeza mapato kutoka Sh. bilioni 2.8 hadi Sh. bilioni 7.2 bilioni wakati kitabu cha mikopo kikifikia sh. bilioni 64 kutoka Sh. bilioni 16 huku  amana za wateja zikifika Sh. bilioni 60 kutoka Sh. bilioni 11 za awali.

Alisema kwa miaka saba ya uhai wa MCB imefanikiwa kufungua ofisi nane za kanda katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Arusha, Kigoma, Rukwa na Mtwara ili kuwafikia wadau kwa urahisi na mawakala wa benki hiyo kila wilaya.

No comments:

Post a Comment

Pages