August 30, 2023

STAMICO yaongeza mapato kutoka bil.1.3/- hadi bil.61.1/-

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO), limefanya mageuzi makubwa yaliyoliwezesha shirika hilo kuongeza mapato kutoka sh. bilioni 1.3 hadi sh. bilioni 61.1 sawa na ongezeko la asilimia 4425.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 28,2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, CPA Dk.Venance Mwasse katika kikao kazi kati ya shirika hilo na wahariri wa vyombo vya habari nchni chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Amesema, mafanikio hayo yameliwezesha shirika sasa kuanza kutoa gawio serikalini, kwani tangu lianzishwe mwaka 1972 lilikuwa halijawahi kupeleka gawio serikalini.

Dk. Mwasse amefafanua kuwa, sababu zilizowawezesha kufikia mafanikio hayo ni kubadili fikra, ushirikishwaji, nidhamu, kujiwekea malengo na kuyatekeleza kwa pamoja.

“Kwa ujumla, tulifikia mahali ikabidi tubadilike kifikira, kuna mashirika ya umma yanayotoa huduma na kuna mashirika ya umma yanatakiwa yajiendesha kibiashara.

“Kwa hiyo tulipoamua kujiendesha kibiashara, tukaamua sasa kwenda kuzitafuta fursa, tulipobonyeza hiyo button tukaona mambo yamekwenda.

"Na mimi kama kiongozi kwa kulitambua hili ni shirika la umma nikaona lazima tuumize vichwa, na kuongeza morali ya wafanyakazi kwa kuona wanajaliwa na mipango iwe inanyooka.

“...Pamoja na kuongeza nidhamu kwenye matumizi ya fedha za umma, tuchague sehemu sahihi, kwa sababu sehemu za kuweka fedha ni nyingi, hivyo unaangalia penye faida.

“Maendeleo huwa yanapagwa kwa hiyo, mnapopanga mambo, lazima yafanyike, mnapanga pamoja na lazima utekelezaji ufanyike, lakini kama kiongozi lazima ufanye uamuzi wenye manufaa kwa umma," alisema CPA Dk. Mwasse.

Katika hatua nyingine, Dk. Mwasse amesema, wanaendelea kungeza uzalishaji wa mkaa mbadala ili kuondoa matumizi ya mkaa unaotokana na miti na matumizi ya kuni.

“Mikakati yetu ni kuendelea kuzalisha kwa wingi ili kuendelea kuwa kimbilio na tumani kwa watumiaji wengi nchini.

Wakatio huo huo, Dk. Mwasse amebainisha kuwa, STAMICO linaendelea kufanya vizuri katika shughuli za uchorongaji madini nchini.

Amesema, ufanisi wao ndiyo umewawezesha kusaini mkataba mnono wa kuchoronga mgodi mkubwa na Geita Gold Mine (GGML) uliopo mkoani Geita.

Mkataba huo wenye thamani ya sh. bilioni 55.2 ulitiwa saini Machi 27,2023.

Dk. Mwasse amesema, mkataba huo ni uthibitisho kuwa watanzania wanaweza kushiriki kikamilifu katika kandarasi zinazotokea katika mnyororo wa thamani wa madini nchini.

Amesema, wanajivunia kufanya kazi na GGM kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu mfululizo wakishirikiana vizuri.

“Kwa hiyo tutaendelea kuimarisha tasnia ya uchorongaji, mradi ambao sisi ni kinara hapa nchini.

Kwa mujibu wa CPA Dk. Mwasse STAMICO imejipanga kuwaendeleza na kuwarasimisha wachimbaji wadogo.

“Tumeweka jicho letu kipekee hapa, tutaendelea kuwapa mafunzo na kubwa zaidi tutahakikisha benki ya wachimbaji inaanzishwa ili kuondoa changamoto ya wachimbaji, mpaka sasa hivi hakuna benki ya wachimbaji.

“Kwa hiyo tunaamini pamoja na kuwaunganisha na benki mbalimbali, lakini wakiwa na benki yao itakuwa mkombozi kwao.”

Hata hivyo, Dk. Mwasse amesema, kupitia mipango na mikakati thabiti ya shirika hilo wanatarajia ifikapo mwaka 2025, shirika liwe linajitegemea.



No comments:

Post a Comment

Pages