September 04, 2023

12 wakamatwa kwa kuficha mafuta

Na Selemani Msuya


MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imekamata wafanyabiashara 12 wanaojihusisha na kuficha mafuta na kufungia vituo viwili kwa miezi sita kwa vitendo hivyo.


Aidha, EWURA imesema inafanyia uchunguzi vituo vya  mafuta 10 ambavyo vinadaiwa kuhusika na kufanya hujuma ya mafuta na iwapo vitabainika kukiuka masharti ya leseni vitachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufungiwa miezi sita.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andilile wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, ambapo ameweka bayana kuwa hatasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa mtu au kampuni itakayobainika kuhujumu biashara hiyo.


Dk Andilile amesema katika operesheni ambayo wamefanya baada ya kuibuka malalamiko ya kuadimika mafuta ya dizeni na petrol wameweza kubaini vituo vya Camel Oil Msamvu Morogoro na Matemba mkilichopo Turiani wilayani Mvomero mkoani humo vilikuwa vinaficha mafuta, hivyo vimefungiwa miezi sita.


Amesema jana walifunga kituo cha mafuta kilichopo mkoani Tabora kinachomilikiwa na Kampuni ya GBP na kwamba watafunga vituo vingine iwapo havitauza mafuta, huku taarifa zikionesha wana mafuta ya kuuza miezi minne.


“Uchunguzi wa EWURA umebaini kuwa kuna baadhi ya wauzaji wa mafuta kwa jumla, wameonekana wana mafuta kwenye maghala, lakini hawauzi kwenye vituo. Mfano mmoja ni Kampuni ya GBP ambayo ina leseni ya jumla lakini vituo vyake havina mafuta,” amesema.


Mkurugenzi huyo amesema pia wamebaini baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakichukua mafuta na kuchelewesha kufikisha vituoni, huku wengine wakiwa na mafuta lakini hawauzi.


Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Petroli, Sura Namba 392, EWURA imepewa jukumu la kudhibiti masuala ya mafuta pamoja na mambo mengine kuhakikisha mafuta yanapatikana muda wote, hivyo wawezi kufumbia macho mtu yoyote ambaye atashiriki kuhujumu biashara hiyo.


“Sio kwamba nawatisha, sheria inatupa nguvu na tunaisimamia ipasavyo, hatovumiliwa mtu yoyote ambaye atakuwa kikwazo katika biashara hii, asichukuliea biashara huria, wakaona kuwa wapo huru kufanya wanavyotaka, hii haikubaliki, biashara ya mafuta ni uchumi,” amesema.


Dk Andilile amesema EWURA imejiridhisha kuwa nchi ina mafuta ya kutosha katika maghala na kwenye meli ambazo zinasubiria nafasi ya kuingia kwenye gati na kushusha mafuta.


“Meli zilizowasili ni MT.Ellie Lady yenye takribani lita milioni 58 za dizeli kwa ajili ya matumizi ya hapa nchini na iliwasili Agosti 29, 2023 na imeanza kushusha Septemba 3 hadi 10 mwaka huu.


MT.Emma Grace yenye takribani lita milioni 17.2 za petroli, iliwasili Agosti 28 mwaka huu, inatarajia kuanza kushusha mafuta Septemba 10 hadi 12,” amesema.


Mkurugenzi huyo amesema meli ya MT.High Tide yenye lita trilioni 22.3 za petrol, iliwasili Agosti 28 mwaka huu inatarajiwa kuanza kushusha mafuta Septemba 12 hadi 16 mwaka huu.


Dk Andilile amesema mafuta yaliyopo kwenye maghala na kwenye meli yatakidhi mahitaji ya siku 19, huku akisisitiza kuwa meli zitaendelea kuingiza mafuta hadi Oktoba 31 mwaka huu kulingana na mpangilio ulioanishwa kwenye zabuni ya uingizaji mafuta kwa pamoja (BPS) zilizofanyika Agosti 31, 2023.

No comments:

Post a Comment

Pages