September 06, 2023

NMB yabainisha mikakati ya kuwakwamua wakulima wadogo

Na Mwandishi Wetu
 
Wakulima wadogo wana mchango mkubwa katika kuhakikisha utoshelevu na uhakika wa chakula nchini jambo ambalo Benki ya NMB imeahidi kuendelea kulifadhili na kuliunga mkono kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
 

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwenye Mkutano Mkuu wa Mifumo ya Chakula ya Afrika (AGRF) 2023, Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Bi Ruth Zaipuna, mbali na utayari huo alibainisha pia jinsi taasisi hiyo inavyoshirikiana na kuwasaidia wakulima hao kupitia huduma na suluhisho mbalimbali za kifedha.
 
Aidha, kiongozi huyo wa NMB alisisitiza umuhimu wa taasisi za fedha kuchangia kuwawezesha wakulima wadogo kiuchumi. Bi Zaipuna alisema pia kuwa ujio wa mifumo ya kidijitali umesaidia sana kuondoa vizingiti vilivyokuwa vikiwakwaza wakulima kuweza kukopa kwa urahisi na kupata huduma nyingine za kifedha.
 
“Taasisi za fedha bado zina kazi ya ziada katika kuwakwamua wakulima wadogo kiuchumi, wengi wao wakiwa wanazalisha kwa ajili ya kujikimu tu huku wakiishi katika umaskini uliokithiri,” alibainisha wakati wa mjadala wa jinsi sekta binafsi inavyoweza kuwasaidia wakulima hao kuongeza utoshelevu wa chakula na usalama wa lishe barani Afrika.
 
Mjadala huo uliandaliwa na OCP Africa kwa kushirikiana na Fertilizer Canada pamoja na baraza la biashara duniani linalojihusisha na maendeleo endelevu (WBCSD). Mkutano huo wa siku nne, unalenga zaidi kujadili mabadiliko ya mifumo ya chakula na kuhakikisha uhakika wa chakula kwa watu wote barani Afrika.

Akizungumzia mchango wa taasisi kubwa za fedha kama NMB katika kuwawezesha wakulima wadogo wa Afrika kiuchumi, Bi Zaipuna alisema kuwafadhili ni suala la msingi kutokana na umuhimu wao kiuchumi na katika maendeleo ya sekta ya kilimo.
 
Takwimu zinadhibitisha umuhimu huo kwani wao ni asilimia 90 ya wakulima wote katika nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara na ni wazalishaji wa asilimia 80 ya chakula chote kinachopatikana katika eneo hili.
 
Kwa mujibu wa Bi Zaipuna, ugumu wa upatikanaji wa huduma za kifedha umekuwa kikwazo kikubwa kwa wakulima wadogo kuweza kufikia uwezo wao wa kiuchumi, changamoto ambayo NMB inapambana kutatua kupitia jitihada mbalimbali.
 
Juhudi hizo ni pamoja na kubuni suluhisho bunifu za fedha kidijitali, programu maalumu za kuwajengea uwezo wakulima pamoja na kampeni za uhamasishaji kama ile ya Teleza Kidijitali ambayo Bi Zaipuna alisema ni promosheni ya mwaka mzima inayoendelea nchini kote sasa hivi.


 
"NMB tunaamini kwa dhati kwamba kuwashirikisha na kuwajumuisha kifedha wakulima wadogo ni njia sahihi ya ustawi wao na kuwakwamua kutoka katika lindi la umaskini,” aliwaambia washiriki wa mjadala huo.


Akifafanua, kiongozi huyo alisema hii inatokana na ukweli kwamba upatikanaji wa bidhaa na huduma nafuu za kifedha  - kama vile akiba, mikopo na bima - ni njia muafaka ya kusaidia kuboresha maisha ya wakulima hawa.
 
Kuhusu jinsi NMB inavyowasaidia kujikwamua kifedha na kiuchumi, Bi Zaipuna alisema benki hiyo inaendelea kuwekeza kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma zake kwa kutanua mtandao wa matawi yake na kuongeza idadi ya mawakala pamoja na huduma za kidijitali.
 
NMB pia imekuwa ikibuni bidhaa mpya na za kisasa pamoja na suluhisho zinazozingatia na kukidhi mahitaji na matakwa ya wateja wakiwemo wakulima wadogo. Bi Zaipuna alisema tafiti zinaonyesha kuwa wengi wao wamekuwa hasa wanakwama kupata ufadhili jambo ambalo linapelekea wengi kukopa kutoka kwenye vyango visivyo rasmi hususani ndugu, jamaa na marafiki.
 
Katika kutatua changamoto hiyo, benki hiyo imeanzisha huduma ya Mshiko Fasta inayowawezesha wateja kukopa hadi TZS 500,000 kwa kutumia simu za mkononi, alifafanua.
 
Kama sehemu ya kutekeleza ajenda ya ujumuishaji kifedha, NMB imekuwa inafungua akaunti mpya za wateja milioni moja na laki mbili kila mwaka hatua ambao Bi Zaipuna alisema inasaidia sana kuwajumuisha wakulima kwenye mifumo rasmi ya huduma za kifedha.


No comments:

Post a Comment

Pages