September 30, 2023

Agizo la Rais Samia laanza kufanyiwa kazi


Waziri wa  Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ,Mohamed Mchengerwa
akizungumza wakati wa Kikao cha Kujadili Utekelezaji wa Maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan  kuhusu Ushirikishwaji wa Halmashauri katika kugharamia Miradi na shughuli za Ulinzi na Usalama. Kushoto  ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni.Kikao hicho kilichoshirikisha Jeshi la Polisi na Wataalamu kutoka TAMISEMI kimefanyika  Ofisi ndogo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

 

  Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wamekutana katika Kikao Maalum lengo ni kujadili utekelezaji wa agizo la  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kuhusu Ushirikishwaji wa Halmashauri katika kugharamia Miradi na shughuli za Ulinzi na Usalama, agizo ambalo lilitolewa Septemba 4, mwaka huu wakati wa Hafla ya Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

 

Kikao hicho kilichohusisha viongozi wa juu wa wizara hiyo huku kikihudhuriwa na wataalamu kutoka Jeshi la Polisi na kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI kilitanguliwa na wasilisho fupi kutoka Jeshi la Polisi juu ya hali ya Vituo vya Polisi nchini ambapo ndipo msingi wa utekelezaji wa agizo la Rais ili kuweza kuzishusha huduma za kipolisi chini kwa wananchi na kudhibiti uhalifu unaotokea katika sehemu mbalimbali nchini.

 

Akizungumza katika kikao hicho Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema sasa ni wakati sahihi kuanza kujadili maelekezo ya Rais Samia na hili jambo linahusisha wizara hizi mbili na sisi tushaanza kupokea fedha na tayari askari wako mafunzoni kwa ngazi ya nyota moja  na wakitoka watakua tayari kwenda kata zote nchi

ni.

‘Kama ambavyo mnafahamu malengo ya Mheshimiwa Rais ya kupeleka serikali kwa watu, sasa kwa kutumia dhana hiyo hiyo sisi tunalipeleka Jeshi la Polisi, kumekua na malalamiko mengi ya wananchi wakati mwingine ya kubambikiwa kesi, lakini yakiwepo mahusiano mazuri itapelekea kupata taarifa mbalimbali za uhalifu, sasa kutimiza azma hiyo mheshimiwa Rais ameamua kuchukua hatua  na mojawapo ni kutupatia fedha za kupandisha vyeo askari kwa ngazi ya nyota moja na hivi sasa zaidi ya askari mia mbili wanaendelea na mafunzo na tutawatawanya katika kata zote, lakini pia ametoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa pikipiki ambazo zitaenda kwa askari kata hao.’ alisema Masauni.

 

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amesema ni muhimu kufanya kazi na kumsaidia Rais Samia na maelekezo yanayotolewa na Amiri Jeshi Mkuu ni muhimu kutekelezwa ili dhana ya kupeleka ulinzi na usalama kwa wananchi kule chini iweze kutendeka.

 

‘Wizara yetu hii ni wizara yake mwenyewe Rais, kwahiyo akitoa maelekezo huko inakua tayari na sisi ashatupa maelekezo sasa hapa ni kuona kwa namna gani tunaweza kuanza utekelezaji wa maelekezo na leo tumeshapata taarifa hii ya takwimu na baada ya hapa makatibu wakuu na timu za wataalamu kutoka pande zote mbili za wizara watakaa kujadili na kuona tunaenda vipi mbele ili kukidhi vile vigezo ambavyo mheshimiwa Rais anavitaka.’ Alisema Mchengerwa.

 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Jeshi la Polisi imesema maeneo mengi yenye idadi kubwa ya watu na makazi yanakabiliwa na upungufu wa vituo vya polisi hali inayopelekea kuwepo kwa tishio la ulinzi na usalama huku vituo vilivyopo ni 485 tofauti na mahitaji halisi ya vituo 1752.

No comments:

Post a Comment

Pages