September 24, 2023

GAMONDI KULA SAHANI MOJA NA MSONDA, MZINZE, KONKONI

NA JOHN MARWA

 

WAKATI wapenzi na mashabiki wa klabu ya Yanga wakiamini wana kibarua kidogo katika mchezo wa mkondo wa pili wa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) dhidi ya Al Merreikh ya Sudan, Kocha Gamondi aahidi kula sahani moja na washambualiaji wake.

 

Gamondi pamoja na benchi lake wameingia kazini kuwanoa washambuliaji wake kuelekea mchezo huo licha ya kuwa Yanga inamtaji wa mabao (2-0) waliyoyapata ugenini, watakuwa wenyeji wa mchezo huo wa marudiano utakaochezwa katika Uwanja wa Azam, Chamazi kuanzia saa 1:00 usiku.

 

Katika mchezo wa kwanza ambao ulichezwa Jumamosi iliyopita Uwanja wa Pele, Kigali nchini Rwanda, Yanga ilishinda mabao 2-0, yaliyopachikwa kambani na Kennedy Musonda na Clement Mzize.

 

Wakati wakiana maandalizi ya kuendea mchezo huo Kocha Miguel Gamondi, amesema kikosi chake kimeanza mazoezi jana jioni huku akihitaji safu yake ya ushambuliaji inayoongozwa na Musonda, Hafiz Konkoni, Mzize na wengine kuongeza umakini.

 

Amesema wanatambua kama wanamchezo mgumu mbele yao, lakini wanahitaji mabao mengi kuhakikisha wanaweka rekodi katika michuano hiyo.

 

"Tunahitaji mabao mengi zaidi katika mchezo ujao maana kila timu inahitaji ushindi katika hatua hiyo kuweza kufuzu hatua ya makundi.

 

"Wenzetu walipoteza mchezo wa kwanza, naamini wanaporudi uwanjani tena watarudi kivingine kuhakikisha wanapata ushindi, tunatakiwa kwenda kupambana kuweza kupata matokeo," alisema kocha huyo raia wa Argentina.

 

Ameongeza kuwa, ataomba uongozi kumtafutia timu iweze kucheza nayo mchezo wa kirafiki kuweza kuona ubora wa washambuliaji wake kabla ya kurudiana na Merreikh.

 

Kocha huyo amewaomba mashabiki wa Yanga kujaa uwanjani siku ya Jumamosi, kuwapa sapoti wachezaji waweze kufanya vizuri katika mchezo huo.

 

Yanga imefika hatua ya kuwania kutinga makundi baada ya kushinda mabao 7-1 dhidi ya Asas FC ya Djibouti katika hatua ya kwanza ya mtoano ya mashindano hayo.

 

Msimu uliopita Yanga ilikuwa mshindi wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC), nyuma ya mabingwa USM Alger ya Algeria na kukosa taji hilo kwa kanuni ya bao la ugenini, ambapo walifungwa mabao 2-1 hapa nyumbani na wakashinda 1-0 ugenini.

 

Yanga iliangukia katika Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia kipigo cha jumla ya mabao 2-1 dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

 

 

No comments:

Post a Comment

Pages