Ufadhili mpya uliotangazwa kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa utasaidia juhudi za maendeleo ya serikali na kuwezesha uboreshaji wa huduma za umma kama sehemu ya Mpango wa USAID wa Democracy Delivers
Leo, katika hafla ya Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) "Democracy Delivers" kando ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken na Kiongozi Mkuu wa Shirika la USAID Samantha Power, kwa ushirikiano na Ford Foundation na Rockefeller Foundation, walihimiza wahisani na washirika wa sekta binafsi kuwekeza nchini Tanzania na nchi nyingine zinazopiga hatua za kidemokrasia.
Balozi wa Tanzania nchini Marekani Elsie Kanza, alijumuika pamoja na viongozi kutoka kundi la kwanza la nchi zitakazofaidika na ufadhili kutoka Mpango wa USAID ujulikanao kama Democracy Delivers ambazo ni pamoja na - Armenia, Jamhuri ya Dominika, Ecuador, Malawi, Maldives, Moldova, Nepal, Tanzania na Zambia - kujadili njia za kuelekeza rasilimali mpya ambazo zitasaidia wanamageuzi na wananchi katika nchi zao ambao wanajenga demokrasia yenye manufaa kwa wote. Mpango wa USAID wa Democracy Delivers, uliozinduliwa mwaka wa 2022 na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Blinken na Kiongozi Mkuu wa USAID Power, unalenga kuongeza msaada, rasilimali na umuhimu katika nchi zinazopitia kipindi cha fursa za kidemokrasia.
“Uhusiano kati ya watu wa Marekani na Watanzania ambao umeendelea kuwa imara kwa zaidi ya miaka 60 unatokana na maadili na matarajio ya pamoja. Lengo ni moja: Tanzania yenye amani na ustawi, ambapo wananchi wote wanaweza kutambua uwezo wao kamili na kutumia uhuru wao wa kimsingi,” alisema Mkurugenzi Mkazi wa USAID/Tanzania Craig Hart. “Tunaipongeza Tanzania na viongozi wake kwa kuanza kufanya mageuzi muhimu ya kidemokrasia yanayowapa fursa wananchi kupaza sauti, kupanua nafasi ya kiraia na uhuru wa vyombo vya habari, na kushirikiana tena na jumuiya ya kimataifa. Maboresho haya tayari yameanza kuboresha maisha ya Watanzania.”
Katika hafla ya Mpango wa USAID Democracy Delivers kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Marekani ilitangaza ahadi za kuisaidia Tanzania. USAID inashirikiana na Bunge la Marekani kutoa hadi dola milioni 5 ili kuunga mkono juhudi za Wizara ya Fedha ya Tanzania kuandaa, kutekeleza, na kudumisha mfumo wa ununuzi wa umma wa kidijitali unaozingatia uundaji wa tovuti ya manunuzi ya kidijitali. Tovuti hii itaongeza uwazi na ufanisi wa manunuzi huku ikipunguza fursa za ufisadi.
Wakati wa hafla hiyo, taasisi na makampuni makubwa ya Marekani pia yalitangaza uwekezaji ili kuimarisha mifumo ya afya, kuboresha upatikanaji wa nishati ya jua, na kusaidia maendeleo ya watoto wachanga na uwezeshaji wa vijana nchini Tanzania.
● Hilton Foundation itawekeza takriban dola milioni 8 ili kuimarisha mifumo ya afya ya msingi, maendeleo ya watoto wachanga na programu za kuwawezesha vijana nchini Tanzania.
● Tanzania ni mojawapo ya nchi nne zinazopokea dola milioni 20 kutoka kwa The Ford Foundation kusaidia upanuzi wa demokrasia. Hii ni pamoja na ufadhili wa kazi ya muda mrefu ya Ford Foundation ya kuimarisha mihimili ya demokrasia, kuongeza ushiriki wa raia, na kuendeleza maadili ya kidemokrasia kwa kukuza ushirikiano kati ya serikali na watu wa Tanzania.
● Skoll Foundation itawekeza dola milioni 16.9 ili kuimarisha mifumo ya afya na kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na Wizara za Afya nchini Tanzania na nchi nyingine tatu. Ufadhili huu utaboresha mwitikio katika kukabili majanga, kuimarisha mifumo ya afya katika ngazi ya jamii, na kubainisha ufumbuzi wa changamoto za mifumo ya afya.
● Kama sehemu ya ruzuku ya takriban dola milioni 11.2 ili kuendeleza upatikanaji wa haki, ufadhili wa jamii, na suluhisho la mabadiliko ya tabia nchi katika nchi zilizopo kwenye Mpango wa USAID Demokrasia Delivers, Mott Foundation itaonyesha mfano mzuri wa kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kwa kuboresha upatikanaji wa nishati ya jua ndani ya minyororo ya thamani ya kilimo katika jamii zilizopo katika maeneo magumu kufikiwa nchini Tanzania.
● Tanzania ni miongoni mwa nchi sita zitakazofaidika na ufadhili wa dola milioni 1.5 kutoka WINGS Foundation kuinua sekta ya uhisani kama mshirika mkuu wa serikali na watendaji wa asasi za kiraia katika mipango ya maendeleo ya ndani. Ufadhili huu unasaidia Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu na juhudi za kulinda na kukuza demokrasia.
Kwa kuweka kipaumbele katika mahitaji ya wananchi na kuimarisha uwazi na uwajibikaji, ahadi hizi zitaimarisha mipango ya mageuzi ya Serikali ya Tanzania na kuwezesha uboreshaji wa huduma za umma, ikiwa ni pamoja na kufanya maamuzi jumuishi na yanayoongozwa na wananchi. Kwa jumla, wahisani na washirika wa sekta ya binafsi wametoa ahadi za zaidi ya dola milioni 110 kusaidia nchi zilizopo kwenye Mpango wa Democracy Delivers lengo likiwa kuhimiza fursa za kidemokrasia.
USAID na washirika wake wamejitolea kuhakikisha kuwa demokrasia inaleta manufaa kwa wote. Ushahidi thabiti unaunganisha demokrasia na matokeo bora ya maendeleo. Nchi zenye Demokrasia hutoa huduma za umma kwa viwango vya juu kuliko zisizo za demokrasia, na hufanya hivyo kwa usawa zaidi. USAID inatoa wito kwa mashirika yote, biashara, na watu binafsi waliojitolea kuendeleza haki na fursa kujiunga na Mpango wa Democracy Delivers katika ubia wa mawazo na vitendo kwa kujitolea kuendeleza mageuzi ya kidemokrasia ili kuleta maisha bora.
No comments:
Post a Comment