September 28, 2023

NMB yatoa vifaa vya Mil. 40/- kwa Shule, Zahanati, Hospitali Mafia

 
Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Zephania Sumaye (wa tatu kulia), akipokea sehemu ya msaada wa vifaa tiba kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa, wakati wa kukabidhi vifaa tiba kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Mafia na Zahanati tano pamoja na madawati 100 kwa Shule ya Sekondari Kilamahewa, vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 40. Makabidhiano hayo yalifanyika katika viwanja vya hospitali hiyo, Septemba 28, 2023. 
Baadhi ya watumishi wa Serikali wakishuhudia makabidhiano hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Mafia Zephania Sumaye (kulia) akiwa na 
Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa katika hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba pamoja na madawati wilayani Mafia, Mkoa wa Pwani.
Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa, akitoa hotuba yake.
Wanafunzi wakiwa wamekaa katika madawati yaliyotolewa na Benki ya NMB kwa ajili ya Shule ya Sekondari Kilimahewa iliyopo wilayani Mafia.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Zephania Sumaye (kushoto), akipokea sehemu ya msaada wa madawati 100 kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa (kulia), wakati wa kukabidhi madawati 100 kwa ajili ya Shule ya Sekondari Kilamahewa pamoja na vifaa tiba kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Mafia, vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 40. Makabidhiano hayo yalifanyika katika viwanja vya hospitali hiyo.


NA MWANDISHI WETU, MAFIA

 

BENKI ya NMB, imekabidhi misaada mbalimbali yenye thamani ya Shilingi Milioni 40 kwa Hospitali ya Wilaya ya Mafia, zahanati tano na shule moja ya sekondari wilayani humo, ikiwa ni sehemu ya Programu ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI) inayoendeshwa na benki hiyo.

 

Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa, ndiye aliyekabidhi misaada hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Zephania Sumaye, katika hafla iliyofanyika leo Jumatano Septemba 27, kwenye Viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya Mafia, iliyopo Kilindoni.

 

Vifaa vilivyokabidhiwa na Baragomwa ni mashuka 200, skrini za kutenganisha vitanda 11, vitanda sita vya kufanyia vipimo kwa wagonjwa, pamoja na masanduku 20 ya pembeni ya vitanda ya kuhifadhia dawa za wagonjwa, vyote vikiwa ni kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya.

 

Vifaa vingine ni pamoja na mashuka 66, magodoro 60, skrini za kutenganishia vitanda 13, vitanda 13 vya kufanyia vipimo wagonjwa, na masanduku 16 madogo ya pembeni mwa vitanda vya wagonjwa kwa ajili ya zahanati tano za Kiegeani, Michueni, Kilindoni, Gonge na Kifinge.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, iliyohudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mafia, Olivanus Thomas Paul na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Kassim Ndumbo, Baragomwa aliitaja shule iliyonufaika na msaada wa madawati 100 kuwa ni Shule ya Sekondari Kilimahewa.

 

“Misaada hii yenye thamani ya Sh. Milioni 40, ni muendelezo wa sapoti zetu kupitia Programu ya Uwekezaji kwa Jamii kwenda Serikali ya Wilaya ya Mafia, ambayo Mei 11 mwaka huu tuliipa misaada ya viti 100 na meza 100 kwa Shule za Sekondari Ndagoni na Jibondo vyote vikiwa na thamani ya Sh. Mil. 15.

 

“Afya na Elimu ni sekta za kipaumbele kwa NMB, na hii ni kutokana na ukweli kuwa hizo ni msingi mkubwa wa maendeleo ya taifa lolote duniani. Tunatambua jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika upatikanaji wa elimu bora, nasi kama wadau vinara, tunawiwa kusaidia utatuzi wa changamoto zilizopo.

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Zephania Sumaye, aliipongeza NMB msaada mkubwa wa vifaa tiba na vifaa vya elimu, vinavyoenda kuongeza nguvu sahihi katika mapambano ya maadui watatu wa Taifa waliotajwa na Mwalimu Julius Nyerere, ambao ujinga, umaskini na maradhi.

 

“NMB mnafanya makubwa sana katika kupambana na maadui wa ujinga, maradhi na umaskini, ambao walitajwa na Baba wa Taifa wakati wa utawala wake na serikali inapambana kuwatokomeza. Msaada wenu huu, unaenda kugusa upungufu wa asilimia 46 wa vifaa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali.

 

“Tunamshukuru Rais Samia kwa kufanya makubwa katika afya na elimu, ambako kutokana na uwingi wa vituo na shule, uhitaji nao umekuwa ukiongezeka na hapa ndipo NMB inapochukua jukumu hili kubwa na zito kiasi cha kuifanya Serikali ya Wilaya ya Mafia ijivunie uwepo wenu.

 

“Katika Jamii za Wafugaji ninakotoka mimi, mtu hata akiwa na ng’ombe 200, yupo dume mmoja kati yao akikosekana tu zizini, tayari mwenye ng’ombe atajua, hii ni sawa na NMB, ni dume ambalo linapokosekana katika kuisapoti Serikali kutatua kero kama hizi, moja kwa moja yenyewe inajua,” alisema DC Sumaye.

 

Alimaliza kwa kusema Serikali Kuu na ile ya Mkoa na hata ya wilaya zinatambua na kuthamini mchango wa benki hiyo, ambao sio rahisi kutolewa na taasisi yoyote ya fedha nchini kutokana na ukubwa wake, huku akituma salamu kwa Afisa Mtendaji Mkuu, Ruth Zaipuna kwa kuwajali na kuwathamini wana Mafia.

 

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Omary Mvulana, akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya Idara za Elimu na Afya za Halmashauri hiyo, aliipongeza NMB kwa namna inavyoguswa haraka kila wanapowakimbilia kuomba usaidizi wa utatuzi wa changamoto walizonazo.

 

“Halmashauri yetu ina shule za msingi, zahanati na vituo vya afya kadhaa na vingi kati ya hivyo vina changamoto mbalimbali. NMB leo inapunguza asilimia tatu ya upungufu wa vifaa tiba na elimu kutoka asilimia 60 ya awali hadi asilimia 57, lakini tunao upungufu wa madawati na wadau zaidi wajitokeze kutusaidia,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages