HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 12, 2023

PROF. MBARAWA ASHUHUDIA MAKABIDHIANO MAKASHA YA UBARIDI KATI YA TRC NA

NA MAGENDELA HAMISI


WIZIRI wa Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa, ameshuhudia makabidhiano ya makasha ya ubaridi kati ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na kutoa wito kwa TRC kujipanga ili kuhimili ushindani na sekta binafsi katika usafirishaji wa mbogamboga kwa kutumia reli.


Prof. Mbarawa ameweka wazi hilo leo Septemba 11, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya makabidhiano ya makasha matano ya ubaridi kati ya TRC na WFP.


Pia amesisitiza kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa kubadilisha sheria na kanuni ili kutoa ruhusa kwa mashirika binafsi na kigeni kutumia reli kusafirisha mbogamboga kwa lengo la kusaidia wakulima kuhifadhi vema mazao yao na matunda wakati wa kusafirisha kwa kutumia makasha ya ubaridi.


 “Serikali inatoa hamasa kwa mashirika binafsi na kimataifa ambayo yanataka kuwekeza na kushirikiana na TRC  katika kufanya miradi ya kimaendeleo tutafanya hivyo na kama mnavyojua tumebadilisha sheria ya reli kwa kuleta mfumo wa ‘Open access’ itafanya kila mtu mwenye mabehewa yake kutumia reli yetu saa 24.


“Kwa sasa tunayarisha kanuni, zikikamilika tutatoa muongozo kwa kila anayehitaji kutumia reli afanye hiivyo, sekta binafsi zifanye hivyo hata Mzee Bahkresa anaweza kufanya hivyo, shughuli hii haitofanywa na TRC pekee, hivyo TRC mnatakiwa kujipanga kwani tunakwenda kufungua mabehewa yote ingawa ninaimani mnauzoefu mkubwa na mtafanya kazi nzuri,” amesema. 


Ameongeza kuwa baada ya makabidhiano hayo kukamilika ni vema TRC ikahakikisha wanayatunza ili kufanikisha kudumu kwa muda mrefu ili iwe na tija ambayo imekusudiwa ya kuwasaidia wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi kwa kutumia mabehewa yenye makasha ya kuhifadhia ubaridi kwa nyuzi joto arobaini.
Aidha amesema kuwa Selikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imeshirikiana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda kuunga mkono jitihada zinazofanywa na TRC na WFP kuhakikisha upatikanaji wa masoko, miundo mbinu ya kuhifadhia  mbogamboga na matunda pamoja na usafirishaji wa uhakika kwa gharama nafuu ili kuwezesha wakulima kunufaika na kuleta maendeleo katika nchi.


,Baada ya mchakato huo wa makabidhiano kukamilika, Prof Mbarawa amewahakikishia wadau wa kilimo na biashara kuwa wizara yake kupitia TRC itahakikisha wakulima na wafugaji wanapata huduma bora ya usafirishaji wa mazao yao kupitia reli.


Amesema Seikali inatambua vema mchango wa kilimo kwa taifa, ndio maana inaendelea kutoa ushirikiano katika shughuli hizo ili kukuza pato la nchi kwa kasi zaidi tofauti na ilivyo sasa na huduma ya kusafirisha mbogamboga na matunda itaanza katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam na baadaye katika mikoa mingine.


Naye Mkurugenzi na Mwakilishi wa WFP hapa nchini, Sarah Gordon, amesema makasha hayo ambayo wamekabidhi kwa TRC yanathamani ya Dola za Marekani 300,037 sawa na Tsh. Milioni 840 na kufafanua kuwa kupitia mradi huo kwa pamoja wataleta mageuzi katika mnyororo wa thamani wa chakula kwa kutumia vifaa vya kupoozea bidhaa za kilimo.


“Dhumuni letu ni kuwa na mnyororo baridi endelevu ambao utapunguza hasara na upotevu kwa kuongeza upatikanaji wa bidhaa zinazovunwa moja kwa moja kutoka shambani zenye virutubishi na za bei nafuu itakayosaidia kutengeneza ajira na kuboresha kipato cha mkulima na kufanya kuwa na uhakika wa chakula na lishe bora kwa wote na hilo alikiwa ni jukumu Kuu la WFP,” amesema.


Amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji 20 wakubwa duniani wa mazao ya bustani yanayovunwa moja kwa moja kutoka shambani kupitia kilimo cha bustani na ni miongoni mwa eneo linalokuwa kwa kasi ndani ya sekta ya kilimo cha taifa kinachoongozwa na wakulima wadogo wadogo
Ameongeza kuwa wakulima hao wamekuwa sehemu ya wanaowakilisha asilimia kadhaa katika kuchangia pato la taifa linalotokana na kilimo bustani ingawa inakadiriwa kuwa kati ya asimilia 30 hadi 40 hupotea katika mnyororo wa thamani kwa sababu ya ukosefu wa hifadhi ya baridi wakati wa kusafirisha.
 Gordon amefafanua kuwa kwa kuzingatia mahitaji ya huduma hiyo wanaweza kutanua mradi huo kwenda katika maeneo mengine ya nchi kwa kutumia reli ikiwemo Arusha, Moshi ,Tanga hadi Dar es Salaam, pia katika mikoa ya Mwanza – Kigoma hadi Dar es Salaam ambako kuna uzalishaji mkubwa wa kilimo cha bustani, mifugo na uvuvi.


Mkurugenzi huyo amekumbusha kuwa WFP imekuwa ikiwaunganisha wakulima wadogo wadogo na masoko tangu mwaka 2009 na mradi huo utatoa usafiri wa uhakika, salama na wa gharama nafuu kwa kuanzia kwenye uzalishaji hadi kwenye masoko na mkazo zaidi utawekwa kwa wanawake na vijana.

No comments:

Post a Comment

Pages