HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 08, 2023

Rais Samia aeleza namna sekta ya kilimo inaweza kuleta mapinduzi

Na Selemani Msuya


RAIS Samia Suluhu Hassan ametaja hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha sekta ya kilimo inafanya mapinduzi kwa wakulima wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.



Ametaja hatua hizo leo Septemba 7,2023 wakati wa mkutano wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika (AGRF) ambapo ametumia nafasi hiyo kuelezea hatua ambazo Serikali inachukua kuondoa changamoto ya masoko.


“Kuhusu masoko kuna shida katika kupatikana masoko lakini katika tafiti ambazo tumefanya tumegundua kuna mambo mawili ambayo yana utata na tunayafanyia kazi


“Jambo la kwanza ni viunganishi ambayo yatatufanya  tujue tuna kiasi gani na kinatakiwa wapi ndani na nje ya nchi ,tukijua hilo tutakuwa na usahihi wa kinachozalishwa upande mmoja kiende upande mwingine,”amesema.


Ameongeza jambo la pili ni mawasiliano ya mkulima na soko lenyewe na kwamba eneo hilo hawajafanya  vizuri bado huku akifafanua wameanza katika baadhi ya mazao kwa mfano korosho.


Amesema wameshuhudia mara kadhaa bei ya korosho ikipanda kwa sababu kuna ushirika wa mkulima na mnunuaji moja kwa moja, hivyo wamemuondoa mtu wa kati ambao walikuwa wanakwenda moja kwa moja kununua mazao shambani na wananunua kwa bei ndogo.


Rais Samia amesema walivyounganisha mkulima na mnunuzi pamoja na soko wanunuaji wananunua kwenye vyama vya ushirika vya wakulima na kwa maana hiyo wanapata muda wa kushindana bei na bei zinapanda.


“Tumeshuhudia hivi karibuni zao la ufuta kwasababu tumeingiza kwenye ushirika na tumetumia mfumo wa stakabadhi ghalani, wakulima wanapeleka mazao yao huko kwenye ushirika , wanunuaji wanashindanishwa bei inapanda,”amesema Rais Samia.


Ameongeza la kufurahisha zaidi ni katika zao la mbaazi ambalo miaka miwili, mitatu nyuma walihamasisha wakulima walime sana na wakalima lakini kwasababu hawakuwaunganisha na soko na hawakuwa na mipango mizuri mbaazi zilianguka bei sana na kuwavunja moyo wakulima


“Mwaka jana (2022) mbaazi iliuzwa kwa Sh.300 kwa kilo lakini mwaka huu(2023) wakulima wameuza kwa zaidi ya Sh.2000 kwa kilo. Sasa huu ndio mtindo tutakaokwenda nao kwenye mazao mengine pia ili kumuunganisha mkulima na soko,”amesema.


Pia amesema hatua nyingine wanayochukua amesema soko linahusu usafiri na usafiri ndio unaleta soko , hivyo Serikali imejidhatiti kujenga barabara kwa kuunganisha mikoa na mikoa , mikoa na wilaya zake lakini barabara kubwa na nchi jirani ili kufanikisha masoko ya nchi hizo.


 “Katika  barabara mwaka jana na mwaka huu tumetoa fedha nyingi sana kutengeneza barabara za ndani ya wilaya ili mazao yasikwame kwa wakulima yaende kwenye masoko


“Sio barabara peke yake tunatengeneza bandari zetu Tanzania , bandari ya Dar es Saalam, Zanzibar ,Tanga na Mtwara , zote ziweze kupokea meli zinazoweza kushusha na kuchukua mazao yetu yanayozalishwa kwenda nje na tumefanikiwa vizuri


“Pia kama mnavyoelewa tumenunua ndege ya mizigo ili isafirishe mazao hasa mazao ya matunda ambayo yanakaa kwa muda ambapo kwa ndege ile sasa tunaweza kuchukua mizigo yetu wenyewe na kuipeleka kwenye soko kuliko kutegemea kwa jirani apakie apelike


“Kwani hatujui wakati wa kupakia pengine mazao yale yale yameandikwa yametoka kwa jirani wakati yametoka Tanzania.Kwahiyo sasa ndege yetu itaweza kutusafirisha mazao yetu,”amesema.


Aidha amesema katika bandari wanajenga sehemu itakayoweza kuhifadhi mazao yanayoharibika kwa haraka yaweze kuhifadhiwa wakati yanasubiri usafiri.“Kwa hiyo tunachukua hatua zote hizi ili kumfikisha mkulima, kufikisha mazao kwenye soko.”


Pia amesema jambo lingine kubwa ambalo wanafanya hasa katika mpango wa  BBT ni kutafuta na kufanya ushirika na watu ambao watakuwa wakiongeza thamani mazao ya vijana.


“Kwa maana vijana wakilima na wakivuna kuwe na mtu anayechukua mazao yote na kuyapeleka kuyaongeza thamani kwenye viwanda vyetu yakiwa yamechakatwa. Kwahiyo hizo ndizo hatua ambazo serikali inazichukua kuimarisha soko.”


Aidha Samia amesema matumizi ya ICT na teknolojia hayaepukiki katika sekta ya kilimo kwa karne ya sasa huku akieleze jinsi inavyotumika nchini katika sekta hiyo.


Akifafanua hilo amesema kupitia mitandao na teknolojia ndio wanaweza kuwatoa  fikra vijana kwamba kulima sio kazi ngumu , hivyo teknolojia inakwenda kurahisha kilimo kwa vijana


“Sasa Tanzania tumejua kilimo ni kujua taarifa zake na kwa maana hiyo tunawekeza sana katika tafiti na katika tafiti tunafanya maeneo yote ya kilimo,uvugaji na uvuvi .


“Katika kilimo tumejielekeza sana kwanza kujua afya ya udongo lakini kabla ya kujua afya ya udongo ni kuwa na kanzi data ili kuweza kufanya vizuri.


“Kwa hiyo kwa kutumia ICT tunaendelea kusajili wakulima ,aina ya kilimo wanachofanya, eneo walionalo na mambo mengine yanayomhusu mkulima.”


Ameongeza lakini ili mkulima huyo aweze kufanya vizuri lazima wajue mkulima yuko kwenye hali gani pale alipo, kwa hiyo wamewawezesha maofisa ugani vifaa vya kupima afya ya udongo ,


“Kwa hiyo kila mkulima atakuwa anapimiwa afya ya udongo kutoka muda mmoja kwenda mwingine na kujua kwa uhalisia anatakiwa kutumia mbegu za aina gani…


“Lakini tumejiingiza katika kuongeza uzalishaji wa mbegu za kisasa , tumeimarisha vituo vya utafiti na mashamba ya uzalishaji mbegu kwa kiwango kikubwa ili wazalishe mbegu sana.


“Kwa mfano Arusha kuna kampuni ya mtu binafsi na kuna wengine nao wanazalisha mbegu.Vituo vyetu vya Serikali na vyenyewe tumeviwezesha na tunategemea ikifika 2025 labda robo tatu ya mbegu zitakazotumika kwa zizalishwe hapa nchini kama sio kujitegemea kabisa,”amesema Rais Samia.


Ameongeza na mbezu zinazozalishwa zinatambulika na zinaweza kuhimili mabadiliko  ya hali ya hewa , pia zinaenda na hali ya udongo uliopo.


Rais Samia amesema wanatumia ICT katika masuala ya umwagiliaji kwani kama itakumbukwa zamani wakisema umwagiliaji ilikuwa ni umwagilia haswa kwa maana ya kuchukua maji na kuyamwaga katika udongo ili mazao yaje kama inavyomwaga mvua.


“Sasa tunamwagilia kwa kutumia teknolojia ya kitalaam ambayo mti humwagiliwa kwa maji yanayotakiwa na muda unaotakiwa.Pia tunatumia teknolojia kujua aina ya udongo ulionao unahitaji maji kiasi hiki na sio kiasi hiki na hiyo itasaidia kufanya matumizi mazuri ya maji tuliyonayo.


“Tunakwenda kutumia ICT katika kuhifadhi mazao ya wakulima.Tunajenga  vihenge vya kisasa vinavyotumia mitambo ya kurekebisha mvuke na kuepusha tatizo la kuwa na sumu kuvu katika mazao yetu, tunakwenda kufanya hivyo kwa kutumia ICT,”amesema Rais Samia.


Amesisitiza wanakwenda kutumia ICT kwenye soko kwani lazima wajue taarifa za mahitaji ya matwaka na ugavi wa mazao yanayozalishwa ndani ya nchi.


“Hivyo  ICT haiepukiki , lakini hata teknolojia katika kutayarisha mashamba na tunahitaji kuwa na mitambo ya kisasa na ndio itakayotumika katika mpango wa BBT.”


Amesema ni vizuri kijana akajisikia fahari anapojishughulisha na kilimo na akiendesha trekta liwe la kisasa na linafanya kazi zaidi ya tatu.”Kwa hiyo ICT haiepukuki na Serikali yetu tumedhamiria kuelekea huko.”


Kwa upande mwingine Samia amebainisha baadhi ya viashiria ambavyo vitathibitisha kufanikiwa kwa mpango wa kilimo wa BBT ambao umenzshwa na Serikali yake kwa kuwapatia fursa vijana kujihusisha na kilimo nchini kupitia mpango huo .


Ametaja baadhi ya viashiria hivyo cha kwanza ni idadi ya vijana walio katika mpango huo ambao wapo zaidi ya  1200 lakini bado kuna maombi mengi kutoka kwa vijana kutaka kuingia katika huo mpango.


“Kwa hiyo  kiashiria cha kwanza ni vijana kuvutika na mpango wa BBT , lakini kiashiria cha pili kitakuwa kwa namna wanavyotumia mbolea katika kuzalisha , jinsi inavyotumika sana ndipo tutajua vijana wameelewa na wanafanya kilimo cha kisasa.


“Matumizi ya mbolea yatatupa kiashiria kwamba kuna matokeo chanya.Kiashiria kingine ni tija itakayopatikana katika kile ambacho vijana watakuwa wamehusika nacho,”amesema.


Rais Samia amesema kiashiria kingine ni soko kwa maana vijana watakavyopeleka hayo mazao sokoni na watakavyoendesha maisha yao huku akisisitiza kiashiria kikubwa zaidi ni kuona maisha ya vijana yanavyoendelea kustawi,


Ameongeza pia kufanikiwa kwa mpango wa BBT ni pale watakapoona wameshusha mfumuko wa bei ya gharama za chakula ndani ya nchi.


“Kama uzalishaji utakuwa mkubwa bila shaka bei za chakula zitashuka na kama tunavyojua mfumuko ndio unasababisha bei za chakula kupanda ndani ya nchi.


“Tukiweza kushusha mfumuko wa bei ya vyakula kitakuwa kiashiria kizuri sana kwamba vijana wanazalisha kwa wingi.”

No comments:

Post a Comment

Pages