September 06, 2023

TSB: Mashine ya kuchakata Mkonge mbioni kufika

Na Mwandishi Wetu, Tanga

BODI ya Mkonge Tanzania (TSB), imesema mchakato wa ununuzi wa mashine za kuchakata Mkonge (korona) kwa wakulima umefikia hatua nzuri ili kukopeshwa mashine hizo.

Mkurugenzi Mkuu wa TSB, Saddy Kambona amesema hatua zote zimekamilika kilichobaki ni kuwakabidhi hati ndogo ili kukamilisha taratibu za kibenki.

 
“Kwa upande wa serikali umeshaagiza korona tano, lakini upande wa wakulima ambao wanataka kununua kupitia mikopo ya benki tumeshafikia mazungumzo na Benki ya NMB tayari ngazi za juu zote tunachotakiwa sisi ni kukamilisha nyaraka ikiwamo kuwapatia wakulima hati ndogo kwa ajili ya kuwasaidia taratibu za kibenki.

“Malalamiko mengi ya wakulima yalikuwa ni kukosekana kwa mashine ya uchakataji, kwa hiyo Mkonge wa wakulima umekuwa unaharibika shambani, wanachakata Mkonge mara moja wakati wanatakiwa kuchakata mara mbili kwa mwaka lakini hata hiyo mara moja yenyewe kuna wakulima Mkonge wao hauchakatwi,” amesema Mkurugenzi Kambona.

Amesema jambo hilo limeathiri vipato vya wakulima na kupunguza kasi, nguvu na mitaji ya wakulima lakini pia inaathiri takwimu za uzalishaji ndani ya nchi kwa sababu wanalo lengo la kuzalisha tani 80,000 ifikapo 2025/26 kwa mujibu wa ilani ya chama lakini kuna lile la kuzalisha tani 120,000 2025/26 kwa mujibu wa maelekezo ya serikali.

“Kwa hiyo leo hii nilikuwa nimewaleta timu hapa kwa kushirikiana na maafisa kutoka Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Tanga kwa ajili ya tathmini kwenye hayo maeneo ili tutengeneze hizo hati ndogo ili wazitumie kwenye kufanikisha hizo taratibu za kibenki.

“Lakini ziko nyaraka nyingine ambayo ni makubaliano kati ya benki, TSB na Amcos zenyewe ili kila mmoja awe na wajibu na uhakika kwamba tunasimamia hizi Amcos kwanza inakamilisha lengo la kupata hizo korona lakini pili inakuwa na uwezo wa kurejesha ule mkopo benki kwa muda ambao tutakuwa tumekubaliana na hizo benki,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, amesema kwa upande wa benki kila kitu kiko sawa ni wao kukamilisha nyaraka hizo ambazo ndani ya wiki mbili zitakuwa tayari zimekamilisha mchakato mzima kuwasilishwa benki ili wao waendelee na mchakato wa kutoa fedha kwenye hizo Amcos ambao tayari wameshapata wazabuni kwa ajili ya kuleta mashine hizo.



No comments:

Post a Comment

Pages