September 07, 2023

AGRF yaanza kuzaa matunda


Na Selemani Msuya


WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amesema siku mbili za Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF 2023), zimeweza kuzaa matunda kwa Serikali ambapo imesaini makubaliano na nchi na mashirika ya kimataifa, ikiwemo kukubaliana na Kampuni ya Mackenzie inayoandaa Mpango wa Kilimo wa Tanzania wa 2050.



Bashe amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya mkutano huo ambao ameweka wazi kuwa zaidi ya washiriki 4,000 wameshiriki, huku wageni wakiwa ni asilimia 50 na Watanzania asilimia 50.


Amesema  leo kutakuwa na kikao cha Marais ambapo wanatarajia ushiriki wa Rais wa Senegal, Kenya, Burundi, Tanzania na zaidi ya mawaziri wa kilimo 38.


Bashe amesema lengo la Tanzania kuandaa mkutano huo ilikuwa kupata fedha za kuendeleza kilimo, ambapo lengo hilo limeweza kufanikiwa kwa wao kusaini mikataba ya makubaliano na Serikali ya Norway ambayo itatoa fedha za utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).


Waziri amesema pia wamesaini makubaliano na Marekani kuhakikisha wanakifanya kilimo kiweze kuvutia na kushirikisha watu wengi


Amesema pia wamezungumza na IFAD ambayo imesema itatoa dola milioni 60, JAICA na wengine ambapo matarajio yao ni kuhakikisha wadau wote hao wanachochea maendeleo ya kilimo.


"Mkutano huu umeanza kuzaa matunda, kwani tumeweza kusaini makubaliano na nchi na mashirika ya kimataifa ili yaweze kusaidia sekta ya kilimo ambayo ni muhimu kwa maendeleo," amesema.


Bashe amesema wamekubaliana na Kampuni ya Mackenzie ili waweze kuwatengenezea Mpango wa Kilimo wa 2050, hivyo wanaona jukwaa hilo limegusa lengo lao.


Amesema pia ushiriki wa vijana katika jukwaa hilo la mifumo ya chakula umeonesha ni namna gani kundi hilo linahitaji kushiriki katika kilimo.


Waziri Bashe amewataka Watanzania wasitarajie matokeo makubwa kwa siku za karibuni, ila matumaini yao ni kuona nguvu kubwa ambayo wanawekeza kwenye kilimo inatoa matokeo kwa siku za karibuni.


Aidha, Waziri Bashe amesema ili Afrika iweze kufanikiwa kwenye kilimo ni wakati muafaka kuungana kwa kila nchi kujikita katika eneo ambalo inaweza kuzalisha kwa wingi na ubora.


Bashe alitolea mfano Zambia ambayo inazalisha zao la Soya kwa wingi, hivyo nchi zinapaswa kushauri mashirika yanayotaka kusaidia zao hilo yapeleka misaada eneo hilo.


Amesema Tanzania ni mzalishaji mkubwa wa zao la mpunga na mazao mchanganyiko, hivyo ni vema kuwekeza nguvu kwenye eneo husika.


Waziri Bashe amesema katika kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija ni muhimu wakulima wakazingatia misingi ya uzalishaji ambayo haina madhara kwa binadamu na afya ya ardhi.


Amesema dunia inahitaji vyakula ambavyo vinazalishwa kwa kufuata misingi ya kilimo hai kutokana na ukweli kuwa ni salama kwa afya, hivyo serikali itaendelea kuweka mkazo katika eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

Pages