September 11, 2023

TUENDELEE KUMPA USHIRIKIANO RAIS WETU

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka wananchi waendelee kumuamini Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa sababu ana dhamira na malengo makubwa ya kuendelea kuboresha maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo na ya wilaya ya Ruangwa.

 

Tujenge imani ya Serikali yetu, tujenge imani na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwa anatupenda na amedhamiria kutuletea maendeleo. Hapa katika kata ya Nanganga tumejengewa shule ya sekondari iliyogharimu shilingi milioni 470, watoto wanasoma.  

 

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumapili, Septemba 10, 2023) wakati akizungumza na wananchi katika vijiji vya Mbecha, Nangumbu, Chimbila na Michenga akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo wilayani Ruangwa, Lindi.

 

Waziri Mkuu amesema Serikali imeidhinisha fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo zikiwemo shilingi bilioni 169 kujenga mradi wa maji wa Nyangao-Ruangwa ambao utanufaisha wananchi katika vijiji 34 vya Ruangwa na 12 vya Nachingwea.

 

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi waishio katika vijiji hivyo pamoja na vijiji vyote ambavyo mradi huo utapita, amewaomba wananchi hao waendelee kuwa na subira na imani na Serikali yao.

 

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha wilaya hiyo inakuwa na miundombinu bora ya barabara Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliridhia kutoa kiasi cha shilingi bilioni 69 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Nanganga-Ruangwa kwa kiwango cha lami.

 

Naye, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema Serikali imefanya maboresho makubwa katika hospitali ya mkoa wa Lindi kwa kufunga mashine ya CT Scan iliyogharimu kiasi cha shilingi bilioni mbili, hivyo imewapunguzia wananchi safari ya kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kufuata kipimo hicho.

 

Amesema mbali na maboresho hayo pia, hospitali ya Kanda ya Kusini iliyoko mkoani Mtwara nayo imeanza kutoa huduma kwa wananchi. “Badala ya wananchi kwenda kufuata huduma za rufaa Muhimbili huduma hizo watazipata Mtwara.  

 

Kwa upande wao, wenyeviti wa vijiji waliishukuru Serikali kwa jitihada zake za kuboresha huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo yao zikiwemo za afya, maji, elimu na miundombinu.  Suala la afya tupo vizuri, tuna zahanati ya kisasa na kuhusu maji wanatapa maji safi na salama,  alisema Mwenyekiti wa kijiji cha Mbecha Twalib Nandonde.

 

No comments:

Post a Comment

Pages