Na Selemani Msuya
IMEELEZWA kiwa watu milioni 283 barani Afrika wanalala njaa kila siku, hali ambayo inachangia ongezeko la utapiamlo na magonjwa yanayotokana na lishe.
Hayo yamesemwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza mbele ya washiriki wa Jukwaa la Mifumo ya Kilimo (AGRF), linalofanyika jijini Dar es Salaam tangu Septemba 5 hadi 8 mwaka huu.
Amesema Bara la Afrika lina ardhi nzuri yenye rutuba ila katika hali ya kushangaza watu wake milioni 283 wanalala njaa kila siku jambo ambalo ni la aibu na halikubaliki.
Rais Samia amewataka washiriki wa Jukwaa la AGRF, kutoka na maazimio ya namna gani nchi za Afrika zitaimarisha mifumo yake ya chakula.
Amesema changamoto zinazoikumba dunia nyakati hizi zinawafanya vijana wa Afrika kutaka mabadiliko ya sera katika sekta ya kilimo katika nchi zao ili kuwafanya wawekeze kwa ufanisi na tija.
"Afrika tumebaki kuwa walalamikaji badala ya kutoa suluhisho kutokana na utajiri wa rasilimali tulio nao, asilimia 65 ya ardhi yote inayofaa kwa kilimo ipo Afrika, tuna maji katika mito na maziwa makuu," amesema Rais Samia
Amesema viongozi wa Afrika wanapaswa kufanya tathmini ya vipaumbele vyao kulingana na mahitaji yaliyopo ili kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo na kuwa na Afrika wanayoitaka.
Rais Samia amesema Afrika imejaliwa kuwa madini mengi hivyo uwekezaji katika sekta nyingine ikiwemo kilimo.
Pia amebainisha mikakati mbalimbali ambayo Tanzania inaitekeleza katika sekta ya kilimo ikiwemo kuongeza bajeti ya kilimo.
Amesema kuanzia mwaka 2021/22 na 2023/24 bajeti ya kilimo iliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 125 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 400.
Rais Samia amesema Tanzania imedhamiria kuifanya sekta ya kilimo kuchangia asilimia 10 katika Pato la Taifa ifikapo mwaka 2030 kutoka asilimia nne ya sasa, kuyafikia masoko ya chakula ya kikanda ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kiongozi huyo amesema serikali inaimarisha miundombinu kwa ajili ya kilimo biashara ikiwemo miundombinu ya usafirshaji na nishati ili kuharakisha na kurahisisha biashara na nchi zingine,"amesema Rais Samia
Amesema katika kuonesha dhamira hiyo inafikiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezielekeza benki za biashara kupunguza riba ya mikopo ya kilimo hadi kufikia asilimia tisa.
Aidha amesema programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) waliyoianzisha inalenga kuvutia vijana wengi kwenye kilimo biashara na mwitikio umeonesha matokeo chanya
Rais Samia amesema anaamini nchi nyingine za Afrika nazo zina mikakati yake ya kuimarisha mifumo yake ya chakula kama inavyofanya Tanzania ambayo ipo tayari kushirikiana na nchi hizo.
Samia amesema serikali inatambua wadau wa kilimo ikiwemo Taasisi ya Mageuzi ya Kilimo Afrika ( AGRA) na nyingine katika kuisaidia Tanzania kuimarisha mifumo yake ya chakula.
No comments:
Post a Comment