Na Selemani Msuya
WADAU wa kilimo duniani wameunga mkono juhudi za Serikali za kufanikisha Mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT).
Wadau hao wameunga mkono juhudi hizo kupitia harambee ya kuchangia iliyoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Husein Ali Mwinyi katika Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) linaloendelea jijini Dar es Salaam.
Katika harambee hiyo wadau walioahidi ni nchi za Marekani, Ethiopia, Ofisi ya Rais ya Mfumo wa Chakula Afrika (AGRF), Benki ya Dunia, Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).
Akizungumza katika harambee hiyo Rais Dk. Mwinyi alisema, kumekuwa na utashi wa kisiasa unaokua kwa kasi Barani Afrika hususani Tanzania unaolenga kuwawezesha vijana na wanawake katika kilimo biashara, hivyo wadau hao watasaidia kuifanya BBT.
Amesema, utashi huo unaonekana kufuatia juhudi mbalimbali ikiwemo kupitishwa mikata ya tamko la mpango wa utekelezaji wa vijana, kunzishwa kwa dawati la vijana katika mpango mpya wa ushirikiano wa pamoja na uwezeshaji mpango wa BBT.
Rais Dk. Mwinyi amesema, hatua ya uwezeshaji wa mradi wa BBT utaongeza ajira kupitia mfumo wa chakula ambapo serikali imeandaa mikakati shirikishi na kutekeleza mipango ya kusaidia vijana na wanawake katika sekta ya kilimo biashara.
“Kutokana na kukua kwa mifumo ya kidigital inayosimamia mabadiliko ya uchumi wa dunia kumekuwa na ongezeko la kasi kwa vijana kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi Afrika kupitia kilimo," amesema.
Amesema hata hivyo bado kuna changamoto ya ushiriki mdogo wa vijana na wanawake katika sekta za kilimo na uvuvi kutokana na upatikanaji mdogo wa rasilimali za uzalishaji, ujuzi na ukosefu wa mitaji.
Amesema vijana wanayo hamu ya kuwekeza sehemu zenye matokeo ya haraka.
Rais Dk. Mwinyi amesema ili kufikia mafanikio yapo maeneo yanahitaji ufumbuzi ikiwemo uptikanaji wa huduma za kijamii vijijini ili kupunguza wimbi la vijana ambao wanao uwezo wa kushiriki katika kilimo kuhamia mjini.
“Pia ni mujimu kumaliza tatizo la kukosekana kwa masoko, vikwazo vya kimazingira na mabadilioo ya tabia nchi, kukosekana kwa miundombinu ya uzalishaji na kutafuta ufumbuzi katika uwekezaji wa teknolojia,”amesema.
Amesema, uwezeshaji wa vijana na wanawake katika sekta hiyo ni ufunguo wa milango ya ajira, kupunguza umaskini na chanzo cha matokeo ya uzalishaji wa chakula na ongezeko la thamani.
Rais Dk. Mwinyi amesema kutokana na hali hiyo serikali ya Tanzania imejidhatiti katika kuwawezesha vijana na wanawake kufikia malengo yao, ikiwemo kuwapo na mazingira wezeshi katika kilimo biashara.
Kwa upande wake Balozi wa Marekani nchini Tanzania Michael Battle, alisema nchi yake itaendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania katika kuboresha mifumo ya kilimo ikiwemo kuwezesha mradi wa BBT na Miradi mingine ya Zanzibar sehemu ya uchumi wa Buluu.
Amesema kwa kushirikina na taasisi za maendeleo nchini kwake hususani ya Bill and Melinda na nyingine zitaendelea kushiriki katika kukuza uchumi wa Tanzania sekta mbalimbali.
“Asilimia 25 ya bajeti ya mfuko wa maendeleo USAID unasaidia Tanzania na kwa sasa tunaenda kukaa kuangali miradi ambayo Marekani inasaidia Tanzania kwa kiasi gani inaendana na kasi inayohitaji ikiwemo kuhusisha maeneo ya kipaumbele yaliyokusudiwa na serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambayo ni kilimo, mifugo na uvuvi,”amesema.
Naye Waziri wa Kilimo Husein Bashe amesema, lengo ka serikali ni kukusanya zaidi ya dola bilioni 2 kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa BBT unaoisha mwaka 2030.
Amesema, hatua hiyo itawezesha ukuaji wa uchumi kwa kuwa kilimo kinachangia asilimi 25 ya Pato la Taifa huku asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo, kinatoa asilimia 75 ya ajira na kuchangia mauzo ya nje ya nchi kwa asilimia 85.
“Lengo la mradi wa BBT ni kujumuisha vijana zaidi ya milioni 16 katika mfumo rasmi wa kiuchumi kupitia kilimo biashara kwa kuwapa elimu na uwezeshaji,”amesema.
No comments:
Post a Comment