Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Islands of Peace Ayesega Buberwa akimuonesha Ofisa Program wa AFSA Famara Diedhiou mbegu asili.
Na Selemani Msuya
SERIKALI imeshauriwa kuweka mkazo katika kilimo hai kwa kuwa ndio kinazalisha chakula safi na salama kwa afya ya viumbe hai na mazingira.
Ushauri huo umetolewa na wadau wa kilimo hai na mbegu asili wakati wakizungumza na mwandishi wa gazeti hili kwenye mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AFS-Forum) lilifanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 5 hadi 8 mwaka 2023.
Akizungumza faida za kilimo hai, Profesa Dorcas Kibona alisema kilimo hicho ndio uhai wa viumbe hai wote na mazingira hivyo dunia inapaswa kuhamasisha kilimo hicho.
Profesa Kibona alisema hakuna uhai kama hakuna kilimo hai na kwamba eneo lolote ambalo linazalisha kwa njia ya kemikali za viwanda lina msongo wa mawazo kuanzia mimea, wadudu, wanyama na mazingira.
"Nimefanya utafiti wa ndizi Kitarasa ambayo imelimwa kwa njia ya kilimo hai matokeo yakawa mazuri sana, nikapeleka India kwa utafiti zaidi ambapo majibu yalionesha ndizi hizo zina sifa ya chakula hai.
Sikuishia hapo nilipeleka Chuo Kikuu cha Cornelia nchini Marekani ambapo maprofesa 42 wamethibitisha mazao yanayolimwa kwa njia ya kilimo hai ndio yenye faida kwa binadamu na viumbe wengine," alisema.
Kibona alisema madhara ya kutumia vyakula visivyozalishwa kwa njia ya kilimo hai ni kupata magonjwa ya kisukari, utapiamlo, shinikizo la damu na upungufu wa nguvu za kiume.
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Dorkin Organic alisema kasi ya matumizi ya vumbi la kongo, supu ya pweza na nyingine inachangiwa na vyakula vinavyozalishwa nje ya mfumo wa kilimo hai.
Alisema wanunuzi wa bidhaa za mazao kutoka nje hasa Ulaya wanataka vyakula vilivyolimwa kwa njia ya kilimo hai, hivyo ni jukumu la nchi kuhamasisha kilimo hicho.
"Kilimo hai ndio kila kitu, haihitaji kwenda darasani, hata mtu aliyeishia chekechea anajua faida ya kilimo hicho, hivyo serikali inapaswa kuweka mkazo katika eneo hili, ili kulinda afya za watu wake na mazingira," alisema.
Mtafiti huyo wa vyakula vya asili alisema yeye ana mbegu zenye zaidi ya miaka 300 na bado zina ubora uleule, hivyo anatoa rai kwa yoyote anayehitaji mbegu asili aitafute Kampuni ya Dorkin Organic.
Alisema hadi sasa wamesambaza mbegu asili kwa wakulima 3,800 katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Songwe, Mbeya, Kigoma na Katavi, huku wakiringia bei ya mazao yao katika soko.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Floresta Tanzania, Richard Mhina alisema jukwaa hilo lina muhimu katika sekta ya kilimo, ila amelishauri kuweka kipaumbele kwa wakulima wadogo wanatumia mbegu asili.
Alisema ni muhimu dunia kujadiliana namna ya kuweka mkazo kwenye mbegu asili ambazo zimeonesha wazi kuwa zina faida kwa jamii hasa kwenye kuongeza virutubisho.
"Nadhani tujikite kuboresha mbegu asili ambazo zina virutubisho moja kwa moja, kwani hizi za kisasa zinahitaji kuwekewa viini lishe, hivyo unaona kuna biashara kwa watu fulani hapo," alisema.
Alisema kilimo kinatakiwa kutoa mazao bora na sio wingi ambao unakuwa na changamoto kwa binadamu na mazingira.
Alisema Floresta wamekuwa wakihamasisha kilimo hai katika mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Arusha ambapo wakulima 15,000 wamefikiwa moja kwa moja, vikundi 600, makanisa 250 na shule 200.
Mwenyekiti wa Mwavuli wa Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Dk Mwatima Juma alisema AFS-Forum imeonesha nia ya dunia kuongeza uzalishaji, lakini lipo ombwe la namna ya kumuinua mkulima mdogo.
"Mkutano huu ni mzuri lakini umekosa ushiriki wa kundi kubwa la wakulima wadogo ambao wanajikita kwenye kilimo hai, washiriki wengi wameonesha kupigania biashara zao za mbolea na viuatilifu ambavyo vina kemikali nyingi zenye madhara kwa udongo na kuongeza mmomonyoko.
Dk Mwatima alisema Afrika inapaswa kupunguza kemikali kwenye kilimo kama sio kuondoa madhara kabisa ili binadamu wawe salama.
Naye Profesa Vara Prasad kutoka Chuo Kikuu cha Kansas State nchini Marekani alisema mbegu asili zina sifa kuu nne, uhimilivu wa ukame na jua, virutubisho, kukabiliana na wadudu vamizi na kujenga afya.
Profesa Prasad alisema iwapo dunia inataka kuondoka katika janga la maradhi kama saratani na mengine ni lazima irudi kwenye kilimo cha mbegu asili.
"Hizi mbegu za kisasa zinatupa matokeo ya muda mchache na madhara ya kudumu kwa mtumiaji, nadhani tunapaswa kurudi katika kilimo hai kwani kina faida nyingi kuliko hasara," alisema
No comments:
Post a Comment