Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Riziki Pembe Juma (kulia) akimkabidhi cheti mmoja wa washiriki wa Vijana Mtandao wa Wanawake Barani Afrika.
Na Talib Ussi
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Riziki Pembe Juma amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kuwa Jinsia na Usawa ni vipengele muhimu vya kufanikisha maendeleo endelevu nchini.
Mhe. Riziki aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifunga Kongamano la Vijana Wanawake Viongozi kutoka nchi 16 Baraza Afrika, lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Alisema masuala ya jinsia na usawa yameainishwa katika Katiba zote mbili, katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya mwaka 1984.
. Alieleza kwamba lengo la kuainishwa humo ni katika kusimamia haki na usawa na kuhimiza ushiriki wa wanawake katika kufanya maamuzi.
Pia alisema katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 imeainisha umuhimu wa Jinsia na Usawa.
Alisema katika kufanisha maendeleo hayo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum (SMT) na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (SMZ) zimeanzishwa kisheria kwa lengo la kuratibu na kusimamia masuala ya Jinsia nchini.
Aidha alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaamini kuwa elimu ni moja ya silaha muhimu hasa kwa wanawake ikiwa watakua na nia ya kufikia maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Alieleza kwamba Serikali imeweka makusudi hatua za kukuza elimu ya wasichana na kuwahimiza waendele kusoma ili wapate elimu ambapo Jamii kwa ujumla inawasaidia wasichana kuendelea na masomo badala ya kuwalazimisha kuingia kwenye ndoa za mapema.
Mhe Riziki alitoa wito kwa washiriki wa kongamano hilo kutumia jukwaa hilo kama fursa ya kujifunza mbinu bora zaidi ambazo zitafanya kuongeza uwezo wao na ujuzi.
Alifahamisha kwamba hatua hiyo itasaidia katika bara la Afrika kuhimiza vijana wa kike kuthamini elimu itakayowasaidia kupata mapato yao na kupata nafasi katika vyombo vya maamuzi.
Kongamano hilo la siku tatu limehudhuriwa na watu 100
wanawake vijana ambao ni wanachama wa harakati pamoja na Maafisa wa zamani na wanaharakati wanaoendesha mashirika ya wanawake yenye mafanikio kutoka nchi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment