March 03, 2024

BONDWA HIKING CLUB YAMUENZI HAYATI MWINYI KWA MATEMBEZI YA KM 21

Katibu wa Klabu ya Bondwa Hiking,  Agnesmwiza Ngusa akizungumza wakati wa matembezi hayo ya Kumuenzi Hayati Ali Hassan Mwinyi kwa mchango wake wa kupenda mazoezi.

Mwenyekiti wa Klabu ya Bondwa Hiking, Wakili Msomi Gabriel Mwansoho, akimueleze hayati Mwinyi namna alivyopenda kufanya mazoezi. 


Na Mwandishi Wetu, Morogoro

 

 

KLABU ya  Bondwa Hiking ya Mkoani Morogoro imefanya matembezi ya KM 21 lengo likiwa ni kuenzi mchango wa Rais wa awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Alhaji Ali Hassan Mwinyi ambae alikuwa kinara katika kuhamasha mazoezi.

 

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Klabu hiyo ya Bondwa Hiking Wakili Msomi Gabriel Mwansoho mara baada ya wanachama na viongozi hao kuweza kufanya matembezi hayo katika safu za milima ya Uluguru Mkoani Morogoro  hadi katika eneo la Morning Site.

 

Akizungumza hayo akiwa katika kanisa la mjerumani ambayo ni njia ya kuelekea morning side  wakili Mwansoho amesema kuwa klabu hiyo inatambua mchango wa hayati Mwinyi katika kupenda kufanya mazoezi ambayo yanasaidia pia katika  yanaimarisha afya ya akili.

 

“SISI kama Bondwa Hiking Club ambao tunapenda mazingira,tunapenda mazoezi,tunapenda kuimarisha afya za akili tunatambua mchango wa Mzee wetu Hayati Ali Hassan Rais wa awamu ya pili katika kupenda mazoezi na busara zake nyingi tumeona wakati anapumzishwa katika nyumba yake ya milele nasi tumsindikize kwa kufanya matembezi haya ambayo tumeanzia Manispaa ya Morogoro Gymkhana Golf Club kwa kupita njia ya Choma hadi hapa katika eneo la Morning side na kisha tutarudi kupitia njia ya kwa Mkuu wa Mkoa’’ alisema  Mwenyekiti wa Klabu ya Bondwa Hiking  Wakili  Mwansoho.

 

Katibu wa Klabu hiyo Agnesmwiza Ngusa amesema anamkumbuka Hayati Ali Hassan Mwinyi kama Rais aliyekuwa mcheshi na mwenye maneno ya busara yenye kuishi milele.

 

Aidha amesema kuwa anatazidi kuishi kwa yale aliyoyaamini hayati Mwinyi kama kuishi na watu kwa ukarimu,kufanya mazoezi pamoja na kuhakikisha wanaandika historia za maisha yao katika hadithi nzuri.

 

Nae Mratibu wa kikundi hicho George Matiku ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan,Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dakta Hussein Ali Mwinyi pamoja na watanzania kwa ujumla kwa kumpoteza mpendwa wao.

 

Hata hivyo klabu hiyo imesema itandelea kumuenzi kwa mambo yote ambayo yalisaidia kukuza uchumi wa nchi ya Tanzania.

 

Nao Baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wamesema kuwa watamkubuka Hayati Rais wa awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaji Ali Hassan Mwinyi kwa mengi ikiwemo kwa ukarimu wake na Rais aliyefanikiwa kuhudumu sehemu mbili katika nyadhifa ya urais.

 

Rais wa zamani wa Tanzania na muasisi wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, Ali Hassan Mwinyi, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 98 February 29,2024.

 

Kifo hicho kilitangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta Samia Suluhu Hassan na kusema kuwa kifo hicho kilitokea majira ya saa 11:30 jioni katika hospital ya Mzena Jijini Dar es salaam.

 

Hayati Mwinyi amezikwa March 2, 2024 huko Visiwani Zanzibar ambapo mazishi ya Kitaifa yaliongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambapo  amesema ataendelea kuyaenzi maono ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Hayati Ali Hassan Mwinyi kwa kusimamia ustawi wa wananchi, kutenda haki na kuwa mstahamilivu.

 

Aidha, Rais Samia amesema kwa ustahamilivu wake wakati wa uongozi, hayati Mwinyi aliheshimu haki za binadamu na utawala bora na kuruhusu maoni tofauti yenye kuikosoa serikali.

 

Vile vile, Rais Samia amesema licha ya Hayati Mwinyi kuwa kiongozi katika vipindi vigumu kisiasa na kiuchumi aliweza kuhakikisha utulivu na kufanya mageuzi makubwa katika nyanja za kisiasa na kiuchumi.

No comments:

Post a Comment

Pages