March 21, 2024

Idadi ya Watalii, Mapato TANAPA vyapaa Miaka Mitatu ya Rais Samia

Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA, Mussa Nassoro Kuji Juma, akizungumza katika mkutano baina ya Wahariri na Waandishi wa Habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) ikiwa ni mfululizo wa program ya kuelezea mafanikio ya taasisi na mashirika ya umma katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Herman Batiho.

Afisa Uhifadhi Mkuu - TANAPA ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Mawasiliano,
Catherine Mbena, akizungumza katika mkutano huo.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Jully Lyimo.


 Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Mhandisi Mshauri, Dkt. Richard John Matolo, akizungumza katika mkutano huo.

Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri, akizungumza katika mkutano huo.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile, katika kikao kazi baina ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Wahariri wa vyombo vya Habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR).
 


Na Mwandishi Wetu


SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), limetangaza mafanikio iliyoyapata katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambako mapato yake yamepanda kutoka Sh. Bilioni 174.1 hadi Bilioni 337.4, ambayo ni ongezeko la Sh. Bilioni 162.7, sawa na asilimia 94.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA, Mussa Nassoro Kuji Juma, wakati akizungumza katika mkutano baina ya Wahariri na Waandishi wa Habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ikiwa ni mfululizo wa program ya kuelezea mafanikio ya taasisi na mashirika ya umma katika kipindi cha miaka mitatu, inayoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina
(OTR).

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Kamishna Kuji Juma alibainisha kuwa, mafanikio ya shirika lake hilo lililoanzishwa mwaka 1959 kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa - Sura ya 412, msingi wake mkuu ni jitihada kubwa zilizofanywa na Rais Samia, pamoja na ushiriki wake wa moja kwa moja wa Filamu ya Tanzania The Royal Tour.

“The Royal Tour ni filamu ambayo imechangia mafanikio makubwa na ongezeko la watalii wanaotembelea Hifadhi za Taifa, kwani kutokana na juhudi hizo za Rais, idadi ya watalii ilianza kupanda mwaka 2021/22 kutoka 997,873 hadi kufikia watalii milioni 1.6 mwaka 2022/23.

“Kufikia nusu ya mwaka wa fedha wa 2023/24 yaa Julai 2023 hadi Machi 19, mwaka huu 2024, idadi ya watalii wa ndani na nje imefikia watalii milioni 1.5, sawa na ongezeko la asilimia 5, ambayo ni juu ya lengo la kupokea watalii milioni 1.3. matarajio kwa mwaka mzima wa 2023/2024 ni watalii milioni 1.8.

“Kuongezeka kwa watalii hao, kumefanya mapato ya jumla ya TANAPA kupanda kutoka Sh. Bilioni 174.7 (2021/2022) hadi kufikia Sh. Bilioni 337.4 sawa na ongezeko la Sh. Bilioni 162.7 ambayo ni saw ana asilimia 94,” alifafanua Kamishna Kuji Juma mbele ya wahariri hao kutoka vyombo mbalimbali vya Habari.

Aidha, Kamishna huyo alibainisha kuwa, kwa Mwaka wa Fedha wa 2023/2024 (Julai 2023 hadi Machi 19, 2024) TANAPA limekusanya Sh. Bil. 340.1 ukilinganisha na matarajio ya kukusanya Sh. Bil. 295.4 mpaka Machi 2024, kiasi ambacho ni ongezeko la Sh. Bil. 44.6 ambayo ni sawa na asilimia 15.

Kamishna huyo akafichua kuwa, shirika lake lina matarajio ya kukusanya kiasi cha Sh. Bil. 382.3 hadi itakapofika Juni 2024, na kwamba mapato hayo ya sasa yanazidi mapato ya Sh. Bil. 282.4 yaliyokusanywa mwaka 2018/2019 kabla ya Janga la UVIKO–19, ambayo
yalikuwa ndio kiwango cha juu cha mapato katika Shirika.

Akizungumza baada ya wasilisho la Kamishna TANAPA, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, alilipongeza shirika hilo kwa ongezeko kubwa la mapato ya jumla, ikiwemo kuvunja rekodi za makusanyo miezi mitatu kabla ya kukamilika kwa mwaka wa fedha, na kulitaka kutobweteka na kulewa sifa, badala yake liongeze ufanisi.

“Shirika likaze msuli licha ya mafanikio hayo, kwani safari bado inahitaji nguvu za ziada kufikia rekodi za wenzetu. Takwimu zinaonesha kuwa wakati sisi tukihangaika na watalii milioni 1.8, wenzetu Misri mwaka jana walipokea watalii milioni 14.9 na wanapata fedha nzuri sana,” alisema Balile.

Bosi huyo wa TEF akaishauri TANAPA kuweka utaratibu wa kuyatambua makaburi ya viongozi wakubwa wa kitaifa yaliyoko Butihama (alikozikwa Rais Julius Nyerere), Chato (John Magufuli), Lupaso (Benjamini Mkapa) na Manga Pwani, Zanzibar (Ali Hassan Mwinyi) kuyafanya sehemu ya Hifadhi za Taifa, ili sio tu kuyalinda, bali kuiingizia serikali pesa.

Balile alienda mbali zaidi kwa kuishauri TANAPA kuiga mfano wa Maktaba za Mifupa ya Mauaji ya Kimbari iliyopo Kigali, Rwanda, ili Tanzania nayo iwe na Maktaba za Meno ya Tembo, ambazo anaamini zitaongeza pato la taifa, kwani watalii wa ndani na wale wa nje ya nchi hupenda kutembelea sehemu hizo na kujifunza masuala mbalimbali.

Balile akalitaka TANAPA kujipanga kusafrisha wahariri kutembelea hifadhi mbalimbali ili kujionea miundombinu ya Hifadhi za Taifa, kuwawezesha kuzungumzia jambo wanalolijua vizuri ili kuongeza ushiriki wao katika Vita ya Kiuchumi ambayo inavihitaji sana vyombo vya habari kuiwezesha dunia kuvutiwa na hifadhi hizo.

No comments:

Post a Comment

Pages