HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 10, 2024

MAENDELEO YA UTALII NA MIUNDOMBINU BAADA YA MVUA KUBWA ZA EL NINO KATIKA HIFADHI YA TAIFA YA SERENGETI

Mobhare Matinyi Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali
Dodoma, Jumapili, Machi 10, 2024: Saa 7:35 mchana.MUHIMU: Taarifa ya mafanikio ya ongezeko la watalii nchini ni kwamba, licha ya makadirio ya idadi ya watalii kwa hifadhi zote za TANAPA kwa
mwaka 2023/24 kuwa 1,387,987 lakini mpaka kufikia Februari 2024 (miezi
nane tu kuanzia Julai 2023), jumla ya watalii 1,451,176 wameshaingia huku
Serengeti ikiwa na wengi zaidi.


 


UTANGULIZI
Itakumbukwa kwamba tangu mwezi Oktoba 2023 nchi yetu ilianza kupata mvua
kubwa za El Nino ambazo hadi sasa bado zinaendelea katika baadhi ya maeneo
nchini. Moja ya athari za mvua hizo ni uharibifu wa miundombinu, ikiwemo
barabara za kwenye hifadhi za taifa zilizo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa
(TANAPA) ikiwemo Serengeti.


Kwa eneo la kaskazini mwa nchi ambako ndiko Serengeti ilipo, El Nino ilikuja
wakati wa majira ya mvua za vuli za Oktoba hadi Desemba na kisha kuendelea
kunyesha na kuunganisha na majira ya mvua za masika ya Machi hadi Mei.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ingawa
chanzo cha El Nino, ambacho ni ongezeko la joto katika bahari ya Pasifiki bado
kipo lakini sasa kinaendelea kupungua. Hata hivyo, kwa kuzingatia kuwa kuna
visababishi na viashiria vingine vya mvua kubwa, bado mvua hizi zitakuwa ni za
wastani au zaidi, ikimaanisha mvua zitakuwa kubwa kuliko ilivyozoeleka.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambayo pia imeathirika na El Nino, ni hifadhi ya
tatu kwa ukubwa nchini yenye kilomita za mraba 14,763. Hifadhi kubwa zaidi
nchini ni Nyerere ikiwa na kilomita za mraba 30,893 ikifuatiwa na Ruaha yenye


2
kilomita za mraba 19,822 lakini Serengeti ndiyo hifadhi ya kwanza nchini kwa
kuingiza watalii wengi zaidi.


Hadi sasa, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeshinda Tuzo ya Hifadhi Bora Afrika
kwa miaka mitano mfululizo. Serengeti ni maarufu zaidi kwa tukio la uhamaji wa
wanyama aina ya nyumbu ambapo kila mwaka nyumbu wapatao milioni 1.5
hutumia miezi kumi wakizunguka ndani ya hifadhi ya Serengeti na kisha kwenda
nchi jirani na kurejea. Katika uhamaji huo tukio la kusisimua zaidi ambalo ndilo
huvuta watalii wengi ni lile la kuvuka mto Mara pamoja na matawi yake.


Serengeti ambayo ilianzishwa mwaka 1959, ni kati ya hifadhi chache Afrika na
duniani ambapo mtalii anaweza kuona wanyama wote watano maarufu, yaani
simba, chui, tembo, nyati na kifaru. Wanyama wengine wengi hifadhini Serengeti
ni pamoja na pundamilia, twiga, jamii ya swala, duma, viboko na mamba.
TANAPA inasimamia na kuendeleza jumla ya hifadhi 21 zenye ukubwa wa
kilomita za mraba 98,908.88 - sawa na asilimia 10.2 ya eneo zima ya Tanzania.
Hifadhi hizo ni:


Arusha (Arusha), Burigi-Chato (Geita na Kagera), Gombe (Kigoma), Ibanda-
Kyerwa (Kagera), Katavi (Katavi), Kilimanjaro (Kilimanjaro), Kitulo (Njombe
na Mbeya), Mahale (Katavi na Kigoma), Manyara (Arusha na Manyara), Mikumi
(Morogoro), Mkomazi (Kilimanjaro na Tanga), Ruaha (Iringa, Dodoma na
Mbeya), Kisiwa cha Rubondo (Geita na Kagera), Rumanyika-Karagwe (Kagera),
Saadani (Pwani na Tanga), Kisiwa cha Saanane (Mwanza), Serengeti (Mara,
Arusha na Simiyu), Tarangire (Dodoma na Manyara), Milima ya Udzungwa
(Morogoro na Iringa), Mto Ugalla (Tabora na Katavi) na Nyerere (Pwani,
Morogoro na Mtwara).


TANAPA ina jukumu la kuendelea kuhifadhi wanyamapori, bioanuai na makazi
ya wanyama katika hifadhi za taifa kwa ajili ya vizazi vijavyo; na pia kuongeza
idadi ya watalii na mapato yatokanayo na utalii katika hifadhi zote za taifa.
Katika kutekeleza majukumu haya kwa ufanisi, TANAPA imefanikiwa kutoa
mchango mkubwa katika idadi ya watalii ambapo kwa mwaka 2022 ilichangia
watalii 697,264 kati ya 1,454,920 walioingia nchini.


Kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Utalii la Dunia (World Travel and Tourism
Council – WTTC) kwenye ripoti ya Tanzania ya mwezi Februari 2023, asilimia
90.7 ya wageni wanaoingia nchini hutembelea vivutio vya hifadhi za taifa, hifadhi
ya Ngorongoro na fukwe za Zanzibar.


ONGEZEKO LA WATALII KATIKA HIFADHI YA SERENGETI


3
Kufuatia mafanikio makubwa ya filamu ya Royal Tour – ambayo Mhe. Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye mwenyewe
alikuwa mshiriki mkuu, idadi ya watalii wanaokuja Serengeti sasa imekwenda
juu kupita malengo makubwa yaliyowekwa kwa mwaka huu wa fedha.
Taarifa ya mafanikio hayo ni kwamba, ingawa makadirio ya idadi ya watalii
kwa hifadhi zote za TANAPA kwa mwaka 2023/24 yalikuwa 1,387,987 lakini
mpaka kufikia Februari 2024 (miezi nane tu kuanzia Julai 2023), jumla ya
watalii 1,451,176 wameshaingia huku Serengeti ikiwa na wengi zaidi.


MIUNDOMBINU YA SERENGETI
Hifadhi za taifa 21 zilizo chini ya TANAPA zina barabara zenye urefu wa jumla
ya kilomita 16,470.6 ambapo Serengeti peke yake ina jumla ya kilomita 3,176.
Kimsingi ndiyo hifadhi yenye mtandao mrefu zaidi wa barabara ambazo ni za
udongo ama changarawe. Barabara hizi zimegawanyika katika barabara kuu
zilizo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa
Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) na kundi la pili la barabara
ndogondogo zilizo chini ya TANAPA yenyewe.


Serengeti pia ina viwanja vidogo vya ndege (airstrips) vipatavyo saba ambavyo
ni Serengeti, Kogatende, Lobo, Lamai, Grumeti, Kusini na Fort Ikoma.
Hivyo basi, watalii wanaokuja Serengeti huja ama kwa njia ya barabara au ndege
ndogo kutoka maeneo mbalimbali nchini yanayopokea wageni kutoka nje au
kutoka kwenye vivutio vingine kama fukwe.


TANAPA yenyewe ndiyo huzitunza barabara hizi na viwanja vya ndege ili
kuhakikisha kwamba watalii wanaendelea kuingia hifadhini. TANAPA hutumia
wataalam wake pamoja na vifaa vyake. Na kwa mujibu wa sera yake ya uhifadhi,
TANAPA hutumia changarawe kutoka ndani ya hifadhi kwa ajili ya matumizi
endelevu, kupunguza gharama na kuepuka kuingiza mimea-vamizi ambayo
huharibu malisho ya wanyama na pia kuleta magonjwa ya mimea.


Katika mtandao wa kilomita 3,176 za barabara za Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,
kilomita 2,407 ni za udongo na kilomita 769 ni za changarawe. Kutokana na hoja
kadha wa kadha za kiuhifadhi hakuna barabara za lami wala zege.
Maji yanayotumika katika matengenezo ya barabara hizi hutoka kwenye visima
badala ya mabwawa na mito iliyopo hifadhini ili kuwaachia wanyama maji hayo
ambayo ni muhimu kwa uhai.


4
Pale ilipotokea changamoto ya mvua za El Nino kulitokea mafuriko makubwa
hifadhini kiasi cha kufunika barabara kuu zinazoleta watalii. Uharibu ulikuwa
mkubwa. Hivyo basi, TANAPA ilichukua hatua za haraka za awali za kuzifanyia
matengenezo barabara hizo ili kuhakikisha kwamba wageni wanaendelea kutalii
na usafirishaji haukwami.


MATOKEO YA JUHUDI ZA TANAPA
Napenda kuchukua nafasi hii kuufahamisha umma na wadau wa sekta ya utalii
kwamba TANAPA katika hatua za awali imekamilisha matengenezo na sasa
barabara hizo zinapitika na watalii wanaendelea kupata huduma zinazostahili.
Hakuna changamoto kubwa iliyotokea kwenye upande wa viwanja vidogo vya
ndege saba vilivyopo zaidi ya maji kujaa kwenye baadhi ya maeneo ya kuegeshea
ndege. Hivyo baada ya maji hayo kukauka, huduma ziliendelea kwa usalama.


Aidha, kwa hatua za kati TANAPA inataka kunyanyua barabara nzima ya Golini
– Naabi – Seronera (km 68) kwa wastani wa sentimita 50 (nusu mita) kufuatana
na ukaguzi uliyofanyika ili kuifanya iwe juu kidogo ya usawa wa ardhi, hivyo
kuruhusu maji kutoka barabarani yapite kwenye mifumo ya mifereji na mitaro
maji iliyopo pembezoni mwa barabara. Kazi hii inaendelea.


NJIA MBADALA ZA UTATUZI WA MUDA MREFU
Lakini baada ya matumizi ya miaka takriban 65 malighafi hizi za changarawe na
maji, sasa zimepungua na kusababisha matengenezo kugharimu fedha nyingi na
kuhatarisha uhifadhi. Hivyo basi, kwa kuangalia hatua za muda mrefu, TANAPA
inatafuta njia mbadala za kuzitunza barabara hizi. Njia hizi mbadala ni zile za
kuweka tabaka gumu kama la zege au lami.


Kwa kuzingatia kanuni za uhifadhi, TANAPA na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania zinaandaa andiko la kitaalam la kuwasilisha kwenye
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)
kuhusiana na suala la kuweka tabaka gumu kwani Serengeti imo katika Orodha
ya Urithi wa Dunia inayosimamiwa na Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO.
Njia ya kutumia andiko la kitaalam ndiyo iliyotumiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya
Eneo la Ngorongoro (NCAA) ambapo sasa imepata kibali cha kujenga barabara
yenye tabaka gumu. Barabara hiyo ndiyo pia inayoingia hifadhini Serengeti kwa
kuzingatia kuwa vivutio hivi viwili maarufu duniani vinapakana.


Kuna barabara kuu nne zenye changamoto zaidi kutokana na upitaji wa magari
makubwa ya abiria na mizigo yanayokwenda mikoa ya jirani ya Mara, Arusha,
Manyara, Mwanza, Shinyanga na Simiyu ambazo TANAPA ndizo inazozilenga
katika mkakati wake wa mbinu mbadala ya tabaka gumu iwapo itakubalika.


5
Barabara hizo pia hupitisha magari ya watalii kati ya 600 hadi 800 kwa siku;
hivyo kuharibika mara kwa mara hata kama hakuna mvua kubwa. Barabara hizo
zenye jumla ya kilomita 291 tu (asilimia 9) kati ya kilomita 3,176 za mtandao wa
barabara katika hifadhi nzima ni kama ifuatavyo:
Ø Golini – Naabi - Seronera (km 68)
Ø Seronera – Lango la Ndabaka (km 121)
Ø Seronera – Lango la Ikoma (km 30)
Ø Banagi (Seronera) – Lobo – Lango la Kleins (km 72).
TANAPA inatarajia kwamba utatuzi wa kudumu utapatikana katika barabara kuu
zinazoihudumia Serengeti na hivyo kuongeza idadi ya watalii nchini kwa kiasi
kikubwa kufuatia matunda ya filamu ya Royal Tour.


TAARIFA ZA ZIADA
Takwimu za watalii 1,451,383 walioingia nchini kati ya Julai 2023 na Februari
2024 kwa mgawanyo wa wanakotoka ni kama ifuatavyo:
o Watalii kutoka nje ya nchi za Afrika Mashariki = 749,365
o Watalii wageni lakini wakaazi wa nchini Tanzania = 10,531
o Watalii wa Afrika Mashariki wakiwemo Watanzania = 230,785.
(Idadi hii ya watalii 230,785 ina watalii Watanzania = 127,650)
o Wafanyakazi wa hoteli, kambi na madereva = 460,702.

No comments:

Post a Comment

Pages