Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amekutana na Kikosi Kazi cha Miji Salama ambacho kinaratibu na kusimamia utekelezaji wa Mradi wa Ufungaji wa kamera(CCTV Camera) maalumu za kuzuia uhalifu ambapo awali zitafungwa katika majiji Matano nchini ambapo lengo ni kudhibiti matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwemo ujambazi, ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani,wizi na matukio mengine ya kiuhalifu.Majiji yatakayofungwa kamera hizo ni Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na Arusha huku lengo likiwa kufunga kamera hizo katika mikoa yote nchini kwa siku zijazo.
Akizungumza na wajumbe wa kikosi hicho Waziri Masauni amesema katika kuimarisha utendaji kazi wa Jeshi letu la Polisi na IGP Wambura yupo hapa kuna maeneo muhimu ambayo yanatakiwa yawe na udhibiti maalumu wa uhalifu hasa kwa kutumia teknolojia ambapo baadhi ya nchi tayari wana mfumo huo na wameanza kufanikiwa kudhibiti uhalifu na makosa ya ukiukwaji wa sheria za usalama.
‘Wananchi wamekua wakikutana na kadhia hii ya uhalifu na unapotaka kudhibiti matukio ya uhalifu kwa dunia ya kisasa ni muhimu kuhudhurisha matumizi ya teknolojia ndio maana serikali tumeanza jitihada za kufunga kamera,sasa mkiwa wajumbe wa kikosi kazi mfahamu mna jukumu kubwa kwa nchi kuhakikisha mradi huu unatekelezeka ili uwe na manufaa kwa nchi yetu.’alisema Waziri Masauni.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camilius Wambura amewataka wajumbe wa kikosi kazi hicho ambacho kinajumuisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za serikali kuhakikisha wanaupitia mkataba huo wa ufungaji wa kamera hizo maalumu ili lengo la mradi huo wa udhibiti wa uhalifu liweze kuleta manufaa kwa nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na Wajumbe wa Kikosi Kazi cha Miji Salama(hawapo pichani), ambacho kinaratibu na kusimamia utekelezaji wa Mradi wa Ufungaji wa kamera(CCTV Camera) maalumu za kuzuia uhalifu ambapo awali zitafungwa katika majiji matano nchini ambapo lengo ni kudhibiti matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwemo ujambazi, ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani, wizi na matukio mengine ya kiuhalifu.Kulia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,IGP Camilius Wambura.Kikao hicho kimefanyika Ofisi ndogo ya wizara,jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
No comments:
Post a Comment