Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Natu El Maamry, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Kibaha Mkoa wa Pwani.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Natu El Maamry, (kulia) akipeana mkono na Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Natu El Maamry (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa benki ya NMB, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Edwin Mhede (wa pili kulia). Wa tatu kulia ni Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu.
NA MWANDISHI WETU
SERIKALI kupitia Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, imesema inatambua na kuthamini mchango wa Taasisi na Mashirika ambayo Serikali ina hisa chache, huku akisema Ofisi yake imejipanga kufanikisha agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, la kukuza mapato yasiyo ya kikodi kutoka katika ngazi zote za Uwekezaji wa Serikali.
Mchechu ameyasema hayo leo Jumanne Machi 12, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa siku tatu baina ya Ofisi ya Msajili Hazina na Wakurugenzi wa Bodi na Maofisa Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ambayo Serikali ina hisa chini ya asilimia 50, uliolenga pamoja na mambo mengine, kutambulisha vipaumbele vya Serikali katika kujenga Uchumi imara.
Kupitia mkutano huo unaofanyika katika Ukumbi wa Shule Kuu ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani, Msajili alibainisha malengo mengine kuwa ni pamoja na kuwapa nafasi washiriki ya kuchangia Mawazo katika kuendesha Uchumi wa nchi, ili kukuza pato la taasisi hizo kutoka asilimia 3 ya sasa hadi asilimia 10.
“Unapozungumzia Mapato ya Nchi yamegawanyika katika sehemu kuu mbili, yaani Mapato ya Kodi na Mapato Yasiyo ya Kikodi. Sisi kama Ofisi ya Msajili tuna nafasi kubwa ya kusimamia Mapato Yasiyo ya Kikodi, kwa sababu yale ni magawio na faida zinazotoka kwenye Mashirika ya Umma na Uwekezaji wa Serikali.
“Ndio maana kabla yah apo hatukuwahi kuwa na mkutano wa pamoja na taasisi na mashirika haya yote ambayo Serikali ina hisa chache chini ya asilimia 50, kwa kawaida huwa tunakutana na zile taasisi na mashirika ambayo Serikali tuna umiliki mkubwa wa hisa zaidi ya asilimia 50.
“Kwa hiyo tunategenea kwamba mkutanio huu utatusaidia sana kukutana pamoja, kutambua wajibu wetu, lakini pia wawe sehemu ya wajenzi wa Uchumi wa Taifa, lakini pia wawe wachangiaji wakubwa katika Mfuko wa Serikali. Tunashukuru mpaka sasa hivi uchangiaji wao ni mzuri wastani wa wanaochangia ni asilimia 50 ya Taasisi zote na wanachokichangia ni kikubwa.
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametaka kuwe na ongezeko kubwa la Mapato Yasiyo ya Kikodi kutoka katika ngazi zote za Uwekezaji wa Serikali, kwa sasa mapato hayo (non-tax revenue) ni asilimia 3, ambapo Rais anataka kuona asilimia hizi zinapanda hadi kufikia 10, ndani ya miaka mitano.
“Na In Shaa Allah tutafikisha asilimia hizo ndani ya muda, kwa sababu tumejipanga, tunaenda vizuri chini ya wizara zetu mbili zinazosimamia kwa kina, ambazo ni Wizara ya Mipango na Uwekezaji na Wizara ya Fedha, lakini pia kwa kushirikiana na wizara zote ambazo taasisi hizi zimewekezwa ili ziweze kusimamiwa kisera ili kuboresha shughuli za kila siku,” alibainisha Mchechu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka, aliipongeza Ofisi ya Msajili kwa kukutana na Taasisi na Mashirika ambayo Serikali ina hisa chache, kutano la kwanza kufanyika tangu kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964 na kwamba huo ni muendelezo wa kudumisha ushirikiano baina ya Serikali na Wawekezaji.
“Namshukuru Msajili wa Hazina kunialika kuja kuhudhuria ufunguzi wa mkutano huu na kunipa fursa ya kujifunza kutoka kwa kila mmoja miongoni mwa Wajumbe wa Bodi na Maofisa Watendaji Wakuu wa taasisi na mashirika shiriki, katika kujadili pamoja njia za kufuata katika kukuza Uchumi wa Taifa.
“Nitumie nafasi hii kufikisha kwenu salamu za Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, anasubiri kwa hamu kusikia majadiliano baina yenu, hasa ukizingatia kuwa umakini wa Rais na Serikali yake uko kwa asilimia kubwa katika kukuza Uchumi na kustawisha taifa na watu,” alisisitiza Balosi Kusiluka.
Akaongeza ya kwamba, mkutano huo una maana kubwa kwa Rais Samia, ambapo unafanyika katika kipindi ambacho anatimiza miaka mitatu tangu alipoapishwa kuchukua nafasi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli na kusimika falsafa ya R4 (4R - Reconciliation, Resilience, Reforms and Rebulding) Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi wa Taifa.
Awali akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Natu El Maamry, alisema kwamba nia na madhumuni ya kukutana na Wajumbe wa Bodi na Maofisa Watendaji Wakuu hao ni kujaribu kuona picha moja wote, hasa ikizingatiwa kuwa taasisi na mashirika ambayo Serikali ina hisa chache, yana umuhimu sana kwa maslahi ya Taifa.
“Kwa hiyo ni muhimu kuwaweka Wajumbe wa Bodi ambao wameteuliwa kuiwakilisha Seriali katika Bodi za Wakurugenzi za taasisi hizi, waweze kuelewa picha kubwa ya namna Mashirika ya Umma yanavyopaswa kuendeshwa chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na majukumu wanayopaswa kuyatanguliza.
“Matumaini yetu kuwa mkutano huu wa siku tatu utakapoisha, basi tutakuwa na Wajumbe, Wakurugenzi wa Bodi na Maofisa Watendaji wenye uelewa mpana wa picha iliyo kwenye mageuzi ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo ndiko tunakotaka mageuzi yaelekee na kwamba Mashirika na na Taasisi za Umma ziweze kuchangia na kuwa gurudumu la maendeleo ya nchi yetu.
“Aidha, Mashirika na Taasisi watambue na kuelewa kuwa, majukumu yao ni kwenda kuangalia na kulinda maslahi ya nchi yetu, ili Serikali iweze kupata gawi la kutosha na kutunisha Mfuko wa Serikali kuiwezesha kutekeleza Maendeleo na Ustawi wa Jamii,” alisisitiza Dk. Natu wakati wa ufunguzi huo.
No comments:
Post a Comment