Na Selemani Msuya
WAANDISHI
wa habari na askari Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wameshauriwa
kutenda kazi kwa kuheshimu misingi ya kisheria, haki za binadamu, utu
wa mtu, haki za watu na haki za msingi za kulinda wananchi.
Ushauri huo umetolewa na Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne wakati
akizungumza na waandishi wa habari kwenye kikao maalum kati ya jeshi la
polisi na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC).
Amesema
jeshi la polisi kanda maalumu kupitia mikoa yake ya kipolisi Temeke,
Ilala na Kinondoni wamekuwa na mijadala na DCPC kwa muda sasa na
wamefikia hatua ya kuunda kamati shirikishi ambayo itasimamia ya hati ya
makubaliano ambayo itawaongoza kwenye utekelezaji wa maazimio yao kwa
mujibu wa sheria.
Kamanda
Muliro amesema ofisi yake itafikisha makubalino hayo kwa Mkuu wa Jeshi
la Polisi (IGP), Cammilius Wambura ili aweze kupitisha na utekelezaji
uweze kuanza.
Amesema
majadiliano hayo yamekuwa na tija kwa pande zote, hivyo ni wazi kuwa
ufanisi utakuwepo kupitia ushirikiano huo ambao wameweza kuanzisha,
kupitia kamati hiyo.
Muliro
amesema ili ushirikiano huo uweze kufanya vizuri ni vema kuweka mkazo
kwenye maarifa ya sheria na kanuni ambapo kila mtu afanye kazi kwa
kuzingatia mipaka yake.
"Kamati
hii inapaswa kusisitiza maarifa ya kisheria na kikanuni kwa waandishi
na jeshi la polisi hali ambayo italeta faraja kwa kila upande," amesema.
Kwa
upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kiposili Temeke, John Malulu
amesema uundwaji wa kamati hiyo unaenda kufungua ukurasa mpya wa sekta
hizo ambazo zina mchango mkubwa kwenye usalama na ulinzi wa nchi.
"Hii
kamati inaenda kukuza na kuendeleza ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi
na vyombo vya habari, naamini tunaenda kuleta mabadiliko chanya,"
amesema.
Mjumbe
wa Kamati hiyo Ndogo, Askofu Emaus Mwamakula amesema ushirikiano huo
unapaswa kuendelezwa kila mahali na kwamba yeye atashiriki kikamilifu
kufanikisha.
"Jeshi la
Polisi na waandishi wa habari kwa muda mrefu wamekuwa wakivutana sana,
ila kwa hatua hii tunaona mambo mazuri siku chache zijazo," amesema.
Naye Sheikh wa Wilaya ya
Ilala, Adam Mwinyipingo amesema yupo tayari kufanya kazi na kamati hiyo
ambayo imelenga kuboresha umoja, amani na usalama kwa mkoa na taifa.
"Makundi mawili
haya yana faida katika jamii, hivyo imani yangu ni kuona matokeo chanya
kwenye eneo la amani na utulivu katika nchi," amesema.
Amesema viongozi wa dini ni watu muhimu
katika kulinda amani, usalama na ahaki hivyo kitendo cha wao kuwepo
kwenye kamati wanaenda kutoa mchango mzuri kwa makundi hayo.
Akitangaza
majina ya wajumbe wa kamati hiyo ndogo, Katibu wa DCPC, Fatma Jalala
amesema hatua hiyo imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kimkakati kati
klabu hiyo na jeshi la polisi hasa kwenye kufuatilia ulinzi na usalama
wa waandishi wa habari wanapokuwa kazini.
Amesema
kamati hiyo ina wajumbe sita ambao ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa
Polisi (SACP), John Malulu, ambaye pia ni RPC wa Mkoa wa Kipolisi
Temeke, Askofu Emaus Mwamakula na Sheikh wa Wilaya ya Ilala, Adam
Mwinyipingu.
Wengine ni Wakili Mkumbo Emmanuel, Katibu Mkuu wa DCPC, Fatma Jalala na Bakari Kimwanga (mwanachama wa DCPC).
"Kuundwa
kwa kamati hiyo ni matokeo ya midahalo mitatu kati ya DCPC na Polisi
kuhusu ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari, lakini pia pamoja na
suala zima la kusimamia haki na sheria.
Midahalo
hiyo iliyoanza Novemba 2023 na kumalizika Februari 2024, iliratibiwa
na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) chini ya
udhaminiwa na shirika la IMS, ilihusisha Kanda Maalum (Ilala ikiwemo),
Temeke na Kinondoni, ambapo maazimio kadhaa ya kiutendaji yalifikiwa.
Miongoni
kwa maazimio hayo ni kuwepo kwa mabonanza ya kimichezo kwa lengo la
kujenga ukaribu, kuhakikisha usalama wa waandishi wanapokuwa kazi na
hata katika operesheni za polisi, kuwepo kwa kanzidata ya waandishi wa
habari ambayo itatambuliwa na polisi, lakini pia Polisi kufanya kazi kwa
karibu zaidi na uongozi wa DCPC.
No comments:
Post a Comment