HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 23, 2024

Muliro:Waandishi, Polisi zingatieni sheria

Na Selemani Msuya          


WAANDISHI wa habari  na askari Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wameshauriwa kutenda kazi kwa kuheshimu misingi ya kisheria, haki za binadamu, utu wa mtu, haki za watu na haki za msingi za kulinda wananchi.                             
Ushauri huo umetolewa  na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kikao maalum kati ya jeshi la polisi na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC).    

                  

Amesema jeshi la polisi kanda maalumu kupitia mikoa yake ya kipolisi Temeke, Ilala na Kinondoni wamekuwa na  mijadala na DCPC kwa muda sasa na wamefikia hatua ya kuunda kamati shirikishi ambayo itasimamia ya hati ya makubaliano ambayo itawaongoza kwenye utekelezaji wa maazimio yao kwa mujibu wa sheria.
                                 
Kamanda Muliro amesema ofisi yake itafikisha makubalino hayo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Cammilius Wambura ili aweze kupitisha na utekelezaji uweze kuanza.
                     
Amesema majadiliano hayo yamekuwa na tija kwa pande zote, hivyo ni wazi kuwa ufanisi utakuwepo kupitia ushirikiano huo ambao wameweza kuanzisha, kupitia kamati hiyo.        

Muliro amesema ili ushirikiano huo uweze kufanya vizuri ni vema kuweka mkazo kwenye maarifa ya sheria na kanuni ambapo kila mtu afanye kazi kwa kuzingatia mipaka yake.

"Kamati hii inapaswa kusisitiza maarifa ya kisheria na kikanuni kwa waandishi na jeshi la polisi hali ambayo italeta faraja kwa kila upande," amesema.
                           
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kiposili Temeke, John Malulu amesema uundwaji wa kamati hiyo unaenda kufungua ukurasa mpya wa sekta hizo ambazo zina mchango mkubwa kwenye usalama na ulinzi wa nchi.                       

"Hii kamati inaenda kukuza na kuendeleza ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na vyombo vya habari, naamini tunaenda kuleta mabadiliko chanya," amesema.             

Mjumbe wa Kamati hiyo Ndogo, Askofu Emaus Mwamakula amesema ushirikiano huo unapaswa kuendelezwa kila mahali na kwamba yeye atashiriki kikamilifu kufanikisha.                          
"Jeshi la Polisi na waandishi wa habari kwa muda mrefu wamekuwa wakivutana sana, ila kwa hatua hii tunaona mambo mazuri siku chache zijazo," amesema.                             
Naye Sheikh wa Wilaya ya Ilala, Adam Mwinyipingo amesema yupo tayari kufanya kazi na kamati hiyo ambayo imelenga kuboresha umoja, amani na usalama kwa mkoa na taifa.                                     
"Makundi mawili haya yana faida katika jamii, hivyo imani yangu ni kuona matokeo chanya kwenye eneo la amani na utulivu katika nchi," amesema.                            
Amesema viongozi wa dini ni watu muhimu katika kulinda amani, usalama na ahaki hivyo kitendo cha wao kuwepo kwenye kamati wanaenda kutoa mchango mzuri kwa makundi hayo.

Akitangaza majina ya wajumbe wa kamati hiyo ndogo, Katibu wa DCPC, Fatma Jalala amesema hatua hiyo imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kimkakati kati klabu hiyo na jeshi la polisi hasa kwenye kufuatilia ulinzi na usalama wa waandishi wa habari wanapokuwa kazini.

Amesema kamati hiyo ina wajumbe sita ambao ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), John Malulu, ambaye pia ni RPC wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Askofu Emaus Mwamakula na Sheikh wa Wilaya ya Ilala, Adam Mwinyipingu.

Wengine ni Wakili Mkumbo Emmanuel, Katibu Mkuu wa DCPC, Fatma Jalala na Bakari Kimwanga (mwanachama wa DCPC).

"Kuundwa kwa kamati hiyo ni matokeo ya midahalo mitatu kati ya DCPC na Polisi kuhusu ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari, lakini pia pamoja na suala zima la kusimamia haki na sheria. 

Midahalo hiyo iliyoanza Novemba 2023 na kumalizika Februari  2024, iliratibiwa na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) chini ya udhaminiwa na shirika la IMS, ilihusisha Kanda Maalum (Ilala ikiwemo), Temeke na Kinondoni, ambapo maazimio kadhaa ya kiutendaji yalifikiwa.

Miongoni kwa maazimio hayo ni kuwepo kwa mabonanza ya kimichezo kwa lengo la kujenga ukaribu, kuhakikisha usalama wa waandishi wanapokuwa kazi na hata katika operesheni za polisi, kuwepo kwa kanzidata ya waandishi wa habari ambayo itatambuliwa na polisi, lakini pia Polisi kufanya kazi kwa karibu zaidi na uongozi wa DCPC.


No comments:

Post a Comment

Pages