March 19, 2024

Polisi Tanga wakoshwa na Amend

Na Mwandishi Wetu,Tanga

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga limesema mafunzo ya usalama barabarani yanayotolewa na Shirika la Amend kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi nchini yanasaidia kutoa elimu ya matumizi salama ya barabara kwa madereva bodaboda wa mkoa huo.



Akizungumza jijini Tanga, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, William Mwamasika amesema mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa madereva bodaboda wa mkoa huo na wanaushukuru Ubalozi wa Uswisi pamoja na Amend Tanzania kwa kuona umuhimu wa madereva bodaboda kupatiwa mafunzo hayo.

"Jeshi la Polisi Kitengo cha usalama barabarani Mkoa wa Tanga tunawashukuru Ubalozi wa Uswisi nchini kwa udhamini wa mafunzo haya na kuona kuna haja ya kuongeza nguvu kwenye utoaji elimu ya usalama barabarani hasa katika kundi hili ambalo linaonekana kuwa hatarini  zaidi."

Pamoja na shukrani hizo, mkakati uliopo kwa sasa ni kuhakikisha mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva bodaboda yanayotolewa katika wilaya zote za Mkoa wa Tanga kwani kwa sasa yanafanyika katika Jiji la Tanga na tayari madereva bodaboda zaidi ya 200 wamefikiwa na lengo ni kuwafikia madereva 500.

Hivyo katika kufanikisha kampeni hiyo Kamanda Mwamasika amesema  watakaa kikoa cha pamoja kuona ni maeneo yapi yafikiwe, ili kuhakikisha vijana hao wa kundi la bodaboda wanapata mafunzo yatakayowawezesha kujilinda wao wenyewe na kulinda abiria wao lakini waachwe kuwa visababishi vya ajali barabarani.



Kwa upande wake Ofisa Miradi wa Amend Tanzania Ramadhan Nyanza ametumia nafasi hiyo kuwaomba vijana wanaojihusisha na bodaboda kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo yanayotolewa bure kwani tayari Ubalozi wa Uswisi wameshafadhili.

"Tunatoa mafunzo haya bure kwa hiyo vijana wajitokeze kwa wingi, watumie mafunzo haya na nafasi hii kupata elimu.Tunafahamu wao ni madereva lakini kuwa dereva bila kutii sheria za usalama barabarani ina maana unakuwa mtu ambaye unaendesha chombo cha moto kwa kudhamiria kusababisha ajali," amesema Nyanza.

Aidha amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa madereva bodaboda katika wilaya za Mkoa wa Tanga na lengo ni kuifikia jamii. Hivyo wanaomba bodaboda wajitokeze kwa wingi katika mafunzo hayo.

Pia amesema katika mradi huo mbali ya kutoa mafunzo hayo, wanatarajia kufanya uboreshaji wa miundombinu salama katika Shule ya Msingi Azimio na Makorora ikiwa ni muendelezo wa miradi wanayoifanya ndani ya Jiji la Tanga ,lengo likiwa kuendelea kuwalinda wanafunzi wanapokuja na kuondoka shuleni.

Pia amesema wanaandaa kanuni za maadili ambazo wanashirikiana na Jeshi la Polisi na kwamba watayajumuisha rasmi katika elimu ya usalama barabarani na kanuni hizo zitakuwa zinalenga kusaidia kupunguza ajali lakini kuwalinda abiria.




No comments:

Post a Comment

Pages