CHAMA
cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kutekeleza ahadi yake ya kutunga
Sheria ya kuiwezesha Tume Huru ya Uchaguzi kusimamia Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa.
Kauli
hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti Bara, Isihaka Mchinjita, leo Machi
17 L, 2024 kwenye mapokezi ya kumpongeza kwa kuchaguliwa na Mkutano Mkuu
Taifa yaliyofanyika katika Ofisi ya Mkoa wa Lindi iliyopo Lindi Mjini.
"Tarehe
2 Februari 2024 kwenye mchakato wa kutunga Sheria ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi Serikali ilileta Jedwali la Maboresho ili kuipa dhamana Tume
ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa
Serikali za vijiji, mitaa na vitongoji kwa kuzingatia utaratibu
utakaoainishwa na Sheria itakayotungwa na Bunge" alisema Mchinjita na
kuongeza;
"Kwa bahati
mbaya, Miswada ya Tume ya Uchaguzi na Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani bado haijasainiwa na Rais kuwa Sheria hadi sasa. Hatujui ni
maboresho gani hasa yamepitishwa kuwa Sheria. Pili, hadi sasa, Serikali
haijaanza mchakato wa Sheria iliyoahidiwa bungeni ya kuipa madaraka Tume
ya Uchaguzi kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Tunaona dalili za
Serikali kupata kigugumizi katika kutekeleza ahadi yake"
"Ni
muhimu Bunge lisimame kidete kuhakikisha maboresho yaliyofanyika
bungeni ya kuipa dhamana Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia uchaguzi wa
serikali za mitaa yanazingatiwa. Ni muhimu mchakato wa kutunga sheria
kwa suala hilo uanze sasa," amesema.
Mchinjita
amesema ACT Wazalendo wameshaiagiza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Chama
kuainisha vipaumbele vya ACT Wazalendo wanavyotaka kuwepo kwenye Sheria
hiyo.
Katika hatua
nyingine, Mchinjita amesema kwa kushirikiana na viongozi wenzake na
Baraza Kivuli la Mawaziri la ACT Wazalendo, atahakikisha kuwa ACT
Wazalendo kinaendelea kuwa chama kinara katika kuzisemea kero za
wananchi wa Tanzania.
Amesema
kuwa Watanzania wana kero nyingi na ACT Wazalendo itazipa kipaumbele.
"Mfano hapa Lindi, Mradi wa kuchakata gesi wa LNG ulishafikia hatua ya
Serikali kusaini HGA wakati Waziri akiwa January Makamba.
"Amekuja
Waziri mpya amerudisha nyuma mjadala kana kwamba tumekuwa na wataalam
wapya wanaomshauri Waziri. Kuna habari kuwa kuna tishio la wawekezaji
kutoka Marekani kujitoa na hivyo kurudisha nyuma jitihada zilizofanyika
kwa muda mrefu," amesem.
Mchinjita
amesema ACT Wazalendo wanaitaka Serikali iharakishe mazungumzo ili
mradi uanze kwa maendeleo ya nchi yetu, Lindi na Kusini kwa ujumla.
Makamu
Mwenyekiti huyo ameweka bayana kuwa kipaumbele chake kingine kitakuwa
kushirikiana na viongozi wenzake katika ujenzi wa chama.
"Nitatumia
sehemu ya muda wangu kuzunguka nchi nzima kuhakikisha kuwa mtandao wa
matawi, kata, majimbo na mikoa ambao tumeujenga nchi nzima unaendelea
kuimarishwa.
Mchinjita
alichaguliwa na Mkutano Mkuu Taifa uliofanyika tarehe 5 na 6 Machi 2024
kuwa Makamu Mwenyekiti Bara wa Chama. Viongozi wakuu wengine
waliochaguliwa ni Dorothy Semu aliyechaguliwa kuwa Kiongozi wa Chama,
Othman Masoud Othman aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama na Ismail
Jussa aliyechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar.
No comments:
Post a Comment