HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 26, 2024

Ubalozi wa marekani waadhimisha hatua muhimu iliyofikiwa katika uhifadhi wa magofu ya kihistoria ya kiswahili ya Kua

 Dar es Salaam – Tarehe 21 Machi, Balozi wa Marekani nchini Tanzania Michael Battle, aliungana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mafia, Mhe. Olivanus Paul Thomas, kuadhimisha kukamilika kwa awamu ya tatu ya mradi wa ukarabati wa magofu ya kihistoria ya Kiswahili ya Kua katika kisiwa cha Juani visiwani Mafia uliofadhiliwa na Mfuko wa Balozi wa Uhifadhi wa Utamaduni (AFCP).


 

 

Kutoka mwaka 2017 hadi 2022, Ubalozi wa Marekani ulitoa ruzuku ya jumla ya Dola za Kimarekani 434,929 (takriban Shilingi bilioni 1.1) kwa taasisi iitwayo World Monument Fund (WMF) kupitia Mfuko wa AFCP wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani. Fedha hizi zilisaidia uhifadhi wa magofu haya ya kale kwa juhudi za pamoja na jamii ya eneo husika. Hafla ya kusherehekea kukamilika kwa ukarabati wa Magofu ya Kua ilihudhuriwa na maafisa wa serikali ya wilaya, mwakilishi kutoka Wizara ya Maliasili, wawakilishi wa WMF, na wanajamii.

 

 

Ukiwa umejengwa nje ya pwani ya Tanzania katika kisiwa cha Juani, mji wa kale wa Kiswahili wa Kua una historia inayoturudisha nyuma hadi karne ya 13, ukiwa kama mojawapo ya makazi makubwa kabisa ya kale ya Waswahili wa Afrika Mashariki. Mji huu wa kale unajumuisha idadi kubwa ya majengo ya makazi ambayo masalia yake yameendelea kubaki hata baada ya miaka mingi, ikiwa ni pamoja na kasri kubwa na misikiti mitano. 

 

 

Yakiwa yanalindwa na Sheria ya Mambo ya Kale Na. 10 ya mwaka 1964, iliyofanyiwa marekebisho na Sheria Na. 22 ya mwaka 1979, Magofu ya Kua ni ushuhuda wa uhandisi wa kipekee wa Kiswahili ulio na umuhimu wa kipekee kihistoria. Balozi Battle alisema, "Kupitia programu ya AFCP, Marekani imehifadhi siyo tu kiini cha Kua bali pia imehakikisha jamii za eneo hilo zinanufaika kutokana na juhudi hizi za uhifadhi."

 

 

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001, Mfuko wa Balozi wa Uhifadhi wa Utamaduni (AFCP) umelenga kulinda maeneo ya urithi wa kitamaduni yanayotambulika duniani kote. Toka mwaka 2002 Watu wa Marekani wamechangia zaidi ya dola za Kimarekani milioni moja kusaidia miradi mbalimbali ya uhifadhi nchini Tanzania. Miradi hii ni pamoja na ukarabati wa Msikiti wa Kizimkazi wa karne ya 18 Zanzibar, magofu ya bandari ya kihistoria ya Kilwa Kisiwani, michoro ya zamani ya miamba huko Kondoa, Nyumba ya Bwanga ya karne ya 19 Pangani, na misikiti ya kihistoria ya Shumba na Micheweni Pemba, miongoni mwa mingine.

 

 

Taasisi ya World Monument Fund (WMF) ambayo ndio mtekelezaji mkuu wa mradi huu, ni taasisi isiyozalisha faida inayoongoza duniani katika juhudi za kuhifadhi maeneo ya urithi wa kitamaduni duniani kote. Ikiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 50 katika nchi zaidi ya 90, wataalam wa WMF hutumia mbinu za kisasa za uhifadhi kulinda amali na maeneo muhimu ya kihistoria na kitamaduni duniani kote.

No comments:

Post a Comment

Pages