April 12, 2024

HATUTORUHUSU UTAPELI KATIKA ZOEZI LA KUHAMA KWA HIYARI KWA WANACHI WA NGORONGORO- DC MSANDO

Na Mwandishi Wetu, Handeni



Mkuu wa Wilaya ya Handeni mheshimiwa Wakili Albert Msando amesema serikali haitoruhusu mtu yeyote kufanya vitendo vya utapeli na udanganyifu katika mradi wa kuhamisha wananchi kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kwenda katika Kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Kijiji cha Msomera Handeni tarehe 11 Aprili, 2024  Mhe.Msando amesema amefika katika Kijiji hicho ili kukutana na mwananchi yeyote ambaye anaamini kuwa serikali haijamtendea haki wakati wa kuhama kutoka ndani ya hifadhi kwenda kijijini hapo ili aweze kusikilizwa na kutatua changamoto yoyote kuhusiana na madai hayo.


Wakili Msando amesema kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya wananchi ambao wakati wanahama kutoka Ngorongoro kwenda kijijini hapo walikuwa wategemezi katika kaya mbalimbali ambazo zililipwa stahiki  zao zote za maendelezo ya mali zao pamoja na motisha ambao wamejitokeza na kudai kuwa wametapeliwa na serikali kitu ambacho si cha kweli.

"Wananchi 132 ambao waliorodhesha majina yao na kuyaleta kwangu niliyatuma majina hayo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na serikali imegundua kuwa watu hao hawakuwa wakuu wa kaya wakati wanahama, Kuna watu wanataka kuleta utapeli katika zoezi hili na wengine wapo nchi za nje wakiamini kwamba kuna fedha za bure ili wafanye utapeli hilo halikubaliki na ndio maana leo nimekuja tena hapa niwasikilize kama wana jambo lolote la ziada”,alisema Mh.Msando.

Kuhusu wananchi watatu ambao majina yao yameongezeka katika taarifa iliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari  jana Mhe.Msando amesema vyombo husika vinafuatilia madai yao kuona kama yana ukweli na kuuhakikishia umma kwamba hakuna mwananchi yeyote ambaye atakubali kuhama kwa hiyari asipate haki zake anazostahili kwa mujibu wa sheria.

Mkuu huyo wa Wilaya mesisitiza kuwa zoezi la kuhamisha watu kutoka ndani ya hifadhi ni la hiyari na ndiyo maana wahusika wote wanahusishwa kuanzia hatua ya uelimishaji, uandikishaji, uthaminishaji na uhamishaji wa wananchi na mali zao ambapo kila mwananchi anayekubali kuhama husaini fomu mbalimbali zinazomuwezesha kupata stahiki zake kwa haraka.

Mhe. Msando ametoa wito kwa wananchi wanaokubali kuhama kwa hiyari kutumia fedha wanazozipata kufanya maendelezo katika  maeneo wanayopewa na serikali badala ya kutumia fedha hizo kwa mambo mengine na mwisho wa siku kutoa lawama kwa serikali na kuanzisha madai mengine.


Vilevile amewataka waandishi wa habari wote wanaotaka kufahamu ukweli baada ya kupata  malalamiko kutoka kwa wananchi kuwasiliana na mamlaka zinazohusika badala ya kuupotosha umma kwa taarifa zisizo na ukweli wowote kwa kuegemea upande mmoja.

Jumla ya wananchi 132 ambao ni wategemezi wa kaya zilizohama kwa hiyari  kutoka  ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kwenda  katika Kijiji cha Msomera  waliripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari wakidai kwamba serikali haijawapa stahiki zao wakati wa zoezi hilo la kuhama kitu ambacho kilikanushwa pia na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.


No comments:

Post a Comment

Pages