April 12, 2024

Wananchi walioathiriwa na wanyamapori wapata kifuta jasho cha milioni 399 Lindi

 NA MWANDISHI WETU

 

WIZARA ya Maliasili na Utalii imetoa kifuta jasho cha shilingi milioni 399 kwa wananchi 1,658 walioathiriwa na wanyamapori wilayani Nachingwea mkoani Lindi.


Mkuu wa wilaya hiyo Nachingwea Mohamed Hassan Moyo amethibisha hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari Aprili 9, 2024 katika ziara ya kuelezea jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika kukabiliana na migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori.
 

"Serikali kupitia utaratibu wake wa kifuta jasho na kifuta machozi, wananchi zaidi ya 1658 kwenye wilaya ya Nachingwea walipatikana na kugawiwa fedha hizo ambazo zilitoka mwaka jana kiasi cha  shillingi 399, 405,000,wote waliokuwa wanastahili walipatiwa," alisema Moyo


Baadhi ya Askari wa Wanyamapori
Moyo amesema wilaya yake imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya mgongano baina ya Binadamu na Wanyamapori na tembo ndio anatajwa kuhusika zaidi kwenye migongano hiyo.
 

Kwamba tembo wanaathiri mali na maisha ya wananchi, lakini pamoja na changamoto hizo kumekuwepo na jitihada nyingi zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA na TAWIRI katika kuelimisha wananchi mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori pamoja na kuwadhibiti.


"Jitihada za TAWA zimefanyika mara nyingi na mimi mwenyewe nimekuwa nikishiriki, jitihada moja ni kwa kutumia helikopta katika kuwaswaga tembo ili warudi hifadhini ," alisema Mkuu huyo wa wilaya


Akibainisha jitihada zilizofanywa na TAWA Katika kukabiliana na migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori  Kanda ya Kusini Mashariki, Mhifadhi Mkuu Kitengo cha Oparesheni, Linus Chuwa amesema TAWA imeanzisha vituo 10 vya Askari wa kukabiliana na wanyamapori hao ambapo vitano kati ya 10 ni vya kudumu  na vingine  vitano ni vya muda mfupi hasa pale matukio ya wanyamapori hao yanapojitokeza.


TAWA pia imefanikiwa kununua gari jipya katika kituo cha Malola ambalo hutumiwa na Askari wa kituo hicho, pia imenunua ndege nyuki (drones) maalumu kwa ajili ya kuswaga tembo ambazo zilitumika katika zoezi la kurudisha tembo hifadhini mwaka 2023, zoezi ambalo linatajwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.


Afisa habari wa TAWA, Beatus Maganja
Jitihada zingine zilizofanywa na TAWA kwa kushirikiana na wadau ni pamoja na kuwafunga visukuma mawimbi tembo watatu ambao ni  viongozi wa makundi  na hivyo kufuatilia mienendo yao ili kuwadhibiti kabla hawajafika katika makazi ya binadamu.

 

Mhifadhi Mkuu, Linus Chuwa ameongeza kusema  TAWA  imepeleka Askari wa wanyamapori wa vijiji 41 (VGS)  katika chuo cha Likuyu Sekamaganga kwa ajili ya kupatiwa elimu ya kudhibiti wanyamapori na amethibitisha kuwa Askari hao hutumiwa na TAWA Katika matukio mbalimbali ya kudhibiti wanyamapori hao.

Kwa upande wake, Afisa habari wa TAWA, Beatus Maganja amesema lengo kuu la ziara hiyo Mkoani humo ni kuelezea jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA katika kukabiliana na wanyamapori na kuwahakikishia wananchi kuwa TAWA iko kazini inafanya kila iwezalo kuwadhibiti wanyamapori hao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile TAWIRI, GIZ na TANAPA.



No comments:

Post a Comment

Pages