Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Mkwawa akizungumza katika Kongamano la maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano.
Na Mwandishi Wetu
HOJA ya kuchangamana kwenye kuoana hususani kwenye jamii ya kipemba inapaswa kutafutiwa ufumbuzi ili kuimarisha Muungano.
Hilo limeibuliwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mchungwani Ubungo, William Chitanda, wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano lililoandaliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam.
"Inaonyesha kuna ugumu wa kuchangamana hasa kwenye masuala ya kuoana, jamii ya kipemba wanakuwa wagumu kuchangamana na makabila mengi Bara au Visiwani.
Amesema ili kuimarisha uhusiano jambo hilo linapaswa litafutiwe ufumbuzi.
Naye Luteni Kanali mstaafu, Kingu Shamte amesema serikali iinaendelea kuzifanyia kazi changamoto za kijamii, kisiasa na kiuchumi, zinazoleta dosari katika muungano, ikiwa ni miaka 60 sasa ya muungano.
Kwa upande mwingine Shamte ameishauri serikali kuwatumia wazee waliokuwepo wakati wa uhuru, wenye uwezo wa kutoa historia ili isipotee.
"Ningeomba semina, mihadhara na makongamano yanayotolewa kuhusu muungano, wahusika wawatumie wazee waliokuwepo ili kuweka historia sahihi "amesema.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Ubungo, Hassan Mkwawa amesema serikali imetatua changamoto iliyokuwa inaonekana kila inapofikia kipindi cha uchaguzi, Visiwani Zanzibar kwa kuwa na serikali ya maridhiano.
"Zanzibar wana Makamu wa kwanza wa Rais toka vyama viwili vya siasa tofauti. Mambo mengi ya muungano yamekuwa yakifanyiwa kazi ikiwemo serikali ya maridhiano," amesema.
Amesema kuwa, masuala yote yaliyoleta 'chokochoko' kwenye muungano yamekuwa yakifanyiwa kazi.
No comments:
Post a Comment