April 05, 2024

Michezo ya kipaumbele kupewa nafasi sawa : Mwinjuma

 Na Jasmine Shamwepu, Dodoma

Naibu Waziri Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Michezo yote ya kipaumbele inapata nafasi sawa

Mwinjuma amesema hayo leo Jijini Dodoma wakati wa Uzinduzi wa Jezi ya timu ya Taifa ya Mpira wa Kikapu ya Tanzania.

"Tuna michezo takribani sita ya kipaumbele inabidi kuhakikishe inapata nafasi sawa kwa maana ya kupewa nafasi ya sehemu kama miundombinu ya michezo na kuwezeshwa kwa timu zetu"amesema

Aidha amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Kikapu ili kuhakikisha wanatengeneza mabadiliko chanya ya kuutoa mpira wa Kikapu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Kuhusu suala la Mpira wa Kikapu kuwa mchezo wa kimashindano kama ulivyo Mpira wa Miguu hapa nchini Mhe.Mwinjuma amesema kuwa ni jambo ambalo inabidi libaki kwenye akili za viongozi wote wanaohusika na jambo hili.

"Ukikaa hivi juu juu ukiwa hufatlia unaweza kufikiri mchezo wa Mpira wa Kikapu umekufa kabisa,lakini ukienda kwenye matukio ya Mpira wa Kikapu unaipata picha kwamba huu mchezo una wapenzi wengi na kuna jukumu la kuhakikisha unachezwa kwenye viwango ambavyo awali walivitarajia"amesema


Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania Michael Kadebe awali akimkaribisha mgeni rasmi ameishukuru Serikali kupitia Wizara yake ya Michezo na Baraza la Michezo Tanzania BMT kwa kuwapatia Ushirikiano wa kutosha na kuwapatia miongozo inayowawezeshakusimamia,kukuza na kuendeleza mchezo wa Mpira wa Kikapu nchini.


Aidha ametoa shukrani kwa kampuni ya Michezo ya Kajumulon ambayo imetoa ufadhili wa kutengeneza Jezi.

"Hatua hii inaashiria maono ya Watanzania mbalimbali waliopo nje wenye moyo wa Uzalendo katika kuinua viwango vya michezo ikiwemo Mpira wa Kikapu katika nchi yetu"amesema.

Kuhusu Jezi hizo Kadebe amesema kuwa ni zaidi ya kitambaa na muundu inajumuisha ndoto,matarajio,na bidii ya wachezaji wanaojitolea kwa mchezo wanaoupenda.

Katika hatua nyingine Kadebe amewaambia wachezaji wa timu ya Taifa ya Mpira wa Kikapu wavae jezi hiyo kwa kujivunia.

No comments:

Post a Comment

Pages