May 17, 2024

Dk. Mwinyi aipongeza CRDB Mafanikio ya Mkakati wa Biashara 2023-2027

 

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akitoa hotuba yake wakati akifungua Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB jijini Arusha leo Mei 17, 2024.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, mara baada ya kuwasili kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) kufungua Semina ya Wanahisa wa benki hiyo leo Mei 17, 2024. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Thomas Sabaya.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, alipowasili kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) kufungua rasmi Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB leo Mei 17, 2024.
Baadhi ya washiriki wa semina hiyo.



Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu (kulia) akijadiliana jambo na
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, wakati wa Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB jijini Arusha.


 
NA MWANDISHI WETU, ARUSHA


RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Benki ya CRDB kutokana na mafanikio iliyopata katika Mwaka wa Kwanza wa Utekelezaji wa Mkakati Mpya wa Biashara wa Muda wa Kati wa Mwaka 2023/27, ambako benki hiyo imevuna Faida Baada ya Kodi ya Sh. Bilioni 424, ambalo ni ongezeko la asilimia 21.

Dk. Mwinyi ametoa pongezi hizo kwa Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti, Wafanyakazi na Wanahisa wa CRDB, wakati wa Semina ya Wanahisa benki hiyo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), uliolenga kutoa elimu muhimu ya masuala ya fedha na uwekezaji kwa wanahisa wake.

Akizungumza na wanahisa hao, Dk. Mwinyi ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, aliishukuru CRDB kwa kuendeleza mashirikiano mema na Serikali yake na kujipambanua kama mshirika sahihi katika kukuza Uchumi wa Buluu Zanzibar, lakini akaonesha kuvutiwa na mafanikio ya taasisi hiyo mwaka jana.
 
“Nimetaarifiwa hapa kuwa mwaka jana CRDB ilianza Mkakati Mpya wa Biashara wa Muda wa Kati (2023-2027), hasa baada ya mkakati mwingine wa miaka mitano kukamilika Desemba 2022.

“Niwapongeze kwa mafanikio ambayo yamepatikana katika mwaka huo wa kwanza wa utekelezaji wa mkakati huu, ambapo tumesikia Faida Baada ya Kodi imeongezeka kwa asilimia 21 kufikia Sh. Bilioni 424, kulinganisha na Sh. Bilioni 351 iliyokuwa imepatikana mwaka 2022.

“Fedha ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya taifa letu. Hivyo basi, Sekta ya Fedha iliyo imara ni nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Ndio maana Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa katika kuhakikisha kuwa sekta hii ina mchango mkubwa katika maendeleo yetu.

“Tunajivunia kuwa na taasisi za fedha imara zikiongozwa na CRDB, benki ambayo imekuwa mshirika muhimu wa kuimarisha dhana yetu ya Uchumi wa Buluu.

“Kupitia Programu za Uwezeshaji kama vile ‘Inuka na Uchumi wa Buluu’, CRDB imechangia sana kuendeleza sekta za kimkakati kama vile utalii, kilimo, ufugaji, uvuvi, mafuta, biashara na ujasiriamali,” alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, Dk. Mwinyi alibainisha kwamba mchango na mafanikio ya CRDB yanatokana na imani thabiti ya Wanahisa kwa benki hiyo na kuwabainishia kuwa uwekezaji wao umeipa nguvu ya kufadhili miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Sekta ya Umma na Binafsi Tanzania Bara na Visiwani.

Kwa upande, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, aliishukuru Serikali, aliyoitaja kama siri ya mafanikio ya benki yake kutokana na utashi wa kisiasa, mazingira wezeshi ya kibiashara yaliyowekwa na Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar – SMZ), pamoja na ushirikiano wa kimkakati uliopo.

“Hii imepelekea benki yetu kuwa na ukuaji endelevu mwaka hadi mwaka, ambako katika Mwaka wa Fedha wa 2023, CRDB imepata Faida Baada ya Kodi ya Sh. Bilioni 423, ambayo ni ongezeko la asilimia 21, kulinganisha na mwaka 2022, huku tukishuhudia ukuaji mkubwa katika viashiria vingine vya utendaji.

“Ukuaji huu tunaendelea kuushuhudia hata mwaka huu, ambapo Matokeo ya Robo ya Kwanza ya Mwaka yanaonyesha benki imepata faida ya Sh. Bilioni 128, kulinganisha na Sh. Bilioni 90 iliyorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana 2023.

“Hivyo basi, tunaposherehekea mafanikio haya, hatuna budi kutoa shukrani zetu za dhati kwa Serikali yetu kwa ushirikiano na mazingira mazuri ambayo sio tu yanasaidia kukuza faida ya benki, bali pia uwekezaji wa wanahisa wetu kupitia gawio na thamani ya hisa,” alibainisha Nsekela.

Alimkumbusha Dk. Mwinyi ya kwamba aliposhika hatamu za uongozi mwaka 2020, walikaa na kumueleza utayari wa benki hiyo kushirikiana na Serikali yake, ambako aliifungulia milango na kutoa maelekezo kwa wasaidizi wake katika ngazi mbalimbali kushirikiana nayo katika kufikia Malengo ya Uchumi wa Buluu.

“Ni kataika dhamira na utayari ule uliouonyesha tokea mwanzo, CRDB imekuwa mdau muhimu katika maendeleo ya Zanzibar na Wazanzibari kwa kujenga ushirikiano wa kimkakati ambao umekuwa na manufaa makubwa,” alisisitiza Nsekela.

Kwa biaba ya Bodi ya Wakurugenzi ya CRDB, Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Ali Hussein Laay, aliahidi kudumisha ushirikiano na Serikali ya Zanzaibar, ambayo kupitia Shirika la Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), inamiliki Hisa Milioni 45 za CRDB, ambazo ni sawa na asilimia 1.6 ya hisa zote.

“Na kikubwa zaidi ni ukweli kwamba umiliki wa ZSSF umekua ukiongezeka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kutoka asilimia 0.03 mwaka 2021, hadi asilimia 1.4 mwaka 2022 na sasa mwaka jana ukafika asilimia 1.6.

“Na kwa hakika ongezeko la uwekezaji wa ZSSF ndani ya miaka mitatu iliyopita, linaakisi mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wako. Ongezeko hili halikuja tu hivi hivi, wawekezaji wetu hawa wametambua kuwa CRDB ni sehemu sahihi ya kuwekeza,” alisma Dk. Laay.

Aliongeza kuwa CRDB hutenga angalau asilimia 30 ya faida yake baada ya kodi kwa ajili ya kutoa gawio kwa wanahisa, ambapo mwaka 2023, ililipa gawio la Sh. 45 kwa kila hisa, kiasi ambacho sawa na ongezeko asilimia 25 ikilinganishwa na shilingi 36 zilizolipwa mwaka wa fedha 2022.

“Jumla ya gawio lililopokelewa na Serikali pamoja na taasisi zake katika kipindi hicho liliongezeka kutoka Sh. Bilioni 36 mwaka 2021 mpaka Sh. Bilioni 45.8,” alibainisha Dk. Laay.

 



No comments:

Post a Comment

Pages