Na Stephano Mango, Mbinga
MWENYEKITI
wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Desderius Haule amebainisha kuwa
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga itaendelea kutenga fedha za mapato ya
ndani kwa ajili ya ukamilishaji na utekelezaji wa miradi mipya
itayokwenda kuleta tija kwa wananchi.
Haule
amebainisha jana akijibu swali la Diwani wa Viti maalum Kata ya
Kihangimahuka Leonora Mwinuka katika mkutano wa baraza la madiwani
kujadili taarifa za robo ya tatu kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2024
lililouliza Je Halmashauri ina mkakati gani wa kukamilisha miradi
viporo.
Haule ameeleza
kuwa pamoja na shughuli nyingine utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni
kipaumbele cha Halmashauri katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Kwa
upande wake Katibu wa Baraza hilo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya
Wilaya ya Mbinga Joseph Rwiza ametoa rai kwa madiwani kushirikiana na
wataalam wa Halmashauri katika kukusanya mapato ili fedha hizo zitumike
katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Rwiza
amebainisha kuwa pamoja na vyanzo vya mapato vilivyopo,Halmashauri
inaendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza mapato pamoja na
kuondokana na utegemezi wa fedha kutoka Serikali Kuu pekee.
Akitoa
salamu za Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kisare Makori
amempongeza Mkurugenzi Mtendaji kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato na
kuvuka lengo la makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha
2023/2024.
Akichangia
mada katika Mkutano huo Diwani wa Kata ya Matiri Mhe. William Mbwambo
ametoa rai kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti UKIMWI kuona namna
bora ya kuwafikia wanawake wengi zaidi wakati wa zoezi la uchunguzi wa
saratani ya shingo ya kizazi.
No comments:
Post a Comment