HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 15, 2024

"MBINGA VIJIJINI TUTAENDELEA KUTENGA FEDHA KUTEKELEZA MIRADI YENYE TIJA KWA WANANCHI" HAULE

Na Stephano Mango, Mbinga 

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya  ya Mbinga  Desderius  Haule amebainisha kuwa Halmashauri  ya Wilaya  ya Mbinga itaendelea  kutenga fedha za mapato ya ndani  kwa ajili ya ukamilishaji  na utekelezaji wa  miradi mipya itayokwenda kuleta tija kwa wananchi.
Haule amebainisha jana akijibu swali la Diwani  wa Viti maalum Kata ya Kihangimahuka Leonora Mwinuka katika mkutano wa baraza la madiwani kujadili taarifa za robo ya tatu kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2024 lililouliza Je Halmashauri  ina mkakati gani wa kukamilisha miradi viporo.

Haule ameeleza  kuwa pamoja na shughuli nyingine  utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni kipaumbele cha Halmashauri  katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake Katibu wa Baraza hilo  Mkurugenzi Mtendaji  Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga  Joseph Rwiza ametoa rai kwa madiwani kushirikiana  na wataalam  wa Halmashauri katika kukusanya mapato ili fedha hizo zitumike katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

Rwiza amebainisha kuwa pamoja na vyanzo vya mapato vilivyopo,Halmashauri inaendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza mapato pamoja na  kuondokana na utegemezi wa fedha kutoka Serikali Kuu pekee.

Akitoa salamu  za Serikali,  Mkuu wa Wilaya  ya Mbinga Kisare Makori amempongeza Mkurugenzi Mtendaji  kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato  na kuvuka lengo la makisio  ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Akichangia mada katika Mkutano huo Diwani wa Kata ya Matiri Mhe. William  Mbwambo  ametoa rai kwa Mwenyekiti  wa Kamati ya  Kudhibiti UKIMWI kuona namna bora ya kuwafikia wanawake wengi zaidi wakati wa zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi.

 

No comments:

Post a Comment

Pages