Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum, Dk. Doroth Gwajima, (wa pili kulia) akiwashuhudia Afisa Mtendaji
Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt.Seif
Shekalage, wakibadilishana nyaraka baada ya kutiliana saini Mkataba wa
makubaliano ya mashirikiano ya kati ya Wizara na Benki ya NMB, wakati wa
hafla hiyo iliyofanyika leo Mei 6/2024 Makao Makuu ya Benki hiyo jijini
Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizra hiyo, Amon Mpanju.
NA MWANDISHI WETU
SERIKALI
imesaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na Benki ya NMB
yatakayoiwezesha benki hiyo kukopesha mikopo ya riba nafuu kwa
wafanyabiashara ndogondogo maarufu Machinga, ambao wametengewa kiasi cha
Sh. Bilioni 18.5 kwa mwaka wa kwanza kati ya miaka miwili ya
makubaliano hayo.
Makubaliano
hayo yamesainiwa jijini Dar es Salaam leo, Serikali kupitia Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, ikiwakilishwa na
Katibu Mkuu wake, Dk. Seif Shekalaghe, huku NMB ikiwakilishwa na Afisa
Mtendaji Mkuu wake, Ruth Zaipuna, wakishuhudiwa na Waziri, Dk. Dorothy
Gwajima.
Akizungumza
kabla ya kumkaribisha Waziri Dk. Gwajima, Dk. Shekalaghe alisema
Serikali wizara hiyo, inaendelea na usajili kwa ajili ya utambuzi wa
wafanyabiashara ndogondogo kote nchini na kuwapatia vitambulishio vya
kidijitali, ili kuwawezesha kukopa fedha hizo kwa riba ya asilimia 7 tu.
“Vitambulisho
hivi vya sasa ambavyo vitakuwa ni vya kidijitali, ni tofauti na vile
vya awali vilivyotolewa kwa Machinga, hivi vya sasa vitahusisha Namba ya
NIDA na maelezo mengine muhimu, ili kumpa fursa mfanyabiashara kukopa
sehemu ya fedha za Serikali zitakazolewa kupitia NMB,” alisema.
Katika
hotuba yake, Waziri Dk. Gwajima aliipongeza NMB kwa makubaliano hayo
yaliyokuja baada ya kushinda zabuni ya Serikali ya kuomba kupitishwa kwa
mikopo hiyo, huku akiwataka wafanyabiashara ndogondogo kuchangamkia
fursa ya kukopa kwa malenmgo na kurejesha kwa wakati.
“Mchakato
wa kupata benki ya kufanya nayo kazi ulikuwa na ushindani mkubwa,
lakini hatimaye NMB ilishinda zabuni hii. Hongereni sana NMB, lakini pia
pongezi nyingi kwa Dk. Seif Shekalaghe, kwa kuweka juhudi kubwa kwenye
kusukuma utekelezaji wa hatua zote zilizopelekea kufanikisha kusaini
makubaliano haya.
“Fedha,
hizi kiasi cha Shilingi Bilioni 18.5 zitakazotumika kutoa mikopo kwa
wafanyabiashara ndogondogo nchini, zimetolewa na Serikali ya Dk. Samia
Suluhu Hassan, ili ziweze kukopeshwa miongoni mwa wafanyabiashara hao na
amefanya hivi kwa kutambua umuhimu wa sekta hiyo.
“Sekta
hii inachangia sio tu katika kukuza Uchumi wa nchi, bali pia katika
kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana
wanaohitimu ngazi mbalimbali za elimu.
“Hivyo,
kutokana na umuhimu wa sekta hii, Serikali ya Dk. Samia, kupitia Wizara
yangu, imechukua hatua madhubuti ya kuhakikisha shughuli za kiuchumi za
wafanyabiashara hao nchini zinaimarishwa ikiwa ni pamoja na kuwapa
fursa ya kupata mikopo ya kuwawezesha kuinuka kiuchumi.
“Rais
alidhamiria kuimarisha ustawi wa wafanya biashara ndogondogo tangu
mwaka 2022 alipounda wizara na kuweka kundi hili kwenye wizara hii,
kisha akatoa fedha kwa ajili ya kujenga Ofisi za Machinga kila mkoa na
kuelekeza wapewe maeneo na hadi sasa mikoa 9 imekamilisha ujenzi na
mikoa mingine wanaendelea.
“Matarajio
ya Rais ni kuona fedha hii inakuwa endelevu na kuwafikia
wafanyabiashara ndogondogo wengi zaidi, Serikali haiku tayari kuona watu
wanakopa na kushindwa kurejesha fedha waliyokopeshwa, kwani kwa kufanya
hivyo watawanyima wengine fursa ya kukopa na kuboresha biashara zao,”
alisisitiza.
Kwa upande
wake, Bi. Zaipuna aliishukuru Serikali kwa kuichagua NMB kupitisha fedha
hizo kwa miaka miwili na kwamba benki yake ina uzoefu wa kutosha
kuhudumia kada hiyo, ambayo tayari wameshahudumu kwa kukopesha zaidi ya
Sh. Trilioni 2 kwa machinga na Bodaboda kote nchini.
“NMB
ina uzoefu mkubwa wa kuwahudumia wafanyabiashara ndogondogo, ambao
tangu mwaka 2020 hadi 2023, imetoa mikopo 129,540 yenye thamani ya Sh
Trillioni 2.03 kwa wajasiliamali wadogo wadogo wakiwemo machinga na
Bodaboda, ukiwa ni wastani mikopo 2,699 kila mwezi sawa na Sh Bilioni
42.3 kwa mwezi.
“Sekta ya
Biashara Ndogondogo na za Kati (SME) ina mchango mkubwa katika ukuaji
wa uchumi kwa nchi za Afrika na Duniani kwa ujumla, huku asilimia zaidi
ya 95 ya biashara zote rasmi zikiwa ni zile ndogondogo na za kati,
zikichangia takribani asilimia 50 ya Pato la Taifa kwa nchi za Afrika
Kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Pia
Biashara ndogo na za kati zinachangia zaidi ya asilimia 80 ya ajira
barani Afrika nah ii ni kwa mujibu wa takwimu zilizotokana na utafiti wa
Jukwaa la Uchumi Duniani,” alisisitiza Bi. Zaipuna.
Alibainisha
ya kwamba mikopo hiyo itakopeshwa kwa wafanyabiashara ndogo ndogo
waliosajiliwa na kutambulishwa na Wizara hiyo, na kwamba kabla ya
kuidhinisha mikopo, NMB itajiridhisha kwa kuwatembelea katika maeneo yao
ili kuhakikisha mikopo hii inawafikia walengwa.
“Mfanyabiashara
atakopeshwa kulingana na mahitaji ya biashara anayoifanya, ambapo NMB
kwa kushirikiana na Wizara itahakikisha wafanyabiashara hawa wanapatiwa
elimu ya kifedha ili kuhakikisha wanakuwa na nidhamu nzuri ya matumizi
ya mikopo na kukopa kwa malengo,” aliongeza.
No comments:
Post a Comment