HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 07, 2024

Serikali kupitia NMB kukopesha Bil. 18.5/- kwa Wafanyabiashara ndogondogo


Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Doroth Gwajima, (wa pili kulia) akiwashuhudia Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt.Seif Shekalage, wakibadilishana nyaraka baada ya kutiliana saini Mkataba wa makubaliano ya mashirikiano ya kati ya Wizara na Benki ya NMB, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo Mei 6/2024 Makao Makuu ya Benki hiyo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizra hiyo, Amon Mpanju.


NA MWANDISHI WETU
 

SERIKALI imesaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na Benki ya NMB yatakayoiwezesha benki hiyo kukopesha mikopo ya riba nafuu kwa wafanyabiashara ndogondogo maarufu Machinga, ambao wametengewa kiasi cha Sh. Bilioni 18.5 kwa mwaka wa kwanza kati ya miaka miwili ya makubaliano hayo.

Makubaliano hayo yamesainiwa jijini Dar es Salaam leo, Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, ikiwakilishwa na Katibu Mkuu wake, Dk. Seif Shekalaghe, huku NMB ikiwakilishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wake, Ruth Zaipuna, wakishuhudiwa na Waziri, Dk. Dorothy Gwajima.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Dk. Gwajima, Dk. Shekalaghe alisema Serikali wizara hiyo, inaendelea na usajili kwa ajili ya utambuzi wa wafanyabiashara ndogondogo kote nchini na kuwapatia vitambulishio vya kidijitali, ili kuwawezesha kukopa fedha hizo kwa riba ya asilimia 7 tu.

“Vitambulisho hivi vya sasa ambavyo vitakuwa ni vya kidijitali, ni tofauti na vile vya awali vilivyotolewa kwa Machinga, hivi vya sasa vitahusisha Namba ya NIDA na maelezo mengine muhimu, ili kumpa fursa mfanyabiashara kukopa sehemu ya fedha za Serikali zitakazolewa kupitia NMB,” alisema.
Katika hotuba yake, Waziri Dk. Gwajima aliipongeza NMB kwa makubaliano hayo yaliyokuja baada ya kushinda zabuni ya Serikali ya kuomba kupitishwa kwa mikopo hiyo, huku akiwataka wafanyabiashara ndogondogo kuchangamkia fursa ya kukopa kwa malenmgo na kurejesha kwa wakati.

“Mchakato wa kupata benki ya kufanya nayo kazi ulikuwa na ushindani mkubwa, lakini hatimaye NMB ilishinda zabuni hii. Hongereni sana NMB, lakini pia pongezi nyingi kwa Dk. Seif Shekalaghe, kwa kuweka juhudi kubwa kwenye kusukuma utekelezaji wa hatua zote zilizopelekea kufanikisha kusaini makubaliano haya.

“Fedha, hizi kiasi cha Shilingi Bilioni 18.5 zitakazotumika kutoa mikopo kwa wafanyabiashara ndogondogo nchini, zimetolewa na Serikali ya Dk. Samia Suluhu Hassan, ili ziweze kukopeshwa miongoni mwa wafanyabiashara hao na amefanya hivi kwa kutambua umuhimu wa sekta hiyo. 

“Sekta hii inachangia sio tu katika kukuza Uchumi wa nchi, bali pia katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana wanaohitimu ngazi mbalimbali za elimu.

“Hivyo, kutokana na umuhimu wa sekta hii, Serikali ya Dk. Samia, kupitia Wizara yangu, imechukua hatua madhubuti ya kuhakikisha shughuli za kiuchumi za wafanyabiashara hao nchini zinaimarishwa ikiwa ni pamoja na kuwapa fursa ya kupata mikopo ya kuwawezesha kuinuka kiuchumi.

“Rais alidhamiria kuimarisha ustawi wa wafanya biashara ndogondogo tangu mwaka 2022 alipounda wizara na kuweka kundi hili kwenye wizara hii, kisha akatoa fedha kwa ajili ya kujenga Ofisi za Machinga kila mkoa na kuelekeza wapewe maeneo na hadi sasa mikoa 9 imekamilisha ujenzi na mikoa mingine wanaendelea. 

“Matarajio ya Rais ni kuona fedha hii inakuwa endelevu na kuwafikia wafanyabiashara ndogondogo wengi zaidi, Serikali haiku tayari kuona watu wanakopa na kushindwa kurejesha fedha waliyokopeshwa, kwani kwa kufanya hivyo watawanyima wengine fursa ya kukopa na kuboresha biashara zao,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Bi. Zaipuna aliishukuru Serikali kwa kuichagua NMB kupitisha fedha hizo kwa miaka miwili na kwamba benki yake ina uzoefu wa kutosha kuhudumia kada hiyo, ambayo tayari wameshahudumu kwa kukopesha zaidi ya Sh. Trilioni 2 kwa machinga na Bodaboda kote nchini.

“NMB ina uzoefu mkubwa wa kuwahudumia wafanyabiashara ndogondogo, ambao tangu mwaka 2020 hadi 2023, imetoa mikopo 129,540 yenye thamani ya Sh Trillioni 2.03 kwa wajasiliamali wadogo wadogo wakiwemo machinga na Bodaboda, ukiwa ni wastani mikopo 2,699 kila mwezi sawa na Sh Bilioni 42.3 kwa mwezi.

“Sekta ya Biashara Ndogondogo na za Kati (SME) ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi kwa nchi za Afrika na Duniani kwa ujumla, huku asilimia zaidi ya 95 ya biashara zote rasmi zikiwa ni zile ndogondogo na za kati, zikichangia takribani asilimia 50 ya Pato la Taifa kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Pia Biashara ndogo na za kati zinachangia zaidi ya asilimia 80 ya ajira barani Afrika nah ii ni kwa mujibu wa takwimu zilizotokana na utafiti wa Jukwaa la Uchumi Duniani,” alisisitiza Bi. Zaipuna.

Alibainisha ya kwamba mikopo hiyo itakopeshwa kwa wafanyabiashara ndogo ndogo waliosajiliwa na kutambulishwa na Wizara hiyo, na kwamba kabla ya kuidhinisha mikopo, NMB itajiridhisha kwa kuwatembelea katika maeneo yao ili kuhakikisha mikopo hii inawafikia walengwa.


“Mfanyabiashara atakopeshwa kulingana na mahitaji ya biashara anayoifanya, ambapo NMB kwa kushirikiana na Wizara itahakikisha wafanyabiashara hawa wanapatiwa elimu ya kifedha ili kuhakikisha wanakuwa na nidhamu nzuri ya matumizi ya mikopo na kukopa kwa malengo,” aliongeza.

No comments:

Post a Comment

Pages