Na Mwandishi wetu, Kigoma
Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetaka watendaji wakati wa uboreshaji
wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura Mkoani Kigoma kuhakikisha wanatunza
vifaa vya uandikishaji ili vikaweze kutumika maeneo mengine nchini.
Hayo
yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa
Rufaa Jacobs Mwambegeke wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa
Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa
Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi
na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza leo tarehe 20 hadi 21
Juni,2024 Mkoani Kigoma.
“Kwa
kusisitiza, ni muhimu kutekeleza majukumu yenu kwa umakini katika kila
eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji hasa ikizingatiwa kuwa,
vifaa hivi vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana na vinatarajiwa kutumika
katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini,” alisema Jaji Mwambegele.
Amesema
kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi kutapelekea athari kubwa
katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu na amewataka kuzingatia
maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili muweze kuyafanyia kazi wakati
zoezi litakapokuwa limeanza.
Aidha,
Jaji Mwambegele amesema matokeo bora ya zoezi hili yanategemea uwepo wa
ushirikiano mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji, serikali,
vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi.
“Ninawasihi
muwe na ushirikiano mzuri na wa karibu na Tume wakati wote mtakapokuwa
mnatekeleza majukumu yenu na ikiwa mnahitaji ufafanuzi au maelekezo
yeyote, msisite kuwasiliana na Tume,” alimema Jaji Mwambegele.
Mapema
kabla ya kuanza mafunzo hayo, washiriki walikua kiapo cha kujitoa
uanachama na kile cha kutunza siri mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rose
Kangwa.
Mafunzo hayo
yanahusisha namna ya ujazaji wa fomu pamoja na kutumia mfumo wa
kuandikisha wapiga kura (Voters Registration System - VRS) ili waweze
kupata uelewa wa pamoja utakaowapa fursa ya kutumia kwa ufasaha mfumo
huo pamoja na vifaa vingine vya kuandikisha wapiga kura.
“Mafunzo
haya, yanawajengea umahiri wa kuwafundisha Maafisa Waandikishaji
Wasaidizi ngazi ya Kata kisha nao watatoa mafunzo hayo kwa Waendeshaji
wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi ambao ndio watahusika na
uandikishaji wa wapiga kura vituoni,” alisema Jaji Mwambegele.
Aidha,
Maafisa TEHAMA watapatiwa mafunzo maalum ya jinsi ya kukabiliana na
changamoto mbalimbali za kiufundi (Troubleshooting) endapo zitajitokeza
wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura vituoni.
Katika
hatua nyingine, Jaji Mwambegele amewaambia watendaji hao kuwa wakati
wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo
katika vituo vya kuandikisha wapiga kura jambo ambalo litasaidia kuleta
uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua
waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za
lazima.
Jaji Mwambegele
alitoa angalizo kwa mawakala hao kutoka vyama vya siasa kuwa
hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa
majukumu yao vituoni.
Tume
imetangaza uzinduzi wa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Mpiga Kura utafanyika tarehe 01 Julai, 2024 mkoani Kigoma ambapo Mgeni
rasmi anataraji kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa na kauli mbiu ya uboreshaji ni
“Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura Ni Msingi Wa Uchaguzi Bora”
No comments:
Post a Comment