July 19, 2024

Jeshi la Polisi Dar lamtia nguvuni Wakala wa Forodha tuhuma za Mauaji na Wizi

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema Juni 28, 2024 lilimkamata na kumuhoji kwa kina Mussa Khamis Bakari (Buda) miaka 30 wakala wa Forodha, Mkazi wa Temeke kwa tuhuma za mauaji ya Abdallah Twahir Selemani ambaye alikuwa rafiki yake.
Hayo yamebainishwa jijini humo na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema mtuhumiwa baada ya kumuua alifanikiwa kuiba pesa za marehemu shilingi Milioni 61 kutoka kwenye akaunti.

“Taarifa fupi za tukio ni kuwa tarehe 1 Mei, 2024 majira ya saa 10:20 asubuhi huko maeneo Mbutu Kichangani, Kigamboni pembezoni mwa barabara itokayo Cheka kuelekea Beach ya Kichangani uliokotwa mwili wa mtu mmoja mwanaume akiwa ameshafariki na baadae mwili huo ulitambuliwa kuwa ni Abdallah Twahir Selemani mkazi wa Chanika,” amesema SACP Muliro na kuongeza,

“Awali tarehe 4 Mei 2024 Jeshi la Polisi lilipokea taarifa ya kupotea kwa Abulllah Twahir Selemani kutoka kwa mama yake kuwa alipotea katika mazingira ya kutatanisha,”.

Kwamba uchunguzi wa Jeshi la Polisi baadae uligundua kuwa Aprili 30, 2024 mtuhumiwa Mussa Khamis Bakari (Buda) alikuwa na marehemu wakitumia gari namba T.928 DFY Suzuki Kei wakitokea Magomeni kuelekea Temeke, Kijichi mpaka eneo ulipokutwa mwili wa marehemu.

SACP Muliro amebainisha kuwa uchunguzi wa vitu mbalimbali umebainisha mtuhumiwa alimuua na baadae kwenda kutupa mwili huo pembezoni mwa barabara ulipookotwa.

Ameendelea kueleza kuwa baada ya kumuua, mtuhumiwa alichukua kadi ya benki ya marehemu na kwa nyakati tofauti tofauti alianza kutoa pesa kiasi cha shilingi Milioni 61 kutoka kwenye akaunti ya marehemu.

Amesema chanzo cha mauaji ni tamaa ya kutaka kuiba pesa kutoka kwa rafiki yake ambaye sasa ni marehemu na hivyo Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.

Katika tukio lingine Jeshi la Polisi limefuatilia matukio ya unyan’ganyi na wizi wa pikipiki katika Jiji la Dar es Salaam na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 23 na pikipiki 39 zilizoibwa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.

Amesema watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia mbinu ya kujifanya abiria na wakifika njiani hujitokeza watu wengine ambao humtishia dereva kwa mapanga kumjeruhi na kumuibia pikipiki hiyo, wakati mwingine pikipiki zinazokuwa zimeegeshwa nje hutumia mbinu ya kuunganisha waya, kuwasha na kuiba pikipiki hizo.

watuhumiwa hao baada ya kuziiba pikipiki wamekuwa wakiziuza kwa gharama nafuu mikoa mbalimbali ikiwemo Mikoa ya Dodoma na Singida.

Kwamba uutiliaji huo umefanikiwa kukamata risiti za kugushi 18 za kusafirishia pikipiki za wizi, kadi 11 za usajili wa pikipiki za kugushi, kadi (03) za usajili wa magari za kugushi, vyeti mbalimbali vya kuzaliwa na kimoja cha ndoa vya kugushi, plate number (03) za pikipiki, kitabu kimoja cha bima ya magari, nyaraka mbalimbali za TRA, barua mbalimbali zenye nembo za jeshi la Polisi Tanzania, mihuri mbalimbali ya manispaa ya Kinondoni,Temeke, IIala, Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, RITA, Mamlaka ya Bandari na mhuri mmoja wa moto ulioandikwa “United Republic of Tanzania” wenye nembo ya bibi na bwana, leaf 56 za kutengenezea kadi za vyombo vya moto, leaf 86 za kutengenezea vyeti vya vizazi na vifo vyenye nembo ya msajili wa vizazi na vifo.

Wakati huo huo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limekanusha taarifa ya sauti inayosambaaa kwenye mitandao ya kijamii ikielezea kuwepo kwa tukio la mwanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kutekwa nyara maeneo ya kituo cha kontena kilichopo ndani ya chuo hicho na watu wasiojulikana wakitumia usafiri wa bajaji kisha kupelekwa Kimara na baadae kutelekezwa eneo la Masaki.

Amesema Jeshi la Polisi limefanya ufuatiliaji wa taarifa hiyo na kubaini kuwa ujumbe huo wa sauti ni wa muda mrefu zaidi ya miaka mitano nyuma na uliwahi kusambazwa kama ulivyo na ufuatiliaji wake ulifanyika ikabainika kuwa hazikuwa habari za kweli.

Ameendelea kusema Polisi wamebaini pia tukio lililoelezwa kuwa kuna mtu aliuawa Sinza kisha kuondolewa ziwa upande wa kushoto na sehemu za siri, hazikuwa habari za kweli na hakuna tukio la namna hiyo kama linavyoelezwa.

“Kuzusha taarifa za uongo zenye lengo la kujenga taharuki au hofu ni makosa. Tunatahadharisha juu ya tabia hizo na Jeshi halitasita kuwatafuta na kuwahoji wanaohusika kwa hatua zaidi za kisheria,” ameongeza SACP Muliro.
Amesema Jeshi la Polisi pia katika kusimamia mifumo ya kisheria ya haki jinai limeendelea kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa matukio mbalimbali ya kihalifu na hatimaye kupatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu.

Akizungumzia kuhusu vitendo vya ubakaji na ulawiti, amesema Jeshi la Polisi limekuwa likichukizwa na vitendo vya ubakaji na ulawiti na katika hatua hiyo mwaka 2023 Juni, mshtakiwa Hussein Shomvi (50) fundi ujenzi, mkazi wa Chanika Zogoali alikamatwa na baadae kufikishwa Mahakama ya Kinyerezi na baada ya mashauri yake kusikilizwa tarehe 10 Juni 2024 alipatikana na hatia ya kosa kulawiti watoto wawili wa kiume wa shule ya msingi na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Washtakiwa wengine Shamim Hamadi (Dj Mush) (30) Mkazi wa Kimara Mwisho, na Waziri Ramadhani (26) Mkazi wa Mbezi Luis na Seif Salum (19) mkazi wa Manzese wote 3 kwa pamoja mwaka 2022 walifikishwa Mahakama ya Kinondoni mbele ya Hakimu Mkazi Nabwike Mbaba na baada ya mashauri yao kusikilizwa terehe 10 Juni 2024 walipatikana na hatia ya Unyangayi wa kutumia silaha na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela. Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa mbalimbali, zitatunzwa na wahusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria

No comments:

Post a Comment

Pages