NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
Mwenyekiti wa umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini amesema atahakikisha analivalia njuga suala la wanawake wajane kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili kupata fursa za mikopo.
Mgonja ameyabainisha hayo wakati akizungumza na baadhi ya wanawake wa UWT kutoka kata za Visiga pamoja na Misugusugu akiwa katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi yenye kuwapa ujasiri wanawake kugombea katika nafasi za uongozi.
Mwenyekiti huyo alisema kwamba katika ziara hiyo anatambua uwepo wa baadhi ya wanawake ambao ni wajane hivyo amewahimiza kujiunga katika makundi ya ujasiriamali ambayo itakuwa ni rahisi zaidi katika kupata mikopo.
"Nipo katika ziara ya kikazi katika kutembelea wanawake wa UWT kutoka kata zote 14 za Jimbo la kibaha mjini na leo nimetembelea kata ya Visiga na Misugusugu ikiwa ni kata ya kumi tangu nianze ziara yangu ,"alisema Mgonja.
Aliongeza kuwa ana imani wanawake wajane wakisapotiwa katika kupewa mitaji na mikopo wanaweza kufanya mambo makubwa na kuweza kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini.
Aliongeza kuwa kwa sasa lengo la UWT ni kuwa na siasa na uchumi hivyo atahakikisha anapambana kwa hali na mali ili kuwasaidia wajane kupata fursa za mikopo ya asilimia 10 ambayo inatolewa na serikali.
Katika hatua nyingine alisema atahakikisha kwamba anawalinda na kuwatunza kwa hali na mali wanawake wajane ambao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya unyanyasaji na kwamba atashirikiana na vyombo vya dola katika jambo hilo.
Kwa upande wake Katibu wa UWT kata ya Visiga alimpongeza Mwenyekiti wa Wilaya kwa ziara yake ya kutembelea wanawake kwa ajili ya kuwahimiza kujitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya uchaguzi.
Nao baadhi ya waheshimiwa madiwani wa halmashauri ya Kibaha mjini hawakusita kuwapa ujasiri kwa wanawake hao kutoogopa kugombea katika nafasi za uongozi hasa katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Baadhi ya wanawake wajane wamesema kwamba wapo tayari kuwezeshwa mitaji pamoja na mikopo na kwamba wakiwezeshwa wanaweza kuondokana na kuwa tegemezi.
Ziara ya mwenyekiti wa umoja wa wanawake (UWT) hadi sasa imefanyika katika kata kumi ambapo leo imefanyika katika kata ya Visiga na Viziwaviza.
No comments:
Post a Comment