Katibu tawala wa Wilaya ya Magu Jubilate win Lawuo akishiriki zoezi la usafi wa mazingira katika eneo la hospitali ya Wilaya ya Magu ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya mashujaa Julai 25/2024.
Katika
kuadhimisha siku ya mashujaa Julai 25, 2024 viongozi wa Serikali,
Viongozi wa Dini, watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Kamati ya
Ulinzi na Usalama na wananchi wameshiriki zoezi la usafi wa mazingira
katika eneo la hospitali ya Wilaya ya Magu ikiwa ni sehemu ya
kuadhimisha siku hiyo ambayo huenzi na kukumbuka mazuri yaliyofanywa na
mashujaa wetu wa Tanzania.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo
Katibu Tawala wa Wilaya ya Magu Jubilate win Lawuo ametoa wito kwa
wananchi wa Magu kuendelea kuwaenzi mashujaa kwa kua wazalendo na
kulinda amani ya nchi kwani ndo msingi wa maendeleo ya Taifa letu.
Amesema
watanzania wote wanatakiwa kuienzi misingi imara ya kizalendo amani na
upendo iliyojengwa na waasisi wa Taifa letu ikiongozwa na Baba wa Taifa
Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume,
misingi ambayo matunda yake tunayafaidi watanzania wote na tujipange
kurithisha kwa vizazi vijavyo.
"Tumekuja hapa kwa ajili ya
kumbukumbu ya wazalendo wetu waliojitoa kipindi hicho katika kulipigania
Taifa letu na matunda yake tunayaona hadi leo na vizazi vyetu vutakuja
kufaidi matunda haya" amesema DAS Lawuo.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mohamed Ramadhani
amesema Magu inawakumbuka mashujaa kwa kujitoa kwao na kusababisha Taifa
kupata ukombozi ambao hadi leo watanzania wanaendelea kufaidi matunda
yaliyotokana na kujitoa kwao. Funzo kwetu ni kuwa wazalendo kwa nchi
yetu kama walivyokuwa Mashujaa wetu ambao walijitoa kwa hali na mali.
Aidha
amesema kuwa mbali na kuwakumbuka Mashujaa waliopigania Uhuru pia usafi
huo umekua ni sehemu ya kuwakumbusha Wananchi kutunza mazingira ya
Wilaya kwa ajili ya afya ya Jamii huku akiwahimiza kufanya usafi kuwa
sehemu ya maisha yao ya kila siku na sio kusubiri matukio maalumu.
Akizungumza
kwa niaba ya viongozi wa Dini Shekh wa Kata ya Isandula Majaliwa Rashid
akimwakilisha Shekh Mkuu wa Wilaya ya Magu amesema viongozi wa dini
wataendelea kuwakumbuka mashujaa kwa kuwaombea dua kwa mazuri
waliyofanya na kusema kuwa wataendelea kuliombea Taifa liendelee kuwa na
amani, upendo na mshikamano.
Kila ifikiapo Julai 25 ya kila
Mwaka,Tanzania huadhimisha siku ya kuwakumbuka Mashujaa waliopoteza
Maisha yao wakiutetea, Kuupigania na Kulinda Uhuru wa Tanzania. Kwa
upande wa Wilaya ya Magu Siku hii pia imeambatana na Shughuli
mbalimbali ikiwemo dua na sala maalumu za kuwaombea Mashujaa waliopoteza
maisha yao na walio hai na kuiombea Amani ya Nchi yetu iendelee
kudumu.
No comments:
Post a Comment